Social Icons

Sunday, 8 February 2015

Jaji Mutungi: Vyama vyote vya siasa ni sawa


Dar es Salaam. Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi amesema, ofisi yake haina chama kikubwa na kidogo na kwamba inahudumia vyama vyote vilivyosajiliwa kwa hadhi inayofanana.

Akizungumza juzi, Jaji Mutungi alisema ofisi yake inavitambua vyama 22 na itatoa huduma zinazofanana kwa hadhi sawa ya ulezi wa vyama.

Kauli ya Jaji Mutungi imekuja huku mgogoro wa Chama cha Siasa cha ACT-Tanzania ukifika katika ofisi yake kutafuta suluhu baada ya viongozi wake wa muda kutofautiana.

“Vyama vyote (mpaka sasa vipo 22 vyenye usajili wa kudumu)...hakuna chama kidogo au kikubwa kwangu na hii dhana sijui ya chama kikubwa imetokea wapi, hii haipo kwangu.”

Utashi wa nchi

Kwa upande mwingine, Jaji Mutungi amewataka wanasiasa kuweka mbele utashi wa kisiasa wakati wa kutekeleza majukumu yao ili kuepusha migogoro ya mara kwa mara ndani ya vyama vyao.

Mlezi huyo wa vyama vya siasa alisema, “Kinachotakiwa ni vyama kujiendesha kama taasisi na siyo mtu, chama kikiwa kama taasisi hii migogoro haiwezi kuwapo na mimi tangu nimeingia hapa sijawahi kupewa shinikizo na mtu yoyote yule ili nikipendelee chama fulani.”

Akizungumzia mgogoro uliopo wa ACT-Tanzania, Jaji Mtungi alisema baada ya kusikiliza pande zote mbili zinazosigana alisema, “Nahitaji kupata muda, weledi na umakini katika kufanya uamuzi...Sitaki kukurupuka baadaye nionekane labda napendelea mtu fulani.” ACT kimekuwa katika misigano baada ya viongozi wake wa muda kutofautiana katika Kikao cha Halmashauri Kuu ya chama hicho iliyokutana mwezi uliopita, kumvua uongozi Mwenyekiti wake wa muda, Kadawi Limbu kwa tuhuma za kukiuka Katiba na kanuni ya chama hicho.

Wengine waliovuliwa uongozi ni Naibu Katibu Mkuu (Bara), Leopold Mahona na Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana, Grayson Nyakarungu.

Uamuzi huo pia uliwavua uanachama Richard Mwigamba na mshauri wa chama, Profesa Kitila Mkumbo.

Limbu

Mwenyekiti wa muda wa ACT-Tanzania, Kawawi Limbu alisema anachofahamu yeye hakuna uchaguzi unaoendelea ndani ya chama hicho kwa sasa. “Suala letu lipo kwa msajili na ukweli utadhihirika lakini mimi bado ni mwenyekiti,” alisema Limbu.

No comments:

 
 
Blogger Templates