Ghafla wote wakakumbuka kama kuna eneo lile la kona, wakawapigia simu vijana wa Kinyarwanda ili wafanye kila wanachoweza kumpita na kwenda kulisubiri eneo lile. Walipokubaliana, nao wakakanyaga mafuta na kuwahi eneo la tukio. Bila kujua, wakawa wameegesha wakiwa wameangaliana uso kwa uso na gari lililokuwa mbele yao. Wote hawakujua wanalisubiri gari moja, lenye fedha.
Sasa endelea..
Sean Jackson, askari wa kikosi maalum cha kupambana na ujambazi, alikuwa ameegesha pikipiki yake yenye namba za kiraia pembeni ya kituo cha daladala cha Afrikana, kisha yeye mwenyewe akaenda kukaa katika mbao za kituo hicho, macho yake yakiwa yanaangaza kila kona ya eneo hilo, kuangalia mambo yanavyokwenda.
Ulikuwa ni mpango maalum wa jeshi la Polisi kuweka askari karibu kila kwenye mkusanyiko, ili angalau kuweza kuwahi au kuhisi matukio yanayotokea. Katika kila umbali wa mita 200 kulikuwa na vijana maalum wasio na sare. Tokea mfumo huu ubuniwe, umeonyesha mafanikio makubwa kwani ujambazi wowote uliofanyika katika maeneo waliyokuwepo, watuhumiwa wote walikamatwa.
Akiwa kituoni hapo, aliliona gari la Night Support likitoka katika kituo cha mafuta, alielewa utaratibu wa usafirishaji wa fedha na alijua lilikuwa na fedha ndani yake. Alilitupia macho wakati likimpita pale alipokuwa na aliendelea kuwa nalo likienda.
Wakati akitaka macho yake yaachane na gari hilo, akapata mshtuko mkubwa baada ya kuliona likikata kona na kupita njia ya uchochoroni. Haikuwa kawaida.Haraka akaifuata pikipiki yake, lakini kabla ya kuwasha, akapiga namba za kampuni ile ya ulinzi, kwani alikuwa na simu za kampuni zote za ulinzi jijini, kwani majukumu yao kuna wakati yaliingiliana.
“Kuna gari lenu limekuja huku Afrikana, lina ratiba gani leo,” Sean alisema kwenye simu mara baada ya kujitambulisha.“Sean vipi kaka, hapa wanaonekana wamefuata hela pale petrol station kupeleka benki kaka,” alijibiwa upande wa pili.
Akakata simu, akawasha pikipiki yake, lakini simu yake ya mkononi ikaendelea kupiga huku na kule, akakanyaga mafuta kiasi hadi alipokuwa umbali wa mita hamsini kutoka lilipo gari lile lenye fedha, katikati yake kukiwa na magari manne.
Akawasiliana na Polisi Kawe, ambako baada ya kuwaelezea hali hiyo, gari tatu zenye polisi waliovalia kiraia zikatayarishwa. Kwa kuwa waliifahamu njia hiyo, walijua maeneo ambayo yangeweza kutumika kwa ujambazi wa kupora fedha kama kulikuwa na mpango huo.
Gari la kwanza likaenda kuegeshwa katika kona inayotokeza barabara ya Mbezi chini kutokea barabara ya Bagamoyo, palepale ambako gari lenye fedha litatokezea. Pikipiki za polisi, maarufu kama Tigo nazo zikawa tayari, zikiwa karibu kabisa na eneo la tukio.
***
Mle ndani ya gari, Meneja akaanza kuhisi hali ya hatari, jinsi magari yalivyokuwa yakimpita na macho yao kwake, yakampa mashaka, akapeleka mkono wake kwenye mfuko alioweka bastola yake, ilikuwepo.
Akaichomoa na kumwambia dereva; “Nahisi kama kuna hatari, kuwa makini.”
Kauli ile ilimpa mshtuko mkubwa sana dereva, lakini akajikaza. Akajiuliza amejuaje, lakini hata hivyo akamdharau, kwa sababu alikuwa na uhakika ana dakika chache tu za kuishi. Akakanyaga mwendo na mara akaingia eneo la kazi!
Watu waliokuwa katika mpango mmoja na dereva walikuwa wa kwanza kulianzisha, mtu aliyekuwa amekaa upande wa abiria kwenye gari hilo dogo, akatokeza na bunduki na kumlenga Meneja ambaye alishamuona na akalala chini haraka. Risasi zilikichakaza kioo cha mbele cha gari lile na kuwashtua askari wawili waliokuwa siti za nyuma.
Wakafungua milango na kutoka nje, lakini wakakutana na risasi zilizowaua palepale. Jamaa wakawa wanakimbia kulielekea gari lile. Kundi la akina Beka likapatwa na mshangao mkubwa kuona mchezo ule, wakausoma haraka na wale vijana wa Kinyarwanda wakatoa ishara ya kuwataka akina Beka kutulia.
Ni mpaka waliposhambulia sehemu ya kuhifadhia fedha kwa ajili ya kulifungua, ndipo na wao walipoanza kurusha risasi zilizowaua watu watatu kati ya wanne waliokuwepo, kisha wakakimbilia na kwenda kutoa mifuko ya fedha.
Mfuko wa kwanza mkubwa ulioshushwa ukarushwa kwa akina Beka waliosogea na pikipiki yao, wakakanyaga mafuta kuondoka kwa kasi eneo lile, Shosi akiwa dereva, Beka amekamatia fuko katikati, mkono mmoja ameinua juu bastola, akipiga risasi ovyo.
Je, nini kitatokea? Usikose kufuatilia simulizi hii ya kusisimua katika toleo lijalo.
Chanzo: Globalpublishers

No comments:
Post a Comment