WANACHAMA watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wametajwa kuwa nyuma ya kauli ya Rais Jakaya Kikwete kwamba kuna watu wana uwezo wa kurithi nafasi yake lakini hawajajitokeza bado, Raia Mwema limeambiwa.
Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, alizungumza hadharani mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Songea, Ruvuma kwamba chama hicho bado hakijapata mgombea na kwamba wanachama wa chama hicho wana wajibu wa kuwaibua ili chama kipate mgombea anayefaa.
"Wapo wengine ni material ya kuwa rais. Hawajijui na wanahitaji kukumbushwa. Kuwakumbusha si dhambi. Tusifanye ajizi kwa jambo hili ambalo ni kubwa kwa maslahi ya nchi yetu," alisema Kikwete wakati wa maadhimisho ya sherehe za miaka 38 ya CCM.
Katika mazungumzo ambayo gazeti hili limefanya na watu wa karibu na Kikwete na makada wa CCM, majina matatu yametajwa kama wanachama ambao japo hawatajwi kwenye vyombo vya habari na duru za kisiasa, wanachama wa chama hicho wanaona kwamba ni watu wanaoweza kuvaa viatu hivyo.
Wanachama hao watatu wanatajwa kuwa na sifa za kutokuwa na kashfa ya ufisadi, kutokuwa na makundi, wanataaluma wasio na shaka na watu ambao tayari wameonyesha uwezo mkubwa wa uongozi.
Raia Mwema limetajiwa majina matatu ambayo yanaelezwa kuwa kifuani kwa Kikwete wakati akitoa kauli yake hiyo.
Brigedia Jenerali Jaji Augustino Ramadhani
Tangu Desemba mwaka 2013, Augustino Ramadhani amekuwa akifanya kazi za kichungaji katika Kanisa la Anglikana, Zanzibar, mara baada ya kustaafu nafasi ya Jaji Mkuu wa Tanzania.
Jaji Ramadhani ana sifa kuu tatu za kipekee. Mosi, ni Mzanzibari, pili ni Mkristo na tatu ni mtu ambaye hajawahi kukutwa na doa lolote katika utendaji wake.
Kwenye hotuba yake hiyo ya Uwanja wa MajiMaji mjini Songea, Kikwete alisema; "Mgombea tunayemtaka ni yule ambaye wananchi wakisikia jina lake linatangazwa Watanzania waseme hapo barabara…. Isiwe wakiulizwa hapo vipi wanasema Aaah, hapo si sawa".
Katika vuguvugu la sasa la Muungano ambapo wapo Wazanzibari wanaoamini kuwa mara hii ni zamu yao kutoa Rais wa Muungano, Jaji Ramadhani anajitokeza kipekee kwa sababu pia ni Mkristo.
Ingawa Tanzania inafahamika kama nchi ambayo haiamini katika kupokezana madaraka kidini, utaratibu unaonyesha kwamba kumekuwa na kupokezana kwa madaraka baina ya waumini wa dini hizi mbili.
Kikwete ni Mwislamu na hivyo inatarajiwa kwamba mrithi wake atakuwa Mkristo. Mwanasheria huyu ni mmojawapo wa Watanzania wachache ambao wana bahati ya kuwa Wazanzibari na pia Wakristo.
"Faida nyingine ambayo Augustino anayo ni ile kwamba yeye ni Muanglikana. Kulikuwa na kilio hapa kutoka kwa baadhi ya Wakristo kwamba marais Wakristo waliopita walikuwa Wakatoliki na hivyo hii ni zamu ya mtu asiye Mkatoliki.
"Jaji Augustino Ramadhani ni mtu mwenye sifa za kipekee. Tatizo ambalo tunaliona ni kwamba itabidi ashawishiwe sana ili akubali kuingia kwenye kinyang’anyiro.
"Yeye alishaamua kumtumikia Mungu baada ya kustaafu. Hana mawazo yoyote ya kutumikia tena wananchi kisiasa. Nadhani Kikwete aliposema wengine wanahitaji kushawishiwa, alimaanisha bwana huyu,” alisema mmoja wa wana CCM wanaotajwa kuwania nafasi hiyo ambaye hata hivyo hakutaka kutajwa jina lake.
"Aaah, sasa si unajua namimi nagombea? Unataka uninukuu kabisa kwenye hilo.? This is my honest opinion (hapa nimezungumza ukweli mtupu). Sijui kama Jaji atakubali. Nafasi yangu iko palepale. Sasa wafuasi wangu watapata picha gani wakisikia nazungumzia uwezo wa mtu mwingine?" alihoji.
Jaji Ramadhani ni miongoni mwa Watanzania wenye historia ya kipekee. Akiwa Jaji Mkuu, hakuweza kuficha mapenzi yake kwa mchezo wa mpira wa kikapu na alikuwa mlezi wa chama cha mchezo huo ngazi ya Taifa.
Ni wakati huo pia ndipo alipoanza kufahamika kama mpiga piano wa kwaya ya Kanisa la Mtakatifu Alban lililopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
Jaji Ramadhani pia alikuwa askari aliyestaafu katika ngazi ya Brigedia Jenerali na pamoja na kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar na Tanzania, amehukumu pia katika Mahakama ya Kijeshi (Court Marshall).
Jambo ambalo watu wengi hawalifahamu ni kwamba babu wa Jaji Ramadhani, Mzee Augustino Ramadhani, alikuwa mmoja wa waanzilishi wa Chama cha African Association (AA) ambacho baadaye kilikuja kuwa sehemu ya muungano uliounda Chama cha ASP, ambacho sasa ni CCM.
Swali pekee ambalo pengine limebaki moyoni kwa Kikwete ni endapo Mchungaji Augustino Ramadhani ataacha kazi ya kuchunga ‘kondoo wa Bwana’ na kurejea kuwaongoza Watanzania kwenda katika nchi ya ahadi?
Dk. Augustine Mahiga
Jina la Mahiga si maarufu sana katika duru za kisiasa hapa nchini lakini pengine ndiye mwanadiplomasia wa Kitanzania anayeheshimika kuliko wote.
Mwaka juzi alimaliza jukumu lake la kuwa Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban ki Moon, nchini Somalia ambapo alisifiwa kwa kufanikisha kuwepo kwa serikali inayotambuliwa na Jumuiya ya Kimataifa pamoja na tishio la magaidi la Al Shabaab.
Mwanzoni mwa miaka ya 1990, Mahiga alinusurika kuuawa na Majeshi ya Charles Taylor, nchini Liberia wakati wa Vita ya wenyewe kwa wenyewe wakati huo yeye akifanya kazi ya kuongoza shughuli za Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la UN (UNHCR).
Mahiga amepata pia kuwa Balozi wa Kudumu wa Tanzania katika kipindi cha kati ya mwaka 2003 hadi 2010, ambapo Raia Mwema limeambiwa alirejesha heshima ya Taifa hili kiasi cha kufikia kuwa mojawapo ya zilizounda Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
"Katika korido za UN, ni wana diplomasia wachache, tena labda wapya ambao hawamfahamu Mahiga ni nani. Amekaa pale muda mrefu na alikuwa mahiri sana. Kikwete anasafiri sana na nadhani ujumbe anaoupata nje ya nchi ni kwamba Mahiga anafaa kuchukua nafasi yake," kilisema chanzo cha gazeti hili kutoka Ikulu.
Katika kipindi cha kati ya mwaka 1980 hadi mwaka 1983, Mahiga alikuwa Kaimu Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, nafasi ambayo ilimpa fursa ya kuifahamu Tanzania nje na ndani.
Kama ilivyo kwa Jaji Ramadhani, Mahiga naye haonyeshi hamu ya kutaka kuwa Rais. Anatumia muda wake mwingi kutoa mihadhara katika vyuo vikuu mbalimbali duniani ambako mihadhara yake mingi huhusu masuala ya Utawala Bora, Utatuzi wa Migogoro, Ulinzi na Usalama na Uhusiano wa Kimataifa.
Dk. John Pombe Magufuli
Katika majina haya matatu, Magufuli ndiye pekee ambaye anafanya kazi za kisiasa na pengine umri wake ni mdogo kulinganisha na wenzake hawa wawili.
Ingawa jina lake limekuwa likitajwa katika duru za kisiasa, Magufuli mwenyewe hajaonyesha dalili za kutaka nafasi hiyo na amewahi kukana hadharani wakati alipohusishwa na mojawapo ya kambi zinazotajwa kutaka kuwania urais kupitia CCM.
Mmoja wa wasaidizi wa Kikwete aliliambia gazeti hili juzi Jumatatu kwamba kuna mambo makubwa matatu ambayo yamewafanya baadhi yao kudhani Kikwete alikuwa akimzungumzia Magufuli.
Mosi, ni ukweli kwamba katika ziara ambazo Kikwete amekuwa akifanya ndani ya nchi, Magufuli amekuwa akionekana kama waziri anayeonekana kuheshimiwa na Watanzania.
Mfano ambao Kikwete amewahi kuusema kwetu unahusu mkutano mmoja wa hadhara uliofanyika Mwanza mwaka jana. Watu wa kule walikuwa wakizomea na kuonyesha alama za Chadema.
"Lakini alipopanda jukwaani Magufuli mkutano wote ulitulia. Mpaka Kikwete alipopanda jukwaani, mkutano ulikuwa umetulia. Nadhani Kikwete ameona kwamba labda huyu ndiye mwana CCM ambaye Watanzania wanamuamini," alisema.
Wakati aliporejea kutoka kwenye matibabu nchini Marekani mwishoni mwa mwaka jana, Kikwete alitamka hadharani kwamba alitaka kutangaza mapema kuhusu ugonjwa wa kansa uliokuwa ukimsumbua, lakini ni Magufuli aliyemkataza kufanya hivyo wakati wa kikao cha Baraza la Mawaziri.
Mwaka juzi, Magufuli pia aliwashangaza watu wakati alipopishana hadharani na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuhusu suala la magari ya mizigo kupita katika barabara yakiwa yamezidi mizigo.
"Ile ilikuwa ni ishara kwamba Magufuli alikuwa akiamini nguvu iliyo juu ya Pinda. Katika hali ya kawaida, si rahisi kwa waziri wa kawaida kutofautiana na Waziri Mkuu hadharani," kilisema chanzo kingine cha gazeti hili.
Msaidizi huyo wa Kikwete alilieleza pia Raia Mwema kwamba katika mojawapo ya misiba ya karibuni zaidi iliyoikumba familia ya Rais, Magufuli alikuwa waziri pekee ambaye alilala msibani kijijini Msata.
"Kama walivyo wenzake, Magufuli anaonekana ni mchapa kazi na mtu ambaye hahusishwi na masuala ya ufisadi ingawa kuna wanaonong'ona kuhusu suala la uuzaji wa nyumba za serikali," Raia Mwema liliambiwa.
Chanzo: Raia Mwema
No comments:
Post a Comment