Social Icons

Wednesday, 18 February 2015

Hadithi: Familia tata - 28


Sasa watu walishajaa, walijitahidi kuuzima kwa mchanga na maji kwenye ndoo, lakini walionekana kama watu wanaofanya mchezo, moto ulizidi kuteketeza vitu, vilivyosikika vikipasuka kila mara!
Sasa endelea...

“Maskini mzee Linus na familia yake wanateketea hivihivi, lakini mbona hatujasikia hata kelele,” majirani wenye majonzi walikuwa wanazungumza nje ya nyumba hiyo wakiwa hawaamini kinachotokea.
Akina Beka walikosea, hawakuichoma nyumba ya akina Stone, bali waliiwasha moto nyumba ya mtu wao. Akilini mwao walijua wamefanya kazi waliyotumwa kikamilifu, walisubiri kukuche wakachukue mshiko wao. Mtu mmoja miongoni mwa watu waliofurika nje ya nyumba, akapata wazo na kubonyeza namba za simu ya mzee Linus.

Aliisikia ikiita hadi ikakatika. Akapiga tena, ikaita hadi kukatika.
“Haiwezekani, simu ya mzee Linus inaita, atakuwa hayupo nyumbani, masikini sijui kama anajua,” mtu huyo alisema kwa sauti iliyowashitua watu wengine, akina mama wakajaribu kupiga namba ya mkewe, nayo ikawa inaita, lakini haikupokelewa, vijana wakapiga namba ya Brown, haikuita hata mara tatu ikapokelewa..

“Hellow mwana uko wapi?” Jaffari, jirani yao mtaani alimuuliza bila hata kumsalimia.
“Dah, afu una bahati kweli, ningekuwa ndani nisingesikia simu yako maana kelele ni nyingi kweli, nipo Club mwana, vipi?” alijibu Brown muda huo ukielekea saa nane na nusu usiku.

Brown hakushangaa kupigiwa simu muda ule na Jaffari kwa sababu walikuwa ni marafiki na wote walipenda kujirusha. Alipoambiwa kuhusu nyumba yao kuungua alishangaa sana!Alianza kuwatafuta wazazi wake kwenye simu, lakini hata hivyo hawakusikia kwa vile kila mmoja alikuwa ametoa mlio kuepuka usumbufu. Brown hata hivyo, hakuwa na wasiwasi wa kuwepo kwa vifo kwa vile alijua hakukuwa na mtu aliyelala humo kwa vile nyumba ilikuwa inapigwa dawa!

Saa kumi na moja alfajiri mzee Linus alishtuka kutoka usingizini, alikuwa anaota ndoto mbaya. Aliposhtuka simu yake ilikuwa inaita, lakini kabla hajaifikia, ikakata. Alipoichukua na kuangalia aliyempigia, akagundua simu nyingi kupigwa katika simu yake, nyingi zikiwa za majirani, akajua kimenuka!

Akamchagua jirani mmoja, akampigia kumuuliza kulikoni. 
“Mzee Linus? Siamini kama ni wewe kweli, uko wapi? Nyumba yako imeteketea kwa moto na sijui kama kuna mtu alilala ndani,” jirani huyo alisema kwa pupa mara tu mzee huyo alipomsalimia na kujua kulikoni kumpigia simu usiku wa manane!

***
Wakiwa bado hawajalala, mzee Komba na mkewe ghafla wakaona mwanga mkubwa ukimulika nyumba yao kutoka upande wa mzee Linus, kwa haraka wakaamka na kuchungulia. Walishangaa sana kuona moto mkubwa kwa jirani yao, lakini wasisikie sauti yoyote ikiita, angalau kuomba msaada.
Haraka wakawafuata watoto vyumbani mwao na kuwaamsha kwa nguvu, walikuwa ni watu wa kwanza kuamka miongoni mwa nyumba zote za jirani na ndiyo waliopiga kelele za kwanza kuashiria kulipuka kwa moto huo.

Waliungana na wengine katika harakati za kuuzima lakini bila mafanikio. Wengi walijaribu kuwauliza chanzo cha moto huo, lakini walisema hawaelewi, wakihisi huenda kulikuwa na hitilafu za umeme. 
Maneno yalikuwa ni mengi wakati watu wakiangalia na kusubiri moto huo umalizike kuwaka. Hadi wakati huo, walishakuwa na uhakika kuwa hakukuwa na mtu yeyote ndani ya nyumba hiyo, kwani wote walikuwa wametoka.

“Lakini, hebu tujiulize jamani, kwa nini moto uwake leo kukiwa hakuna mtu ndani, wote kwa pamoja walikwenda wapi,” mtu mmoja, ambaye mtaani hapo alijulikana kama Ndocha, aliuliza huku akiwakazia wenzake macho, kuonyesha kuhitaji majibu.
“Lakini kweli eti jamani?” mtu mwingine naye akadakia na mara moja, mjadala mpya juu ya tukio hilo ukaanza.

Hisia za kuwepo kwa mpango maalum wa kuichoma nyumba hiyo kutoka kwa mzee Linus mwenyewe ukaanza kusemwa taratibu.

Inaendelea

Chanzo Globalpublishers

No comments:

 
 
Blogger Templates