Alipotokeza tu nje ya geti la nyumba yake akiwa na Tonny, macho yake yakatua kwa Stone, aliyekuwa amesimama upande wa pili wa barabara, taa kutoka nyumba za mtaani zilimfanya aonekane bila kikwazo.
Sasa endelea...
Kwa mara ya kwanza tokea azaliwe, mzee Linusu alishtuka na mapigo ya moyo wake yakaanza kupiga harakaharaka. Alimkazia macho kijana yule wa jirani, ambaye naye alionekana kuwa bize na simu yake, akiwa hajishughulishi na mtu yeyote. Tonny naye alishtuka alipomuona Stone lakini akapiga moyo konde akaungana na baba yake kuelekea kwa mzee Komba.
Wakatoka na kupiga hatua kadhaa mbele hadi walipofika getini kwa mzee Komba. Hawakugonga, walilisukuma na kutokezea ndani ambako walikutana na mwanga mkali wa taa za sebuleni. Kwa kuwa walikuwa wenyeji, walisukuma mlango na kuingia ndani ambako walimkuta mzee Komba akiwa amekaa na mkewe. Ingawa walikuwa wamezoeana sana, lakini ujio huu uliwashtua kidogo, wote wakasimama kuwapokea.
“Karibuni, karibuni sana,” alisema mzee Komba huku akimpa mkono mzee mwenzake na baadaye Tonny.
“Asante ndugu yangu, tumekaribia,” alisema mzee Linus na kutoa nafasi kwa Tonny ambaye aliwaamkia wazee wale kisha kukaa kwenye sofa kubwa.
Hakutaka kupoteza muda, mara moja akaanza kusimulia kitu kilichowapeleka pale. Mzee Komba na mkewe walisikiliza kwa makini na kwa mbali, wakaanza kuhisi hatari, maneno ya baba yake Tonny yalikuwa na viashiria vya uvunjifu wa amani.
Baada ya kutoa maelezo hayo, wazazi wake Stone wakabakia wapole, hawakujua waanzie wapi, lakini maneno yale yaliwaingia vizuri na kwa kupima mazingira, hata wao waliona dhamira isiyo nzuri kwa mtoto wao.
***
Stone alipotazama simu yake ya mkononi ili kujua nani anapiga, akajikuta akitamka kwa sauti kidogo.
“Kimenuka” alisema na kupokea simu ya baba yake ambaye bila kumsabahi wala nini, alimtaka kuingia ndani mara moja. Dakika moja baadaye, akaingia sebuleni na kuungana na watu aliowakuta.
“Stone una lolote la kutuambia kuhusu kilichotokea usiku huu wewe na huyu mdogo wako,” baba yake alimwuliza kwa taratibu.
“Tulikuwa tumeongozana wakati tunarudi nyumbani, lakini hatukuongea,” Stone alisema kwa ufupi.
“Nimesikiliza maelezo yake hapa, inaonekana kama kuna kitu kibaya ulitaka kumfanyia, kwa sababu mwanga wa gari ulipowamulika, ulikuwa hatua mbili tu nyuma yake na hakuweza kukusikia wakati ukimsogelea, ulitaka kufanya nini?” baba yake alimwuliza tena.
“Nilikuwa nataka kumtania kwa kumtisha,” Stone naye alisema, lakini uso wake ulionyesha wazi alichokisema hakikufanana na moyo wake.
“Stone, kuna mambo mengi yametokea katika familia zetu hizi, mimi siwezi kukulazimisha useme, lakini naungana na hawa kuwa haukuwa na nia njema kwa Tonny, kama ulikuwa na lengo lolote baya, nakuomba sana mwanangu uliache, hatupo tayari kuona mtu anatuliza makusudi,” alisema baba yake na kumtaka kuondoka sebuleni.
Stone akasimama bila kusema neno na kuingia chumbani kwake.
Mazungumzo mafupi yaliendelea pale sebuleni kabla ya wageni kuaga na kuondoka. Walipofika nje, hawakuingia ndani kwao, bali walipitiliza na kwenda kuchukua Bodaboda, wakapanda kuelekea Kituo cha Polisi cha Wazo.
Katika kaunta ya Polisi, Tonny alianza kuwasimulia askari wawili waliokuwa wakiwahudumia. Baada ya maelezo yake, askari akawauliza maswali kadhaa na kuwaambia wanaweza kuondoka kuelekea nyumbani, lakini wawe makini kwa muda wote.
Saa tano kamili za usiku, geti la mzee Komba likagongwa. Ugongwaji wake ulionyesha ni wa mtu mgeni, kwani ulikuwa ni kwa sauti kubwa. Kwa kuwa alikuwa bado sebuleni wakiwa na mkewe wakiendelea kulizungumzia sakata lile, yeye mwenyewe akasimama na kwenda kufungua.
Ni polisi.
Je, nini kitatokea? Usikose kufuatilia simulizi hii ya kusisimua wiki ijayo.
Chanzo: Globalpublishers
No comments:
Post a Comment