Rais Barack Obama na kansela wa Ujerumani Angela Merkel jana(09.02.2015) wameelezea juhudi za pamoja za kufikiwa suluhisho la muda mrefu la kidiplomasia katika mzozo kati ya Urusi na Ukraine.
Rais Barack Obama na kansela wa Ujerumani Angela Merkel jana katika Viongozi hao hata hivyo hawajatoa njia ya wazi ya vipi mataifa ya magharibi yataweza kusonga mbele iwapo mazungumzo ya kuleta amani wiki hii yatakwama.
Obama ameonesha uwezekano kwamba Marekani inaweza kwa mara ya kwanza kutuma silaha za kupambana na vifaru pamoja na silaha nyingine za kujihami nchini Ukraine. Wakati hakuna uamuzi ambao umekwisha chukuliwa, rais Obama amesema ameamuru kikosi chake kutafakari "Iwapo kuna vitu vingine vya ziada vinavyoweza kufanywa kuisaidia Ukraine kuimarisha ulinzi wake katika mapambano dhidi ya uvamizi wa Urusi.
"Kile nilichokiagiza kikosi changu ni kuangalia hatua mbali mbali za kuchukua. Ni njia gani nyingine zinaweza kuchukuliwa kumfanya Bwana Putin abadilike na uwezekano wa silaha kali za ulinzi ni moja katika nafasi hizo ambazo zinachunguzwa."
Suluhisho la kijeshi
Lakini kansela wa Ujerumani Angela Merkel anapinga vikali kulipatia silaha jeshi la Ukraine lililozingirwa. Kansela wa Ujerumani , ambaye huenda ana uhusiano mzuri zaidi na rais wa Urusi Vladimir Putin , ameweka wazi kwamba hajakata tamaa juu ya uwezekano wa majadiliano ya kidiplomasia kuweza kuleta mpango wa amani ambao hadi sasa haujapatikana.
"Kila mara imethibitika kuwa ni sahihi kujaribu tena na tena kutatua mzozo kama huu," Merkel amesema.
"Sioni kabisa uwezekano wa suluhisho la kijeshi, lakini tunapaswa kufanyakazi kutafuta zaidi suluhisho la kidiploamsia."
Baadaye jana katika mkutano na waandishi habari pamoja na waziri mkuu wa Canada Stephen Harper, Merkel amesisitiza , "Nina matumaini kwamba tutaweza kutatua mzozo huu kwa njia za kidiplomasia kwasababu nafikiri kwa njia za kijeshi mzozo huu hauwezi kutatuliwa."
Putin anaendeleza sera za kimabavu
Harper amesema anafurahia juhudi za Ujerumani na Ufaransa kuleta suluhisho la amani lakini ameongeza: " Kwa bahati mbaya katika wakati huu Bwana Putin amekataa njia za kidiploamasia. Anaonekana kuelekeza ajenda zake kupitia matumizi ya nguvu.
Wakati huo huo zaidi ya wanajeshi 600 wa Urusi wameanza luteka ya kijeshi katika jimbo la Crimea, leo siku moja kabla ya mkutano kuhusu mzozo wa Ukraine katika mji mkuu wa Belarus Minsk.
Nayo majeshi ya serikali ya Ukraine yanaripotiwa kupata mafanikio katika maeneo yanayoshikiliwa na waasi mashariki mwa Ukraine.
Msemaji wa jeshi la Ukraine Eduard Basurin amesema jana(09.02.2015) kuwa wameuzingira mji wa Debaltseve , ambao umekuwa ukikabiliwa na mapigano makali katika muda wa wiki zilizopita, na kuutenga mji huo na barabara kuu.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape / rtre
Mhariri: Yusuf Saumu
Chanzo: dw.de
No comments:
Post a Comment