Social Icons

Sunday, 8 February 2015

Vita ya Mbatia na Mrema sasa moto


Dar/Dodoma. Vita ya ubunge baina ya wenyeviti wawili wa vyama vya upinzani, James Mbatia na Augustine Mrema imezidi kupamba moto baada ya kushambuliana bungeni kuhusu kusigana kwenye harakati za ubunge wa Jimbo la Vunjo.

Kwenye vikao vya Bunge na nje, Mrema, mwenyekiti wa TLP, amekuwa akimlalamikia Mbatia (NCCR-Mageuzi) kuwa anamuingilia kwenye jimbo lake, lakini juzi alikwenda mbali zaidi alipoomba kuwasilisha taarifa ya hali yake kiafya na kutumia nafasi hiyo kumshambulia mpinzani wake, ambaye pia jana aliomba nafasi kama hiyo kujibu mapigo.

Msuguano wa wawili hao, ambao waliwahi kuwa pamoja kwenye Chama cha NCCR, ulitokana na uamuzi wa Mbatia kutangaza nia ya kugombea ubunge wa Vunjo, jimbo ambalo kwa vipindi viwili limekuwa chini ya Mrema.

Juzi usiku, Mrema, ambaye pia amewahi kuwa mbunge wa Jimbo la Temeke, alisoma taarifa hiyo ya hali yake ya afya akisema kuwa yeye si mgonjwa kama inavyodaiwa na atagombea tena ubunge kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Katika taarifa yake aliyoimbatanisha na ripoti za madaktari kuhusu vipimo alivyofanya na ambayo alitumia dakika 15 kuisoma, Mrema alimtuhumu Mbatia kwamba amevamia jimbo hilo na kuwambia watu wasiwachague wagombea wa TLP, akiwamo na yeye (Mrema) kwa sababu ni marehemu mtarajiwa, ana saratani na Virusi vya Ukimwi.

Akieleza jinsi Rais Jakaya Kikwete na Spika Anne Makinda walivyofanikisha safari zake za kwenda nchini India, kuchunguzwa afya yake, kutibiwa saratani ya mapafu pamoja na kupima Ukimwi, Mrema alisema: “Awali nilikuwa na saratani ya mapafu, lakini baada ya kupata matibabu kwa mwaka mmoja, nimepima tena na ripoti za madaktari zinaonyesha kuwa nimepona.

“Nilipima na ukimwi na vipimo vimeonyesha sina maambukizi yoyote. Kweli Mungu mkubwa. Hafi mtu hapa. Mimi ni mzima wa afya na nitagombea ubunge maana ndiyo unanitoa roho.”

Hata hivyo, Mbatia, ambaye ni mbunge wa kuteuliwa na Rais, jana jioni alikanusha madai hayo bungeni akisema hayana ukweli wowote.

“Sijawahi kumnyanyapaa mtu mwenye Ukimwi. Kuzeeka hakuna mjadala ila kuwa na busara ni uamuzi tu. Hakuna mwenye hati miliki ya uongozi, wenye hati miliki ni wananchi,” alisema.

Mbatia alitangaza nia hiyo ya kugombea ubunge wa Vunjo Julai 29, mwaka jana, ikiwa ni siku moja baada ya wafuasi wa vyama vya CCM, Chadema, NCCR-Mageuzi na TLP kumwita jimboni humo, wakimtaka achukue uamuzi mgumu ya kurejea nyumbani kugombea ubunge. Mbatia amewahi kuwa mbunge wa jimbo hilo mwaka 1995 hadi 2000.

Akifafanua madai yake juzi, Mrema alidai Desemba mwaka jana akiwa katika matibabu India, Mbatia na wapambe wake ambao ‘wamepiga kambi’ katika jimbo hilo, walitumia mwanya huo kufanya mikutano ya hadhara waliyoipa jina la Delete TLP (futa TLP), kuwaeleza wananchi kuwa yeye (Mrema) ni marehemu mtarajiwa, hivyo hatakiwi kuchaguliwa kuwa mbunge.

“Waliwashawishi wananchi kutochagua wagombea wa TLP katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Vitongoji kwa sababu ya afya yangu. Mbatia anataka yeye ndiyo achaguliwe kwa kuwa ana afya nzuri,” alisisitiza. Mrema alisema muda wa kampeni haujafika na wala jimbo la Vunjo halijatangazwa na serikali kuwa lipo wazi, hivyo kitendo cha Mbatia kuanza kampeni mapema ni kinyume na Sheria ya Uchaguzi.

Chanzo: Mwananchi

No comments:

 
 
Blogger Templates