Social Icons

Friday, 20 February 2015

Hadithi: Familia tata - 31


“Mimi nafikiri mngezungumza na baba maana mimi hapa nilipo nitadondoka wakati wowote, sina nguvu kabisa,” alisema mama huyo huku akikaa chini pembeni ya gari lake. Wale askari walimwelewa, wakamwomba ampigie simu mumewe, wakimtaka kufika kituo kidogo cha Polisi Wazo kwa mahojiano mafupi.
Sasa endelea.....

Mke wa mzee Linus akachukua simu yake na kubonyeza namba za mumewe, alipopokea akamweleza kuhusu wito wa Polisi. Akakata na kuirudisha kwenye mfuko wake wa kwapani.

Mzee Linus alijua kimenuka, hakuelewa atasema nini kwa Polisi. Lakini baada ya kutafakari na kujijibu maswali aliyojiuliza, aliamua kwenda, lakini kwanza baada ya kuwa amefika nyumbani kwake.

Akachukua bodaboda iliyomfikisha hadi nyumbani kwake. Alishangaa kuona umati wa watu ukiongezeka, licha ya kwamba kulishakucha. Watu wote walimwangalia yeye. Alionekana kusikitika sana kwa tukio hilo, lakini baadhi ya watu walimtilia shaka, walimuona kama anayefahamu kilicho nyuma ya pazia.

Mzee huyo alizunguka zunguka kuitazama nyumba yake huku akizungumza peke yake, kichwani mwake alikuwa anawaogopa zaidi polisi kuliko hasara aliyoipata. Alimuomba Mungu ampe nguvu aweze kuwajibu vizuri maswali yao!
***
Wakiwa chumbani kwao, simu ya mama Juddy iliita, alipoangalia katika kioo, jina la mpigaji lilimshangaza, kabla ya kupokea, akamuonyesha mumewe, ambaye naye alionyesha mshangao.
“Haloo,” aliita baada ya kuipokea.

“Habari za leo mama,” upande wa pili ulijibu.
“Tunashukuru Mungu tumeamka salama, sijui wewe huko baba,” mama Juddy alijibu akiwa na hamu ya kutaka kujua sababu ya kupigiwa simu.

“Huku wazima. Vipi, kuna kitu gani kimetokea huko kwenu?” mpigaji aliuliza.
“Huku kwetu? Huku kuko shwari tu baba,” alijibu mama.
“Kweli?”

“Eeeh, kwani vipi baba,”
“Kama ni hivyo sawa, tutawasiliana wakati mwingine.”
“Haya asante, kukiwa na lolote tutakuambia,” alisema mama na kukata simu.
Ni mganga wao!

Mzee Komba alikuwa na hamu kubwa ya kusikia kilichosemwa na mganga wao, lakini aliposimuliwa, hakuona kama kulikuwa na chochote cha kutilia shaka…
***
Mzee Linus baada ya kuiangalia nyumba yake ilivyoungua, alimfuata mkewe na kumtaka kuingia ndani ya gari ampeleke Polisi. Yeye alienda upande wa dereva, akashika usukani na kuondoa gari taratibu.
“Sikiliza mke wangu, mimi ni mumeo, tuna watoto, hiki kilichotokea ni kikubwa sana, kitatugharimu, lakini nadhani mimi ni muhimu zaidi ya nyumba,” alisema taratibu huku akiendesha kwa mwendo wa taratibu sana.

“Kwa hiyo,” mkewe alimjibu huku sura yake ikiwa imejikunja.
“Nataka unisaidie, vinginevyo ninaweza kuangamia na kuizidishia familia yetu matatizo,” alisema huku akionyesha huzuni kubwa.

“Nikusaidie nini, kuichoma tena moto nyumba?” mama alizidi kufoka. 
Mzee Linus akaamua kunyamaza. Aliendesha gari kama mita hamsini, akalisogeza pembeni na kuliegesha. Kichwa chake akakiinamisha kwenye usukani, akionekana kuwa na mawazo mengi.

Mkewe alibakia ameegemea kiti chake, naye akili yake ikiwa mbali kabisa kimawazo. Watu waliokuwa wakipita ambao waliwafahamu, waliwaonea huruma, walijua kwa nini ni lazima wawe kama walivyokuwa!

Baada ya kama nusu saa ya kukaa pale pembeni, hatimaye mzee Linus aliliwasha gari na kabla ya kuondoka, akamuita mkewe, alipoitika akaanza tena kumsemesha akisisitiza amsaidie katika tatizo lililo mbele yake. Mkewe akaamua kumsikiliza anachotaka kusema, ili aone kama anaweza kumsaidiaje.

“Kule Polisi, nataka nikadanganye, sitasema kama tulitoka wote kwa sababu ya nyumba kupigwa dawa, nikisema hivyo nitajikamatisha,” alisema mzee Linus, macho yake yakiwa usoni mwa mkewe, moyo wake ukimdunda!

Mkewe akamtupia macho kwa mshangao, kitu kama hakumwelewa vile. Akili yake ikampeleka kuamini moja kwa moja kuwa mumewe ndiye aliyechoma moto nyumba yao. Lakini akajiuliza, kwa nini?

Inaendelea.

Chanzo: Globalpublishers

No comments:

 
 
Blogger Templates