“Lakini kweli eti jamani?” mtu mwingine naye akadakia na mara moja, mjadala mpya juu ya tukio hilo ukaanza.
Hisia za kuwepo kwa mpango maalum wa kuichoma nyumba hiyo kutoka kwa mzee Linus mwenyewe ukaanza kusemwa taratibu.
Sasa endelea...
Mzee Linus akachanganyikiwa. Ghafla mwili wake wote ukaloa jasho ndani ya sekunde kumi tu, akili yake haikujua nini cha kufanya na wala hakuelewa ataanza vipi kumfahamisha mkewe juu ya tukio hilo.
Wakati akihangaika kichwani mwake kujiuliza jinsi gani atafanya, mara mkewe naye akaamka, simu yake ambayo ilikuwa chini ya mto aliolalia, ikawa inaita, akaichukua na kuipeleka sikioni huku akimshangaa mumewe alivyoloa jasho chapachapa!
“Whaaaat,” mke wa mzee Linus aliruka ghafla kitandani huku simu yake ikianguka chini, mara tu baada ya kupewa taarifa ya kuteketea kwa nyumba yao.“Baba Brown, usitaka kunitania kabisa, niambie kwa nini umechoma nyumba yetu moto, niambie sasa hivi kabla sijaenda Polisi, huwezi kuturudisha kwenye umasikini kirahisi namna hii,” alifoka mama huyo, sasa akiwa amesimama chini, akihema kwa sauti kubwa.
Mzee Linus hakujua aseme nini, akajilaumu kwa kitendo chake cha kufanya siri mpango ule, maana kama angemweleza, wangeweza kujua ni bahati mbaya. Na sasa, baada ya tukio kutokea, hakukuwa na jinsi yoyote ya kumweleza maneno akayaelewa!
“Lakini ni ya kwetu kweli? isije ikawa ni ya jirani yetu,” mzee huyo alijaribu kujifariji, akiamini huenda wamekosea kumpigia.
“Watu wawili hawawezi kukosea kukupigia wewe na mimi kutuambia juu ya kuungua kwa nyumba, hilo jasho la nini, si wamekupigia wao? Au unatoka jasho kwa ajili ya nini, nyumba iliyoungua ni yetu na wewe ndiye uliyeichoma, kwa nini?” aliendelea kufoka mama wa watu.
Mzee Linus akainamisha kichwa chake chini, lakini sekunde chache baadaye, kama aliyekumbuka kitu, akainua uso wake na kumwambia mke wake.
“Tulia, kuna kitu kinaanza kunipa picha kuhusu hili tukio, tulia usiwe na haraka kwanza, ngoja nifanye utafiti kidogo nitakujuza,” maneno hayo hata hivyo hayakusaidia lolote, mama huyo alivaa nguo zake na kutoka nje, alikochukua gari na kuliwasha kuelekea eneo la tukio!
“Chuga, nini kimetokea, mbona umenigeuzia kibao,” mzee Linus alimwambia Dayani, mara tu mkewe alipotoka nje na kuhakikisha akiliwasha gari lao na kuondoka. Kauli hiyo ilimshangaza rafiki yake, ambaye alikuwa akijiandaa kukutana na vijana wake wa kazi kwa ajili ya kuwapongeza kwa kazi nzuri!
“Vipi, mbona sikuelewi?” naye alimjibu mwenzake ambaye alimwelezea kuhusu simu alizopigiwa kuwa ni nyumba yake ndiyo iliyoungua badala ya mtu waliyekusudia.
Dayani akaomba azungumze na vijana wake, ambao baada ya kuwauliza kuhusu nyumba waliyoichoma, walimhakikishia kuwa ni ileile waliyoikagua mchana wake.
“Nataka kuwaambia hivi, mmezingua, mmeifanyia nyumba ya mshkaji wangu na mnanijua vizuri nilivyo sitaki ujinga, kazi zenu zote huwa nawalipa vizuri kwa sababu mnazifanya vizuri, sasa mnapokosea kama hivi ni lazima muwajibike, chagueni adhabu inayofanana na ile nyumba,” Dayani aliongea kwa ukali, hali iliyomtisha Beka, aliyekuwa na simu.
Simu ikakatika, lakini iliendelea kubaki sikioni mwa Beka kwa sekunde kadhaa mbele, kisha akamwambia Shosi;
“Tumekwisha babaake”
“Kivipi,” Shosi akasema huku akihema, tena akiwa ameshamsogelea karibu, alimfahamu vyema Dayani, hakuwa na masihara kwenye kazi.
“Anadai nyumba tuliyoichoma siyo yenyewe, tuliyoifanyia ni ya rafiki yake,” Beka alisema huku sura yake ikionyesha hofu ya dhahiri.
Inaendelea
Chanzo: globalpublishers
No comments:
Post a Comment