Social Icons

Tuesday, 10 February 2015

Hadithi: Familia tata - 23


Ni Stone ndiye aliyekuwa anaendesha gari lao, kila mtu alionekana kuwa na mawazo mengi kichwani mwake, hakuna aliyejua wanachowaza. Walifika Kituo cha Polisi Wazo muda wa saa mbili kasoro robo asubuhi.

Sasa endelea...

Baba yake Stone alikuwa wa kwanza kushuka garini, akapepesa macho yake kuangalia watu wengi waliokuwa wamejazana kituoni hapo. Watu walikuwa wamejaa pale kwa ajili ya kuwadhamini ndugu zao waliokabiliwa na makosa mbalimbali.

Mzee Komba akatoa simu yake ya kiganjani, akabonyeza namba kadhaa, akaisogeza sikioni. Upande wa pili ukapokea, mazungumzo yalikuwa mafupi, akaikata na kumtaka mwanaye kushuka garini ili waelekee kituoni.

Wakajitambulisha, tayari taarifa zao zilikuwepo, wakatakiwa kuingia chumba kimoja walichoelekezwa, humo wakakutana na ofisa wa polisi aliyevalia kiraia. Akawakaribisha na mara moja akaanza kuzungumza nao juu ya wito wa Stone.

“Jana alikuja jirani yenu kulalamika kwamba wewe ulidhamiria kumfanyia kitu kibaya yule kijana, sasa nataka uniambie, kwa nini ulikuwa unamsogelea kwa kumvizia, tena uchochoroni?” aliuliza yule ofisa wa polisi, ambaye awali alijitambulisha kama Koplo Sam alimuuliza Stone.

Stone alilitegemea swali hili, alishapanga kitu cha kusema, hivyo harakaharaka akajibu.
“Afande, yule ni mdogo wangu, familia zetu ni marafiki kwa miaka mingi, mimi lengo langu lilikuwa ni kumtania kwa kumtisha na wala sikuwa na nia nyingine.”

“Sikiliza Stone, ni rahisi mtu wa kawaida kuweza kukuelewa, lakini siyo watu kama sisi ambao tunasomea namna ya kutambua nia au kusudio la kutenda uhalifu. Katika ishu yako, ukiangalia eneo, muda na namna ulivyomsogelea karibu bila yeye kukusikia, tunahisi ulikuwa na dhamira mbaya,” Koplo Sam alisema huku mzee Komba akijaribu kumtazama mwanaye kwa umakini mkubwa.

“Kweli afande, sikuwa na nia yoyote mbaya,” Stone alijibu tena.
Baada ya majadiliano mafupi, askari aliwaruhusu kuondoka, lakini akimpa onyo Stone kuwa jambo lolote baya litakalomkuta Tonny, yeye atakuwa mtuhumiwa wa kwanza, bila kujali wapi limetokea!
Wakainuka bila mzee Komba kusema jambo lolote, njiani wakiwa garini, akamsemesha kijana wake. Akamtaka kuyachukulia kwa uzito mkubwa maneno ya askari, kwa sababu hata kama jirani yao atadhuriwa na mtu mwingine, itakuwa ni juu yake.

“Lakini hata hivyo Stone, wewe kutaniana na mtoto kama Tonny umeanza lini? Mbona hata mimi napata mashaka na dhamira yako?” alimuuliza Stone ambaye macho yake aliyakaza mbele. Hakumjibu baba yake.

***
Mzee Linus hakupata usingizi kabisa, akili yake yote ilikuwa kwa Stone, hakutaka kuamini maneno yake kuwa eti alitaka kumtania. Kwa mara ya kwanza moyoni mwake, akaanza kuichukia familia ya jirani na rafiki yake wa muda mrefu. Usiku wa saa tisa alikurupuka kutoka usingizini, akawaza sana kabla ya kujikuta akitamka..hawanijui!

Ni kweli,  walikuwa hawamjui. Mzee Linus alikuwa mtata tokea utoto wake. Alikuwa na matukio mengi ya kushangaza na kushtusha. Akiwa darasa la pili, aliwahi kumpigilia msumari kwenye goti mtoto wa jirani yao. Msumari huo uliingia vibaya kiasi cha kusababisha binti huyo mdogo kukatwa mguu.

Kijijini kwao alikuwa mtukutu, mwenye kupigana kila siku na wenzake hadi baba yake alipoamua kumpeleka mjini kwa kaka yake, ambaye hakuwa na kijana wa kike. Alipofika huko Singida, haraka sana akazoeleka kiasi cha kuonekana kama ni mtu wa zamani kuliko ukweli wake.

Pamoja na kuwa alikuwa na akili nzuri darasani, lakini nje, alikuwa kwenye makundi ya vijana, wakipora watu usiku na kuwabaka wasichana. Mara tatu alishawahi kukamatwa na Polisi kwa kutajwa na wenzake kwenye matukio, lakini mara zote baba yake mkubwa, aliyekuwa mfanyabiashara aliyefanikiwa, alitoa kitu kidogo na yeye kuachiwa..!

Je, nini kitaendelea? Usikose kufuatilia simulizi hii katika toleo lijalo.

No comments:

 
 
Blogger Templates