Social Icons

Sunday, 8 February 2015

Hadithi: Familia tata - 19


“Mimi nilikuwa kwa shangazi Boko kama nilivyoaga pale, jamani anakusalimu sana, ila kidogo hali yake goigoi maana alikuwa na homa,” Mama Tony alimwambia mwenzake huku wameshikana mikono, macho yao yalipokutana, kila mmoja alionekana kuamini kuondoka kwa tofauti kati yao.
Sasa endelea...

Maisha ya familia zile mbili yalirejea katika hali yake ya kawaida kama mwanzo, ingawa kulikuwa na aina flani ya hofu kwa kila mwanafamilia. Hisia za kuwa mauaji ya mwisho yalikuwa ni ya kupangwa, yaliendelea kubakia moyoni mwa akina mama wale ambao hata hivyo, waliamua kusamehe kama walivyoahidi.

Marafiki wawili, wao hawakuwa hata na chembe ya mawazo hayo, waliamini kabisa vifo vya watoto wao vilitokea kwa mipango ya Mwenyezi Mungu na si vinginevyo. 
Lakini hali ilikuwa tofauti kabisa kwa Stone, kijana aliyekuwa na mwili mkubwa, mpole na asiyependa kuzungumza sana.

Alikuwa na hasira na alitaka kulipiza kisasi. Kisasi chake akihamishie kwa nani ndilo lilikuwa tatizo lake kubwa.

Familia ya Mzee Linus ilisaliwa na watoto watatu, Tonny ambaye ni mdogo kabisa, Maria aliyekuwa na umri kama wa Stone na ambaye alikuwa ndiye mtoto mkubwa pamoja na Ziggy aliyemfuatia. Ingawa familia zao zilikuwa marafiki, Stone hakuwahi kuwa karibu na yeyote kutoka kwa mzee Linus, zaidi ya kuheshimiana na kushirikiana kwenye matatizo na furaha.

“Huyu mama ninamtamani sana kwa sababu najua alikuwa karibu na mwanaye, lazima walishirikiana kupanga mauaji,” Stone aliwaza, akiwa chumbani kwake, wakati akitazama taarifa ya habari ya televisheni.

Lakini pia Tonny, aliyehusika na kifo cha dada yake, Judy, naye aliingia katika orodha. Ingawa aliendelea kuamini kuwa kifo cha ndugu yake yule kilitokea kwa bahati mbaya kweli, lakini muendelezo wa matukio ulimkuta akianza kumchukia mtoto huyo.

“Anyway, ili kwenda sawa, nitawaua wote wawili,” alijikuta akisema kwa sauti. Ghafla, akajikuta akivaa sura ya ukatili, akatamani kuufanya unyama wakati uleule. Akapiga magoti na kupiga ishara ya msalaba, akauzuia uso wake kwa mikono yake, akajikuta akibubujikwa na machozi!
***
Mwaka mmoja ulishapita sasa tokea vifo vya Asfat na Festo. Kila mmoja aliamini kutokuwepo kwa tatizo lolote baina ya wanafamilia, bila kujua kwamba kulikuwa na mtu mmoja miongoni mwao aliyekuwa na malengo ya ajabu.

Kila siku, roho ya Stone ilizidi kuwa mbaya, akatamani kufanya mauaji ya kisasi muda ule ule, lakini jinsi gani atafanya, ili asinaswe, lilikuwa ndilo tatizo kubwa. Mara mbili alishawahi kumvizia Tonny anaporudi toka shule, lakini mara zote aliambatana na wenzake.

Kijana huyo alikuwa na kituo maalum ambacho gari la shule yao lilikuwa likiwashusha. Kuanzia hapo kulikuwa na mwendo kiasi hadi kufika nyumbani kwao. Kabla ya kufika kwao, kulikuwa na vichochoro viwili ambavyo Stone angeweza kumfanyizia.

Stone akaamua kuanza na mikakati thabiti ya kumuua kwanza Tonny, kwa sababu ni rahisi. Akadhamiria kulifanya zoezi lile mapema iwezekanavyo. Alihitaji kuwa peke yake, tena bila silaha. Angeweza kumkaba shingo na kumuua au hata kumpiga ngumi kadhaa shingoni.

Alikuwa na uwezo huo kwa sababu Stone alikuwa ananyenyua vyuma na anafanya mazoezi ya ngumi, alishiba kweli kweli na vijana wengi walimuogopa. Siku hiyo akadhamiria kufanya kweli!
Ilipofika saa moja kasoro, muda ambao Tonny huwa anashuka ndani ya gari lao, akawa maeneo ya karibu amejificha.

Dakika chache baadaye, gari la shule likafika, na kama bahati kwa Stone, kijana yule alishuka peke yake.
Tonny akaanza kutembea taratibu kuelekea kwao, kichwani mwake akifikiria jinsi gani atafanikiwa kufanya home work ya hesabu, somo alilokuwa analichukia kuliko yote, ingawa darasani kwao, yeye ndiye alionekana kiboko yao kwa hesabu.

Akapita uchochoro wa kwanza bila kukutana na mtu, akakaza mwendo maana giza lilishaanza kuingia…

Je, nini kitatokea? Usikose kufuatilia simulizi hii ya kusisimua katika toleo lijalo.

Chanzo: Globalpublisher


No comments:

 
 
Blogger Templates