Viongozi wa Ukraine, Ujerumani na Ufaransa wanashinikiza juu ya mkutano wa kilele pamoja na Rais Vladimir Putin wa Urusi Jumatano, katika jitihada ya kusitisha umwagaji damu Mashariki mwa Ukraine.
Rais wa Ukraine Petro Poroshenko, Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel na Makamo wa Rais wa Marekani Joe Biden
Viongozi hao wanne walizungumzia mkutano huo wakati wa mazungumzo yao ya simu jana, kama sehemu ya kupata suluhisho la kudumu katika mzozo huo baina ya majeshi ya Ukraine na waasi wanaiunga mkono Urusi. Hayo yameripootiwa wakati kansela wa Ujerumani Angela Merkel akiwa Washington kwa mazungumzo baadae leo na Rais Barack Obama.
Onyo la rais Putin wa Urusi
Rais wa Urusi Vladmir Putin hata hivyo ameonya kwamba Mkutano wa kilele unaopangwa na viongozi wenzake watatu, Angela Merkel wa Ujwerumani Francois Hollande wa Ufaransa na Petro Poroshenko wa Ukraine katika mji mkuu wa Belaruss-Minsk, utaweza tu kufanyika, ikiwa watakubaliana dondoo kadhaa za kujadiliwa hadi wakati huo. Putin aliyasema hayo wakati alipokutana na Rais wa Belaruss Alexander Lukashenko Jumapili.
Kansela Merkel na Rais Hollande walisafiri pamoja kwenda kwanza Kiev kwa mazungumzo na Rais Poroshenko na baadae Moscow kuzungumza na Rais Putin, ambaye nchi za magharibi zinamshutumu kuwa yuko nyuma ya mgogoro wa miezi 10 sasa nchini Ukraine. Leo (Jumatatu) maafisa wa wizara za mambo ya nchi za nje za nchi hizo nne watakutana mjini Berlin kuandaa mazungumzo hayon kati ya viongozi hao wanne hapo jumatano, wakati Kansela Merkel akimuarifu Rais Obama leo juu ya juhudi mpya za amani, wakati watakapokutana Ikulu mjini Washington.
Shinikizo kwa serikali ya Marekani
Obama anakabiliwa na shinikizo zaidi kumtaka kuisaidia kwa silaha serikali ya Ukraine ili kuliimarisha jeshi lake linalokumbwa na hali ngumu katika mapambano na waasi wanaotaka kujitenga Mashariki mwa nchi hiyo.
Lakini Merkel na mataifa mengi ya Ulaya yanaamini silaha haziwezi kubadili mkondo wa vita hivyo, badala yake kuvifanya vipambe moto zaidi.
Wakati huo huo mapigano mapya Ukraine yamesababisha vifo vya raia 12. Duru za serikali na wale wanaotaka kujitenga zimearifu pia kwamba wanajeshi 12 wa Ukraine wameuwawa katika saa 24 zilizopita.Mgogoro huo wa Ukraine imeshawauwa karibu watu 5,400.
Vita vinavyoendelea mashariki mwa taifa hilo lililokuwa zamani sehemu ya Umoja wa Kisovieti, ilikuwa mada kuu katika mkutano wa Usalama uliofanyika mwishoni mwa juma mjini Munich ambapo waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steimeier na mwenzake wa Marekani John Kerry waliikumbusha Urusi kuwa inachaguo ama kujiunga na nchi za magharibi kutafuta suluhisho la mzozo huo unaoendelea kuwaga damu au iwe tayari kutengwa zaidi .
kansela Merkel alisema sio wazi kwamba mazungumzo zaidi na Rais Putin yataleta makubaliano, lakini nafasi zote za kidiplomasia ziko wazi.
Chanzo: dw.de
No comments:
Post a Comment