“Kwa thamani ya sasa, nadhani siyo chini ya milioni 150,” alisema kwa utulivu.
“Basi, leo hiihii utapata mzigo, usiwe na wasiwasi,” alisema Dayani na kukata simu.
Mzee Linus akaonyesha tabasamu usoni mwake, hali ambayo iliendelea kumshangaza mkewe.
Endelea...
Mzee Linus akamueleza kila kitu mkewe, kama kilivyokuwa kuanzia mwanzo hadi mwisho. Alipomaliza, akavuta pumzi ndefu, mzigo mkubwa sasa ukawa kwa mke wake ambaye naye alipumua kwa nguvu, moyoni akiwa na wasiwasi mwingi.
Wakati mumewe akiwa anataka kumsikia atakavyosema, mama Tonny alibakia kimya kwa muda mwingi, akitafakari kile alichokisikia. Hatimaye akafunguka.
“Hivi tumefikia kiwango cha kutaka kuangamizana kweli baba Tonny?” alimuuliza mumewe.
“Kama Stone alitaka kumuua mwanetu, sisi tuna sababu gani ya kuwaonea huruma, kama mbwai mbwai tu,” alisema mumewe.
“Dah, ni hatari kwelikweli, haya sasa wameunguza nyumba yetu, itakuwaje?” aliuliza.
Ndipo mzee Linus akamuelezea habari nzuri alizopata hivi punde kutoka kwa Dayani, kwani siku hiyohiyo walikuwa na uhakika wa kuzipata shilingi milioni mia moja na hamsini.
Baada ya kuridhishana kwa maelezo hayo, safari ya kuelekea polisi ikaendelea na hata walipofika, walichukua muda mfupi kumaliza mahojiano, kwani hakukuwa na lolote ambalo polisi walilikomalia na wote waliona kama ni ajali ya bahati mbaya.
Baada ya kutoka hapo, walielekea kwenye hoteli waliyolala jana yake na kuendelea kulipia chumba chao, kwa vile hawakuwa na sehemu ya kwenda kwa muda huo. Walikaa na kutafakari jinsi watakavyozitumia fedha walizokuwa wakizitegemea kutoka kwa vijana wa Dayani.
Wakakubaliana kutafuta kiwanja na kujenga sehemu nyingine mbali na pale, ili pamoja na mambo mengine, kuwaepuka kabisa majirani zao, kwani uhasama wao sasa ulizidi kipimo, kwani wakati wowote wanaweza kuuana.
***Wakiwa bado chumbani kwao wakiendelea na mazungumzo yao, simu ya mama Juddy iliita tena na kwa mara nyingine, mganga wao ndiye aliyekuwa akipiga. Kabla ya kupokea, akamuonyesha mume wake na baadaye akaipeleka sikioni.
Alisikiliza kwa muda wa kama dakika mbili hivi, lakini sura yake ilibadilika haraka na jasho likaanza kumtoka. Hadi alipomaliza kusikiliza, mikono yake ilibakia kifuani kwake, akihema alimwambia mumewe.
“Huwezi kuamini alichoniambia mganga, eti nyumba yetu ndiyo ililengwa ichomwe moto na hawa majirani zetu, lakini kibao kikawageukia,”
“Unasema?” aliuliza mzee Komba huku akihema.
Mkewe akarudia kumwelezea. Wakashindwa kuamini, wakalazimika kufunga safari hadi Salasala kusikia vizuri ana kwa ana.
Mganga hakuwaficha, akawaeleza kila kitu kilivyokuwa na baada ya hapo akamalizia kwa kuwaambia.
“Na muda wowote kuanzia hivi sasa, watakamatwa kwa sababu wataunganishwa kwenye kesi ya mauaji ambayo inaelekea kutokea hivi sasa.”
“Kivipi, kwani kuna mtu aliyekufa mle ndani?” mzee Komba alimuuliza mganga.
“Hapana, kuna mauaji yanaelekea kutokea muda siyo mrefu ujao, wao ndiyo chanzo, kabla ya jua kuzama, watakuwa polisi,” mganga aliongea, lakini hawakuweza kabisa kuelewa maana yake.
Baada ya mazungumzo kadhaa, baadaye wateja hao wawili waliaga na kuondoka kuelekea kwao, wakiwa na mawazo mengi sana vichwani mwao, maelezo waliyopata kutoka kwa mganga yaliwachanganya kabisa.
Hata hivyo, walijikuta wakishindwa kufanya lolote kwa sababu hawakuwa na ushahidi wowote wa kuwakamata majirani zao. Hata hivyo, wakaambizana kuongeza umakini katika kujilinda.
***
Beka na Shosi walikuwa wamesimama nje ya kituo cha mafuta cha Afrikana, wakimsoma meneja ambaye walipewa mchongo kwamba angechukua fedha za makusanyo ya wiki ili azipeleke benki. Nyendo za Meneja huyo zilionyesha kuwa wakati wowote angekabidhiwa mzigo aupeleke.
Dakika kumi baadaye, gari la Night Support, lilifika katika kituo hicho, likageuka na kuelekeza upande wake wa nyuma katika mlango wa chumba cha meneja. Watu waliovalia mavazi ya walinzi binafsi walikuwa imara na bunduki zao, wakiwa wanaangalia huku na huku.
Zoezi la kupakia fedha lilifanyika kama dakika kumi hivi, mlango wa gari ukafungwa, walinzi wawili wakapanda nyuma, meneja akapanda mbele na taratibu gari likaanza kuondoka kuifuata barabara ya lami kuelekea mjini..!
Je nini kitatokea? Usikose kufuatilia simulizi hii katika toleo lijalo Jumatano.
JIUNGE NA GLOBAL BREAKING NEWS

No comments:
Post a Comment