Social Icons

Saturday, 7 February 2015

Hadithi: Familia tata - 17


WAKAMALIZA vinywaji vyao, wakaanza kuliekea gari. Asfat akaomba aendeshe yeye, Festo akamruhusu, akazunguka kushoto, akimuacha msichana akielekea kulia.

Asfat aliliondoa gari taratibu na kuliingiza barabarani, akaanza safari ya kuelekea nyumbani kwao, Nakasangwe.
 Akili yake yote ilipanga kumuangamiza Festo katika mteremko unaotoka kwa Mzee Mathias kuelekea nyumbani kwao. Kulikuwa na mtaro ambao alidhamiria uwe mwisho wake.

Kila mtu alikuwa kimya, Festo alirejesha kumbukumbu za jinsi alivyotumia muda wake na msichana huyo, miguu yake ikiwa juu ya dash-board, viatu akiwa amevivua. Alifumba macho katika staili flani ya kuuita usingizi. Macho ya Asfat yalikuwa barabarani, akiyakwepa mashimo ya maji, pamoja na mifereji iliyochimbwa kwa ajili ya kupitisha mabomba ya maji kila baada ya urefu mfupi.

Alipofika eneo hilo la kwa Mzee Mathias, wakielekea katika mteremko mkali, Festo akiwa anasinzia, Asfat akaongeza mwendo, akaifuata nguzo moja kubwa ya zege, iliyojengwa kutenganisha ukuta wa shule ya sekondari ya Maendeleo na makazi ya wananchi. Nguzo ilikuwa upande wa Festo, akiwa ameuma meno, akalilenga gari usawa ule ule aliokaa Festo! 

Kishindo kikubwa kikasikika, kikafuatiwa na makelele ya gari kukosa mwelekeo na baadaye kidogo, gari hilo likaishia kwenye mtaro ambapo pia lilitoa mshindo mkubwa!!!!!
***
Mama Tonny alikuwa amesubiri sana chips alizomuagiza Asfat, akaona muda unayoyoma. Kwa akili ya utu uzima, hakutaka kujisumbua kumpigia simu kumkumbusha, alijua mwanaye ameshakuwa mtu mzima, mambo mengine siyo ya kumfuatilia sana, akaamua kuingia chumbani kwake kulala.

Na hata alipoungana na mumewe chumbani, hakusema lolote kuhusiana na Asfat. Hawakuwa na kawaida ya kuwaulizia watoto wao, hasa wakubwa, kwani huo ulikuwa ni wakati wao na wenyewe waliamua kuishi maisha hayo. Waliamini vijana wao wanao uwezo wa kujisimamia wenyewe na hivyo ndivyo walivyoishi, hawakuwahi kusikia matatizo yoyote kwao, kuhusiana na maisha yao nje ya nyumba.

Walizungumza mambo yao ya maisha, mipango endelevu ya kipato cha familia yao na hatimaye wakaingia kwenye ulimwengu mwingine usiosimulika, kabla ya kila mmoja kupitiwa na usingizi!!
***
Kevin, kijana mwenye umri wa miaka 19, bitozi, jirani yao akina Festo, alikuwa amejibanza kwenye ukuta wa moja ya nyumba za maeneo hayo, akiwa anazungumza na msichana mpenzi wake, Munira. Hawa ni wapenzi wa muda mrefu, lakini muda mwingi hawako pamoja kwa vile msichana alikuwa akisoma Arusha, katika shule ya kimataifa ya Tanganyika wakati Kevin, ambaye mtaani alifahamika kama Kev, alikuwa akisoma Morogoro High School.

Wakiwa wamekumbatiana ukutani hapo, walisikia gari dogo likiendeshwa kwa mwendo wa kasi kuteremka kuelekea eneo la makazi yao. Mwendo ule uliwatisha, wakaachiana…
“Munny, wale watakuwa ni majambazi wametoka kufanya uhalifu, ule mwendo hawafiki,” Kev alimwambia mpenzi wake, wakiliangalia gari hilo lilivyokuwa likishuka kwa mwendo mkali na wa kutisha.
“Kev, Kev wanakufa hao jamani,” Munira alimwambia mwenzake, sasa akiwa amemkumbatia kwa nguvu, huku akihema!!!
***
Kishindo kile kilikuwa ni kikubwa sana, kilisikika kwa nguvu kwa kila mmoja. Baba na Mama yake Tonny walishtuka usingizini kutokana na mlio ule wa kutisha, wakazi wengine wote wa eneo lile nao walisikia.

Ingawa ulikuwa ni usiku, vumbi kubwa lilionekana kutokea eneo la ajali. Watu wakaanza kusogea taratibu. Kulikuwa kimya, hakuna mtu aliyeonekana ametoka, hakuna sauti iliyosikika kuomba msaada. Wakazidi kusogea, tochi zikiwaka, zikasogea zaidi na kulikuta gari limelala mtaroni!

Je nini kimetokea? Kuna usalama wowote kwa walio ndani ya gari? Usikose kufuatilia katika toleo lijalo ujue kinachoendelea katika simulizi hii ya kusisimua.


Chanzo: Globalpublishers

No comments:

 
 
Blogger Templates