WAZIRI wa Ujenzi, John Magufuli, amejitosa katika kinyang’anyiro cha kuwania Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Raia Mwema linafahamu.
Uthibitisho wa wazi kuhusu hatua hii ya Magufuli ulikuwa wakati wa msiba wa mtoto mkubwa wa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga, Fidel, uliotokea Januari mwaka huu, ambapo waziri huyo anadaiwa kumuarifu kiongozi huyo wa chama cha Cord kuhusu suala hilo.
Vyanzo vya Raia Mwema vimeeleza kwamba Raila na Magufuli ni marafiki wakubwa na ndiyo maana Mtanzania huyo aliamua kutumia nafasi hiyo kumueleza mwenzake yaliyo ya moyoni.
“Utakumbuka alipofariki baba mzazi wa Magufuli, Raila alikuja msibani. Hawa ni marafiki wa muda mrefu. Sasa kule kwenye msiba mheshimiwa aliamua kumueleza mwenzake. Hili mimi nalifahamu,” kilieleza chanzo hicho cha gazeti hili.
Jina la Magufuli limekuwa likitajwatajwa kama miongoni mwa majina ya watu wanaofaa kumrithi Rais Jakaya Kikwete baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, ingawa amekuwa hana spidi kwenye suala hilo kama walivyo baadhi ya wanasiasa wengine ndani ya CCM.
Wiki mbili zilizopita, Raia Mwema lilibashiri kwamba Magufuli ni mmoja wa wanasiasa ambao wanaweza kupitishwa na CCM kumrithi Kikwete kutokana na sifa yake ya uadilifu na uchapakazi.
Wakati akizungumza kwenye maadhimisho ya miaka 38 ya CCM yaliyofanyika mjini Songea, Ruvuma, mwanzoni mwa mwezi huu, Kikwete alisema wapo viongozi wazuri ndani ya chama hicho wenye sifa lakini hawataki nafasi hiyo na wanatakiwa kushawishiwa.
Kauli hiyo ilitafsiriwa na wengi kama kuwaandaa wana CCM na jina la mgombea ambaye hatajwitajwi kwa sasa; huku majina ya Augustino Ramadhani, Dk. Augustine Mahiga na Magufuli yakitajwa.
Katika mazungumzo na mmoja wa wasaidizi wa Kikwete wiki mbili zilizopita, Raia Mwema liliambiwa kwamba kuna mambo makubwa matatu ambayo yamewafanya baadhi yao kudhani Kikwete alikuwa akimzungumzia Magufuli kwenye hotuba yake ya Songea.
Mosi, ni ukweli kwamba katika ziara ambazo Kikwete amekuwa akifanya ndani ya nchi, Magufuli amekuwa akionekana kama waziri anayeonekana kuheshimiwa na Watanzania.
“Mfano ambao Kikwete amewahi kuusema kwetu unahusu mkutano mmoja wa hadhara uliofanyika Mwanza mwaka jana. Watu wa kule walikuwa wakizomea na kuonyesha alama za Chadema.
"Lakini alipopanda jukwaani Magufuli mkutano wote ulitulia. Mpaka Kikwete alipopanda jukwaani, mkutano ulikuwa umetulia. Nadhani Kikwete ameona kwamba labda huyu ndiye mwana CCM ambaye Watanzania wanamuamini," alisema.
Wakati aliporejea kutoka kwenye matibabu nchini Marekani mwishoni mwa mwaka jana, Kikwete alitamka hadharani kwamba alitaka kutangaza mapema kuhusu ugonjwa wa kansa uliokuwa ukimsumbua, lakini ni Magufuli aliyemkataza kufanya hivyo wakati wa kikao cha Baraza la Mawaziri.
Mwaka juzi, Magufuli pia aliwashangaza watu wakati alipopishana hadharani na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuhusu suala la magari ya mizigo kupita katika barabara yakiwa yamezidi mizigo.
"Ile ilikuwa ni ishara kwamba Magufuli alikuwa akiamini nguvu iliyo juu ya Pinda. Katika hali ya kawaida, si rahisi kwa waziri wa kawaida kutofautiana na Waziri Mkuu hadharani," kilisema chanzo kingine cha gazeti hili.
Msaidizi huyo wa Kikwete alilieleza pia Raia Mwema kwamba katika mojawapo ya misiba ya karibuni zaidi iliyoikumba familia ya Rais, Magufuli alikuwa waziri pekee ambaye alilala msibani kijijini Msata.
"Kama walivyo wenzake, Magufuli anaonekana ni mchapa kazi na mtu ambaye hahusishwi na masuala ya ufisadi ingawa kuna wanaonong'ona kuhusu suala la uuzaji wa nyumba za serikali," Raia Mwema liliambiwa.
Katika kuchagiza hilo, jarida la The Indian Ocean linalochapwa na taasisi inayoheshimika barani Afrika ya Africa Intelligence, katika toleo lake la Februari 13, 2014, limemtaja Magufuli kama kipenzi cha Kikwete na mtu ambaye anaweza kumuunga mkono.
Jarida hilo ambalo hufanya uchambuzi wa masuala mbalimbali ya nchi zilizo katika mwambao wa bahari ya Hindi barani Afrika, limefanya uchambuzi kuhusu kinyang’anyiro cha kuwania urais kupitia CCM haswa baada ya kashfa ya akaunti ya Escrow.
Chanzo: Raia Mwema

No comments:
Post a Comment