Miongo kadhaa ya ukame wa taji la kombe la Afrika unakaribia kufikia mwisho, kati ya Cote D'Ivoire na Ghana, lakini timu moja itaendelea na kilio hicho leo Jumapili(08.02.2015) katika fainali ya kombe hilo mjini Bata.
Cote D'Ivoire inapambana na Ghana leo Jumapili katika uwanja wa mjini Bata katika fainali, na timu zote zinawania hatimaye kushinda taji hilo la bara la Afrika baada ya miaka kadhaa ya kulikosa chupu chupu.
"Ni fainali inayopambanisha timu mbili nzuri, timu mbili zenye uwezo mkubwa katika soka la Afrika kwa muda mrefu sana, "kocha wa Cote D'Ivoire Herve Renard amesema siku ya Jumamosi. "Tunafahamu haitakuwa rahisi."
Tembo wa Cote D'Ivoire waliingia katika mashindano haya kama moja ya timu zinazopigiwa upatu kutoroka na taji hili kwasababu ya wingi wa nyota katika kikosi chake, ambacho kinajumuisha Yaya Toure, Wilfried Bony na Gervinho. Lakini wanamkosa Didier Drogba, ambaye alitundika madaluga kwa kikosi hicho.
Tembo wanakomsa Drogba
Wakiwa na Drogba , Tembo wa Cote D'Ivoire , walifikia fainali ya kombe la mataifa ya Afrika mwaka 2006 na mwaka 2012, wakipoteza michezo yote katika mikwaju ya penalti. Ushindi pekee wa kikosi hicho ulikuwa mwaka 1992, wakati walipoishinda Ghana kwa mikwaju 11-10 ya penalti.
"Huo ni wakati wetu uliopita," amesema mlinzi wa Cote D'Ivoire Wilfried Kanon. "Hivi sasa , wakati tuliokuwa nao ni kesho(leo), na hatutaki kuipoteza nafasi hii."
Ghana mabingwa mara nne
Mabingwa mara nne wa kombe la mataifa ya Afrika Ghana pia imekuwa moja kati ya timu bora kabisa katika bara hilo katika miaka ya hivi karibuni, lakini ilishinda mara ya mwisho kombe la Afrika mwaka 1982.
Kikosi cha hivi karibuni kabisa kilifikia robo fainali ya kombe la dunia mwaka 2010 na baadaye fainali ya kombe la mataifa ya Afrika miezi michache baadaye.
Leo wakiwa katika fainali yao ya tisa, moja zaidi ya mabingwa mara saba Misri , Black Stras wana kikosi chao cha nyota, ikiwa ni pamoja na Asamoah Gyan, Christian Atsu na Andre Ayew.
Gyan , ambaye aliumia wiki iliyopita katika mchezo wa robo fainali ambapo timu hiyo ilishinda dhidi ya Guinea na kukosa mchezo wa nusu fainali dhidi ya Guinea ya Ikweta , huenda asiwe fiti vya kutosha katika mchezo wa leo Jumapili(ß8.02.2015).
Lakini Ayew yu tayari.
"Najaribu kuinua kiwango cha mchezo wangu juu na juu zaidi kila wakati, " Ayew amesema. "Kitu muhimu ni kesho(leo)."
DRCongo yanyakua nafasi ya tatu
Wakati huo huo Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo imefanikiwa kushika nafasi ya tatu katika mashindano haya baada ya kuishinda Guinea ya Ikweta kwa mabao 4-2 kwa mikwaju ya penalti.
Timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana kwa dakika 120, katika uwanja wa Estadio de Malabo uwanja huo ukiwa kimya kutokana na ghasia za mashabiki wa Guinea ya Ikweta katika mchezo wa nusu fainali dhidi ya Ghana.
Javier balboa na Raul Fabrini walikosa mikwaju yao wakati DRCongo ikishinda kwa mikwaju 4-2.
Vyombo vya habari vyakosolewa
Nae rais wa shirikisho la kandanda duniani FIFA Sepp Blatter na mwenyekiti wa shirikisho la kandanda barani Afrika Issa Hayatou wamevishutumu vyombo vya habari vya mataifa ya magharibi kwa kuichukulia kama kashfa ghasia zilizofanyawa na mashabiki wa Guinea ya Ikweta na kuchafua heba ya mashindano ya kombe la mataifa ya Afrika katika mchezo wa nusu fainali kati ya Ghana na Guinea ya Ikweta.
Vitu mbali mbali pamoja na chupa za maji zilirushwa kwa wachezaji na mashabiki wa Ghana, helikopta ya Polisi iliitwa kutoa msaada na kuwatawanya mashabiki uwanjani na mzozo uliendelea nje ya uwanja baada ya mchezo huo ambao ulicheleweshwa kwa zaidi ya nusu saa kabla ya Ghana kushinda kwa mabao 3-0.
"habari nzuri sio habari nzuri, habari mbaya ndio habari, " Blatter amewaambia waandishi habari siku ya Jumamosi katika utiaji saini makubaliano ya ushirika kati ya FIFA na shirikisho la CAF.
Tunazungumza tu kuhusu mabaya, Soka, ambayo ni kitu kizuri, kiache kiendelee, muuache mchezo wa mpira uendelee kwa amani, unatayarishwa vizuri, waache waendelee nao.
Sioni upande hasi wa kandanda ya Afrika ambayo vyombo vya habari vinataka kuonesha," Blatter ameongeza. " Nikawaida, tunakosoa kile kizuri, bila kufanya hivyo kwa kibaya. Jukumu ambalo halipendezi la vyombo vya habari ni kudhani na kutabiri.
Rais wa CAF pia amevikosoa vyombo vya habari kwa kukuza mambo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / ape
Chanzo: Dw.de
No comments:
Post a Comment