Saa tano kamili za usiku, geti la mzee Komba likagongwa. Ugongwaji wake ulionyesha ni wa mtu mgeni kwani ulikuwa ni kwa sauti kubwa. Kwa kuwa alikuwa bado sebuleni wakiwa na mkewe wakiendelea kulizungumzia sakata lile, yeye mwenyewe akasimama na kwenda kufungua.
Sasa endelea...
Ni polisi.
“Shikamoo mzee,” mzee Komba aliamkiwa na askari aliyekuwa amening’iniza bunduki mabegani mwake, mara tu alipofungua geti.
“Marahaba kijana, vipi mbona usiku sana?” aliitikia na kuuliza swali ambalo Polisi hao walimjibu kuwa walikuwa wamekuja kumchukua kijana wake aitwae Stone kwani kulikuwa na malalamiko kidogo juu yake, hivyo walimtaka kituoni kwa mahojiano.
“Malalamiko gani ambayo hayawezi kusubiri kukuche vijana wangu, ninawaombeni kama inawezekana nimlete mwenyewe kituoni kesho asubuhi,” mzee Komba aliwasihi askari.
Askari hao wakakataa na mzee Komba naye akagoma kumtoa kijana wake usiku ule pasipo kwanza kuelezwa kosa la kijana wake. Ubishi ulikuwa mkubwa uliolazimisha majirani kuamka na mjumbe kuitwa.
Ingawa mzee Linus na familia yake waliamka na kutoka nje, lakini alibaki kimya bila kusema lolote wakati rafiki yake alipokuwa akibishana na Polisi. Mjumbe wa mtaa, mzee Masta, aliwauliza kwa busara askari wale, shauri lililopo kituoni linalomuhusu Stone.
“Tumesema tatizo litajulikana hukohuko kituoni, sisi tunafanya ubinadamu mnatuona wajinga, au mnataka tuingia ndani kwa nguvu?” Polisi mmoja, kati ya watatu waliokuwepo alisema. Kutotajwa kwa sababu ya kuja kumchukua Stone, kulichochea vurugu za wananchi ambao sasa walishakuwa wengi.
Hatimaye Polisi walishindwa, wakakubaliana na mzee Komba kuwa ampeleke mwanaye kituoni mapema kesho yake, vinginevyo wangekuja kumchukua mwenyewe.
Polisi walipoondoka, watu waliendelea kujadili kwa muda suala hilo. Kwa kuwa mzee Linus hakuchangia lolote wakati wa mabishano yale, mzee Komba alimfuata alipokuwa amesimama nje ya geti la kuingilia ndani kwake. Akamuuliza sababu ya kutomsaidia katika ishu ile, akasema aliogopa kuisaliti nafsi yake.
“Kuisaliti nafsi yako kivipi?” aliuliza mzee Komba.
“Ni mimi ndiye niliyeenda Polisi kuwataarifu kuhusu Stone kama tulivyokuja kwako jana, tulijadiliana na mama tukaona kama kuna hatari hivi, ni bora Polisi wakajua kinachoendelea,” mzee Linus alisema huku akimtazama mwenzake usoni bila kupepesa macho.
Mzee Komba hakutegemea kusikia maneno yale, alitambua kuwa mkutano wao wa mapema kuhusu suala lile ulishaweka mambo sawa. Hakudhani kama kulikuwa na umuhimu wa kwenda kuripoti polisi tukio ambalo limeshajadiliwa kama familia. Akamtazama kwa macho ya kutoamini, akamuuliza kuhusu maelezo aliyotoa huko, akajibiwa kwamba ni hofu juu ya usalama wa kijana wake kutokana na mwenendo wa Stone.
Taratibu mzee Komba akaondoka kurejea ndani kwake, aliwashukuru watu wachache waliobaki nje wakizungumza kwa kitendo chao cha kutoka nje na kwenda kumsaidia. Ndani, akawakuta mkewe akiwa amekaa na Stone sebuleni.
“Sasa kwa nini hawajasema kosa lake hao Polisi,” mke wake aliuliza, swali ambalo mzee Komba alilitegemea.
“Majirani wameenda kushtaki kuhusu Stone, wanaamini alitaka kumdhuru kijana wao, wamekwenda kutoa taarifa juu ya usalama wa mtoto wao. Kwa hiyo Stone ukae ujipange ujue cha kusema mbele yao.”
Stone akahisi ubaridi umepita ghafla mwilini mwake kabla ya hali yake kurejea kawaida. Akauma midomo yake na kuiachia. Wazazi wake wakatazamana.
***
Waliwahi sana kuamka, Stone akafanya mazoezi kwenye vyuma vyake vilivyokuwepo uani, baba yake naye akajinyoosha viungo chumbani kwake kabla ya wote kuingia bafuni kujimwagia maji, baada ya chai, safari ya kwenda kituo cha Polisi ikaanza.
Ni Stone ndiye aliyekuwa anaendesha gari lao, kila mtu alionekana kuwa na mawazo mengi kichwani mwake, hakuna aliyejua wanachowaza. Walifika kituo cha Polisi Wazo muda wa saa mbili kasoro robo asubuhi.
Je, nini kitaendelea? Usikose kufuatilia katika toleo lijalo.
Chanzo: Globalpublishers
No comments:
Post a Comment