Social Icons

Thursday, 12 February 2015

Makubaliano ya kuweka siraha chini yafikiwa Minsk

Viongozi wa Urusi, Ukraine, Ujerumani na Ufaransa ambao walikuwa wakijadiliana Minsk wamefikia makubaliano ya kusitisha mapigano. Mazungumzo ya viongozi hao yaliyoanza jana usiku yaliendelea hadi hivi punde

Kansela Merkel (kulia) na rais Francois Hollande wakihudhuria mkutano wa kimataifa wa mjini Minsk kuhusu mustakbal wa Ukraine

Baada ya zaidi ya masaa 14 ya majadiliano viongozi wanaohudhuria mkutano wa kimataifa katika mji mkuu wa Byelorusi-Minsk,waliamua kutosema mengi,ila kusifu maendeleo yaliyoweza kufikiwa.Leo asubuhi viongozi hao kutoka Ujeruani,Urusi,Ufaransa na Ukraine waliotoka nje kidogo kabla ya kurejea upya katika ukumbi wa mazungumzo kujaribu kulifikia lengo lao-yaani makubaliano ya kuweka chini silaha.

Ubalozi wa Ukraine mjini Minsk ulidokeza hapo awali makubaliano hayako mbali kufikiwa na yanazungumzia mpango wa kuweka chini silaha utakaoanza kufanya kazi jumamosi ijayo pamoja na kutengwa eneo marufuku kwa silaha-lakini hakuna maelezo zaidi yaliyotolewa.

Hivi punde shirika la habari la Reuters limenukuu duru kutoka viongozi wa pande hizo nne zikizungumzia onyo la waasi wanaoelemea upande wa Urusi wanaotishia kutotia saini makubaliano ya kuweka chini silaha ikiwa serikali ya mjini Kiev haitowarejesha nyuma wanajeshi wake toka mji wa Debeltseve.

Watu tisaa wameuwawa na 35 kujeruhiwa katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita

Rais Petro Poroschenko (kulia) wa Ukraine

Vikosi vinavyoelemea upande wa Urusi,mashariki ya Ukraine vinazidi kuitia kishindo serikali ya mjini Kiev kwa kuendeleza mapigano mabaya kabisa kuwahi kushuhudiwa karibu na njia ya reli ya mji wa Debeltseve.

Watu tisaa wameuwawa na 35 kujeruhiwa kufuatia wimbi hili jipya la mapigano mashariki ya Ukraine,wimbi lililoanza samba na mazungumzo ya amani ya Minsk."Wanajeshi wawili wa Ukraine wameuwawa na wengine 21 kujeruhiwa amethibitisha msemaji wa vikosi vya wanajeshi wa Ukraie Vladyslav Seleznyov mbele ya waandishi habari.

Mkutano wa kilele wa Minsk ni mchanganyiko wa pirika pirika za kila aina,milango inayofungwa na kufunguliwa,vikao vya pande tatu tatu-mara kati ya kansela Angela Merkel,rais Francois Hollande na rais Vladimir Putin wa Urusi na baadae kati ya kansela Merkel,rais Hollande na rais Poroschenko wa Ukraine.

Rais Petro Poroschenko amekiri kansela Angela Merkel na rais Francois Hollande wamejitolea kwa dhati kuhakikisha makubaliano yanafikiwa.

Hatimae pande zinazohasimiana zimeridhia

Rais Vladimir Putin wa Urusi akizungumza na waandishi habari mjini MInsk

Hatimae baada ya muda wa masaa 16 ya mazungumzo magumu rais Vladimir Putin wa Urusi amesema yeye pamoja na viongozi wenzake kutoka Ujerumani,Ufaransa,na Ukraine wamekubaliana silaha nzito nzito ziondolewe toka nyanja za mapigano na makubaliano ya kuweka chini silaha yaanze kufanya kazi february 15 ijayo.

"Tumefanikiwa kuhusu mada muhimu" amesema rais Putin alioyenyesha kuwa mcheshi alipokuwa anazungumza na maripota mjini Minsk.Hata hivyo ameongeza kusema Kiev bado haitaki kuzungumza moja kwa moja na waasi.

Kansela Angela Merkel na rais Francis Hollande wanaotarajiwa baadae hii leo kushiriki katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels wamesema watawataka viongozi wa Umoja huo waunge mkono makubaliano ya Minsk.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AP/dpa/AFP/Reuters

Mhariri: Gakuba Daniel

Chanzo: dw.de

No comments:

 
 
Blogger Templates