Zoezi la kupakia fedha lilifanyika kama dakika kumi hivi, mlango wa gari ukafungwa, walinzi wawili wakapanda nyuma, meneja akapanda mbele na taratibu gari likaanza kuondoka kuifuata barabara ya lami kuelekea mjini..!
Sasa endelea...
BEKA na Shosi waliliacha gari hilo hadi lilipofika katika kituo cha daladala, wakapeana ishara na wenzao waliokuwa wamekaa kwenye gari lililoegeshwa njia panda ya kuelekea Mbezi juu. Wakaifuata pikipiki yao aina ya Boxer na kuanza kuondoka taratibu kuingia barabarani.
Gari lililokuwa mbele, ambalo walipeana ishara na kina Beka, lilikuwa na watu wanne, wote wakiwa na bunduki zilizokatwa vitako. Waliliona lile gari likienda mwendo wa kasi, walitaka shughuli ile ifanyike kwa haraka, hapohapo barabarani eneo la Makonde.
Mpango ulikuwa ni kwamba baada ya kulivamia, wangevunja mlango wa gari kwa risasi kisha makasha ya fedha yangepewa akina Beka ili wakimbie nayo njia za vichochoroni na nyingine waondoke nazo.
Katika kikosi hicho kulikuwa na takriban watu sita, wale waliokuwa kwenye gari, walikuwa ni vijana wa Kinyarwanda ambao muda mwingi katika maisha yao wametumia katika vita katika misitu ya Kongo wanakotumikia vikundi vya kijeshi kwa malipo maalum.
Mara ya mwisho, walikitumikia kikundi cha M23 kabla ya kuamua kukimbia baada ya kusikia majeshi ya Tanzania yamekwenda huko kuisaidia serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Walipoondoka walifikia Mwanza, ambako daima walikutana na bosi wao, Ntumba, ambaye ndiye kiunganishi kikubwa cha askari walioasi Rwanda, wanaotumika katika matukio mbalimbali ya ujambazi nchini.
Ntumba alipata simu ya Dayani asubuhi kuhusu kazi inayotakiwa kufanywa siku inayofuata naye akawapandisha ndege vijana wale wanne, ambao wanafahamu vizuri lugha ya Kiswahili.
Walilifuata gari lile lililobeba fedha wakitaka wakafanye tukio katikati ya barabara, lakini ghafla bila wao kutarajia, wakashangaa kuliona linapinda kona kuingia kushoto. Kwao, huko ndiko kulikuwa sehemu nzuri zaidi kwa kazi yao.
Walipoliona linakata kona, Beka na Shosi nao wakajikuta wakitabasamu, zoezi lingekuwa rahisi kuliko walivyoliona jinsi ambavyo lilitakiwa kufanywa pale barabarani.
***
Moyo wa dereva ulikuwa unadunda wakati alipoanza kumwambia meneja wa kituo kile cha mafuta.
“Inabidi tupite njia hii kuepuka foleni, ukiwa umebeba hela nyingi kama hii kupita njia kubwa, ukikwama kwenye foleni ni rahisi watu kutuvamia,” alisema huku mapigo ya moyo wake yakiongezeka.
Akili ya meneja ikajikuta imepata maswali mara moja, mbona kila siku tunapita njia hii na hakuna kinachotokea? Hata hivyo, aliamua kunyamaza, akashika sehemu aliyoweka bastola yake, akakuta ipo imetulia, akajiweka sawa kwa lolote, maana machale yalishaanza kumcheza.
Simu ya dereva ikaita, alipoitoa na kuitazama kwenye kioo chake, jina lililojitokeza likamtisha, lakini hakutaka kuonyesha hofu yake. Akaipokea na kusema neno moja tu “Yes”.
Jibu hilo lilimtosha mpigaji aliyekuwa ameegesha gari katika njia ambayo gari lile lilikuwa linapita. Ndani ya gari lile kulikuwa na watu wanne, wote wakiwa na bunduki. Walishajiandaa kwa mauaji na uporaji fedha!
Walikuwa wamesimama eneo ambalo ndilo lilipangwa kwa ajili ya shambulizi la kushtukiza, ambalo kwa mujibu wa mipango ya awali, lingetakiwa kumwacha hai dereva tu, ikibidi akiwa na majeraha kidogo kwa sababu yeye ndiye mkuu wa mipango!
Ilikuwa ni kwenye kona, ambapo hata hivyo kulikuwa na eneo pana la kuweza kupishana magari hata matatu. Ni kona ambayo hakukuwa na nyumba ambayo mlango wake wa kutokea au kuingilia uliiangalia barabara. Lilikuwa ni eneo zuri kwa wapanga mashambulizi, kwani kama lingeweza kuchukua muda mfupi, wahalifu wangeweza kutoweka bila kipingamizi.
Kundi la akina Beka na Shosi walijaribu mara kadhaa kulipita gari lile ili walikinge kwa mbele, lakini ilishindikana, ama sababu ya magari mengine kupishana au wembamba wa barabara.
Ghafla wote wakakumbuka kama kuna eneo lile la kona, wakawapigia simu vijana wa Kinyarwanda ili wafanye kila wanachoweza kumpita na kwenda kulisubiri eneo lile.
Walipokubaliana, nao wakakanyaga mafuta na kuwahi eneo la tukio. Bila kujua, wakawa wameegesha wakiwa wameangaliana uso kwa uso na gari lililokuwa mbele yao. Wote hawakujua walilisubiri gari moja, lenye fedha..!!
Inaendelea.
Chanzo: Globalpublishers

No comments:
Post a Comment