Mkewe akamtupia macho kwa mshangao, kitu kama hakumwelewa vile. Akili yake ikampeleka kuamini moja kwa moja kuwa mumewe ndiye alichoma moto nyumba yao. Lakini akajiuliza, kwa nini?
Sasa endelea...
“Unataka uende ukasemaje,” mkewe alimuuliza.
“Kila mtu awe na sababu yake, zungumza na watoto waambie unachoweza kuwaambia ili wasiseme kama waliondoka kwa sababu ya nyumba kupigwa dawa, mimi nitasema tulitoka kulala hoteli kama moja ya taratibu zetu, kwamba mara kwa mara tunatoka kubadilisha mazingira,” mzee Linus alizungumza huku macho yake yakiwa bado kwa mkewe.
“Unafikiri maelezo hayo yatawaridhisha Polisi?” alimuuliza.
“Wewe nisaidie kwa hilo, hayo mambo mengine niachie mimi,” mumewe alijibu.
“Ni hilo tu ndilo unalotaka nikusaidie?” mkewe alimuuliza.
“Ndiyo”
“Nitakusaidia kwa hilo, lakini kwa masharti,” mkewe alisema.
“Masharti gani?”
“Niambie sababu ya wewe kuichoma moto nyumba yetu.”
***Beka na Shosi walikuwa wamekaa mbele ya Dayani, katika mojawapo ya vibanda ndani ya baa kubwa ya Zanzi. Mwenyeji wao alionekana kuwa na hasira za dhahiri, alitaka maelezo kutoka kwa vijana wake ili aweze kujua nini cha kuwafanya.
Vijana wale walijitahidi kujieleza kadiri walivyoweza, wakisema kuwa walifanya mahesabu ya kutosha na walishalifahamu eneo lile kwa kadiri walivyoweza, lakini wakashangaa kwa kilichotokea.
“Unajua mnanishangaza sana, itawezekanaje iwe hivyo mnavyosema? Yaani kwa mfano unajua kabisa unanipiga ngumi mimi, halafu eti umpige huyu, itawezekanaje?” Dayani aliwauliza uso wake ukiwa umezidi kufura kwa hasira.
Kwa jinsi walivyomtambua Dayani, vijana wale wawili wakajikuta wakianza kulia, walifahamu mwisho wao ulikuwa umefika, kwa sababu moja ya sifa kubwa za bosi wao, ni kutotaka masihara kwenye kazi.
“Sikilizeni, mimi nimefanya kazi hii kwa miaka mingi sana, nimenusurika mara nyingi sana kuuawa, nilichojifunza ni kwamba dawa pekee ya kuepuka kuuawa ni kuua, mmesikia?”
“Tunaomba utusamehe bosi, usituue, tunaomba tukafanye tena ile kazi, hata ikibidi leo,” Beka, huku akitoa machozi, alimuomba Dayani, aliyekuwa anavuta sigara.
“Sasa niwasamehe na hii nyumba ya rafiki yangu mliyochoma?”
“Tutatafuta hela tumlipe bosi, tuambie tu ni shilingi ngapi tutatafuta, wajinga wengi tu wana hela, tutaipata,” Shosi alisema, huku akili yake ikifikiria vituo vya mafuta, maduka makubwa na wafanyabiashara wanaoweza kuwa na hela.
“Sawa, nitataka mfanye jambo moja la msingi, tena kwa haraka kabisa, nataka mumlipe fedha za nyumba hiyo, ngoja niongee naye, hela hizi zipatikane leoleo,” alisema Dayani na kuchukua simu yake, akabonyeza namba za rafiki yake.
***
Mzee Linus alikuwa ametumbua macho baada ya kuulizwa swali lile, hakujua aseme nini, baada ya kutafakari sana kwa haraka, akaamua aseme ukweli ili mkewe ajue, potelea mbali kama atamwelewa au la.
Alipokohoa kama ishara ya kutaka kuanza kuzungumza, simu yake ikaita, jina la rafiki yake Dayani likajitokeza, akasita, ikaita kwa muda lakini baadaye akapokea.
“Niambie Chuga,” alijibu mara tu alipopokea.
“Poa, aisee, sasa nimeongea na vijana, watakulipa leoleo, sema ni shilingi ngapi thamani ya nyumba yako?” Dayani aliongea kwa kujiamini. Masikioni mwa mzee Linus, zilikuwa ni habari njema ambazo hakuzitegemea.
“Kwa thamani ya sasa, nadhani siyo chini ya milioni 150,” alisema kwa utulivu.
“Basi, leo hiihii utapata mzigo, usiwe na wasiwasi,” alisema Dayani na kukata simu.
Mzee Linus akaonyesha tabasamu usoni mwake, hali ambayo iliendelea kumshangaza mkewe. Anafurahi wakati nyumba yetu imeungua? Huyu ana nini? Alijiuliza mara mbilimbili mke wake, alijua kuna siri kubwa nyuma ya pazia, akakohoa kumpa ishara mumewe kwamba anahitaji kujibiwa swali lake.
Itaendelea.
Chanzo: Globalpublishers

No comments:
Post a Comment