Kulikuwa kimya, hakuna mtu aliyeonekana ametoka, hakuna sauti iliyosikika kuomba msaada. Wakazidi kusogea, tochi zikiwaka, zikasogea zaidi na kulikuta gari limelala mtaroni!
Michirizi ya damu ilionekana ikitoka ndani ya gari na kusambaa katika mtaro.
Mtu mmoja akakumbuka kuangalia namba za gari, alipoziona na kuhakiki, akapiga kelele!
“Festo huyu jamani, atakuwa amekufa, maskini weee!”
Watu wakazinduka, haraka wakalifuata gari ili kulikagua. Wakakuta watu wawili wamekunjwa. Ilikuwa rahisi kumtambua Festo, licha ya kuwa alikuwa amebanwa sana, lakini mwanamke aliyekuwa upande wa dereva, aliwasumbua watu kumtambua mara moja. Hakukuwa na dalili za uhai kwa watu hao, maana wote walionekana wametulia, hakuna aliyeonyesha kuhangaika!
Baada ya kazi kubwa, dakika 45 baadaye, walifanikiwa kuitoa miili ya watu wale wawili waliokuwa ndani. Wanawake walikaa mbali, wakilia, hasa baada ya kutambuliwa kwa Festo, wakabakia wameziba midomo yao wakitafakari mtu wa pili angekuwa ni nani.
Nywele bandia alizovaa Asfat mara ya mwisho, ndizo zilizowafanya waliomuona jioni hiyo, kutambua kwamba ndiye alikuwa abiria mwingine kwenye gari lililopata ajali ile mbaya.
Maiti wale wakapakiwa katika gari, wakakimbizwa hospitalini kwa uhakika zaidi. Katika hospitali ya Mwananyamala, daktari alithibitisha kwamba wawili hao walikuwa wamefariki!
***
Nyumba zile majirani zilipata msiba mkubwa wa ghafla, maneno, kama ilivyo kawaida yakaanza kutolewa na watu wa karibu. Katika miaka yote ya urafiki wao, kujuana kwao, haikuwahi kutokea hata mara moja kwa Asfat na Festo kuwa karibu kiasi hata cha kupanda gari moja. Tukio lile liliwashangaza wengi, akiwemo mama yake Asfat.
“Mume wangu, nina mashaka sana,” Mama Tonny alimuambia mumewe, wakiwa wawili chumbani kwao, wakati ndugu wakiwa nje ya nyumba yao.
“Juu ya nini mama Tonny, usiwe na mawazo sana, tuzidi kumshukuru Mungu,” mumewe alimwambia, akiwa hana wazo lolote kichwani mwake.
“Festo kaniulia tena mwanangu,” Mama Tonny alisema, huku machozi yakiendelea kumtoka. Tokea alipopata taarifa ya kifo cha Asfat, machozi hayakuwahi kukoma kutoka, ilishageuka sehemu ya maisha yake.
“Ni ajali, mbona na yeye amekufa? Usimlaumu marehemu, tuwaombee wote wapate mapumziko mema kwa Mungu,” alisema mumewe.
“Hapana, roho yangu inasita kumsamehe, amemuua makusudi mtoto wangu, alipania kumuua,” Mama Tonny alizidi kulia.
“Kama ni mtu kusababisha kifo, basi ni Asfat ndiye kamuua mwenzake kwa sababu yeye ndiye alikuwa anaendesha,” mumewe alisema huku akifikiria kifo cha mtoto wake mwingine aliyekufa kwa ajali, Santo.
“Asfat aendeshe gari la Festo, wapi na wapi. Lile gari na ule mwendo ni wa Festo, kila mtu anasema ulikuwa ni mwendo mkali sana kama anavyoendeshaga,” Mama mtu alizidi kutoa machozi wakati akizungumza.
***
Katika nyumba ya jirani, kwao akina Festo, wazazi nao walikuwa chumbani kwao, kila mmoja akiwa na yake kichwani. Ni mama ndiye aliyeanza kuzungumza juu ya msiba huo mkubwa.
“Asfat ameamua kulipiza kisasi kwa Festo,” alisema kwa sauti ndogo, maneno yaliyomshtua sana mumewe!
“Kwa nini unasema hivyo, kisasi cha nini?” mumewe aliuliza.
“Yule mtoto hakuwahi kukubali kama Santo aligongwa na gari kwa bahati mbaya, siku zote aliamini Festo alifanya makusudi. Ni dhambi, lakini acha nipate, simpendi kabisa huyu mtoto, ingekuwa amri yangu, maiti yake ningeitupa porini iliwe na wanyama,” mama aliongea kwa uchungu, machozi yakimtoka.
“Wewe ulijuaje?” mzee Linus, sasa akiwa ametoa macho aliuliza kwa shauku.
“Haikuwa siri, kila mtu hapa mtaani alijua jinsi alivyokuwa akimzungumzia Festo,” mama aliongeza.
“Eti?” baba mtu aliuliza tena, sasa akiwa amesimama na kuvuta kumbukumbu kwa hisia kali!
Itaendelea,
Chanzo: Globalpublishers
No comments:
Post a Comment