Social Icons

Thursday, 12 February 2015

Hadithi: Familia tata - 25


“Lete habari Chuga,” Dayani alimwambia mzee Linus. Wote wawili walionekana umri kuanza kuwatupa mkono. Aliposikia kauli hiyo, mzee Linus akajikuta akicheka kwa sauti!
Sasa endelea..

Mzee Linus alimtazama tena mshirika wake wa uhalifu wa hapo zamani, sura yake ilionyesha shauku kubwa ya kusikia habari kutoka kwa mwenzake. Kuona hivyo, mzee huyo akamsimulia kisa chote cha mwanaye, akamwelezea na hofu kubwa aliyonayo, sambamba na historia ya kutatanisha kati ya familia hizo mbili majirani.

“Kama ulivyonisimulia kuhusu huyo kijana ni kweli, basi sitashangaa nikisikia siku yoyote mtoto wetu akikutwa amekufa. Unakumbuka tulivyomzimishaga yule mchaga kule Singida siku zile? Tena ni wewe ndo ulimfuata kwa staili hiyohiyo na hakuliona tena jua, nafikiri tumuondoe mara moja huyo sijui Stone,” Dayani aliongea taratibu, lakini akionyesha msisitizo mkubwa.

Wakakubaliana kuhusu hilo. Dayani aliuliza maswali mengi kuhusu eneo wanaloishi, mazingira yake, nyenendo za Stone na habari nyingine nyingi alizohitaji kujua kabla ya kukamilisha kazi ambayo ilikuwa mbele yake, ambayo hata hivyo, ilikuwa ni ndogo mno kwake.

“Kwa hiyo Chuga, nakulipa shilingi ngapi?” mzee Linus alimuuliza Dayani.
“Acha mambo yako wewe, kwa hiyo mimi nikihitaji msaada wako inabidi nikulipe, nitamalizana na vijana, wewe kapumzike,” alijibiwa.

Waliendelea na mazungumzo yao ya hapa na pale hadi mchana, walipoanza kujipooza kwa bia baridi, kazi waliyoifanya hadi jua lilipozama. Dayani alimpatia kijana wake mmoja amuendeshe kwa gari lake hadi nyumbani kwake, kwani alihofia kwa kinywaji kile, lolote lingeweza kumtokea.

***
Mabadiliko ya uhusiano baina ya familia hizi mbili sasa yalikuwa ni dhahiri. Hakukuwa tena na ucheshi wala uchangamfu kama zamani. Mzee Komba alishaona dalili za rafiki yake wa siku nyingi kubadilika. Kitendo chake cha kumpeleka mwanaye polisi, wakati walishakaa na kuzungumza hakukipenda.
Ili kuhakikisha anailinda familia yake, alikaa chini na mkewe ili kutazama jinsi gani wangeweza kufanya. Walijadiliana vitu vingi, lakini baada ya muda mrefu wa majadiliano, hatimaye wakafikia muafaka kwamba wajilinde kwa dawa za waganga wa jadi.

“Ninamjua mganga anayeweza kufanya kitu kwa ajili yetu na bahati nzuri nilishawahi kuzungumza naye kuhusu hili jambo,” mke wa mzee Komba alimwambia mumewe.
“Unasemaje? Mbona hujawahi kuniambia,” alimwuliza.
Mke wake akamwelezea kwa kifupi kuhusu siku aliyoamua kwenda kwa mganga huyo, ingawa hakumweka wazi jinsi alivyofahamiana naye.

“Basi kesho inabidi twende,” mzee Komba alisema, jambo ambalo lilipingwa na mkewe.
“Hapana, haya mambo yakishaongelewa, jambo lifanyike mara moja, muda bado tunao, tuwashe gari twende, hapo Salasala wala siyo mbali mume wangu.”

Mzee Komba akakubali, wakafanya maandalizi kidogo na muda wa saa kumi na moja jioni siku hiyo, wakatoka na gari yao kuelekea kwa mganga. Nusu saa baadaye walikuwa kwenye foleni wakisubiri kwenda kumuona mtaalamu huyo wa mambo ya giza.

Zamu yao ilipofika, wakaingia na kuketi katika mkeka uliokuwa mbele ya mganga kama ilivyokuwa utaratibu. Baada ya salamu, mganga akawa wa kwanza kuwasemesha.

“Ule mpango wake wa wakati ule, sasa ndiyo wakati wake,” mganga, ambaye alimkumbuka sana mkewe mzee Komba, alisema na mwanamke huyo na mumewe kujikuta wakipatwa na mshangao mkubwa.
“Umejuaje bwana mkubwa,” mwanamke huyo aliuliza.

“Vifaa vyangu vinaonyesha kila kitu, kuna kitu kibaya sana kinaelekea kutokea kwenu wakati wowote kuanzia sasa,” alisema na kuwazidishia, siyo tu mshangao, bali hofu ndani ya mioyo yao!

Je, nini kitaendelea? Usikose kufuatilia simulizi hii ya kusisimua katika toleo lijalo.


Chanzo: Globalpublishers

No comments:

 
 
Blogger Templates