Kwa ujumla makubaliano ya kusitisha mapigano mashariki mwa Ukraine kati ya vikosi vya serikali na vya waasi, Minsk II, yameanza rasmi licha ya kugubikwa na ufyatulianaji risasi wa hapa na pale.
Wanajeshi wa Ukraine wakicheza mpira karibu na Debaltseve siku ya tarehe 15 Februari 2015, ishara ya kuanza kwa usitishaji mapigano.
Milio ya risasi iliendelea kusikika hadi usiku wa kuamkia Jumatatu (16 Februari) kwenye maeneo kadhaa mashariki mwa Ukraine, muda mchache kabla ya kuanza rasmi kwa muda wa kusitisha mapigano, lakini kufikia usiku wa manane takribani maeneo mengi yalikuwa kimya.
Hata hivyo, waasi walisema kuwa wasingetekeleza makubaliano hayo kwenye eneo la Debalseve ambako wamewazingira wanajeshi wa Ukraine, huku msemaji wa jeshi la Ukraine akisema kwa kiasi kikubwa usitishaji mapigano unaheshimiwa, licha ya kwamba wanajeshi wake wameshambuliwa zaidi ya mara 10 tangu makubaliano kuanza. Hakuna mwanajeshi aliyeuawa.
Gavana wa mkoa wa Luhansk anayeelemea upande wa serikali, Hennadiy Moskal, aliliambia shirika la habari la Reuters kuwa kuna sehemu ya waasi ambao hawayatambui makubaliano hayo. "Leo saa sita na nusu usiku walirusha makombora yao kwenye eneo la Hirsk, kijiji kiitwacho Toshkovka. Mchana wake walivurumisha maroketi 40 kwenye mkoa wa Luhansk unaodhibitiwa na serikali. Kwa hivyo, kwa hakika wanajaribu kuyavunja makubaliano ya Minsk kwa lengo la kumvunjia heshima Igor Plotnisky ambaye hawampendi."
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ambaye alichangia kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa mkataba wa Minsk II kusitisha mapigano ya Ukraine.
Igor Plotnisky ni kiongozi wa Jamhuri wa Watu wa Luhansk, serikali iliyojitangazia uhuru wa mkoa huo, ambaye alisaini makubaliano ya Minsk kwa niaba ya wapiganaji wa waasi.
Wasiwasi wa jamii ya kimataifa
Jumuiya ya Usalama na Ushirikiano barani Ulaya, OSCE, ambayo ndiyo yenye dhamana ya kufuatilia usitishaji huo wa mapigano, imesema waasi waliwakatalia kuingia kwenye mji huo wa Debaltseve, wakisema kuwa haumo kwenye makubaliano hayo ya Minsk.
Akizungumza na Rais Petro Poroshenko wa Ukraine, muda mfupi kabla ya kuanza kwa muda wa kusitisha mapigano, Rais Barack Obama wa Marekani alielezea wasiwasi wake juu ya ghasia kwenye mji wa Debaltseve.
Obama alizungumza pia na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, ambaye ndiye aliyewezesha kupatikana kwa makubaliano hayo ya Minsk, akiwa na Rais Francois Hollande wa Ufaransa katika mazungumzo yaliyowashirisha Rais Poroshenko wa Ukraine na Vladimir Putin wa Urusi.
Makubaliano hayo, ambayo yalipatikana baada ya mazungumzo ya usiku kucha kati ya mataifa manne siku ya Alhamisi mjini Minsk yanakusudia kuanzisha eneo lisilo shughuli za kijeshi na kuondolewa kwa silaha nzito.
Zaidi ya watu 5,000 wameshauawa kwenye mzozo huo ambao umepelekea suitafahamu kubwa kati ya Urusi na mataifa ya Magharibi kuwahi kushuhudiwa tangu kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia.
Siku ya Jumatatu, Umoja wa Ulaya ulichapisha orosha mpya ya raia wa Ukraine na Urusi wanaolengwa na vikwazo vya Umoja huo kwa kile kiitwacho kuhujumu uhuru wa Ukraine, ambayo inawajumuihsa manaibu waziri wa ulinzi wa Urusi, Arkady Bakhlin na Anatoly Antonov na pia naibu mkuu wa majeshi, Andrei Kartapolov.
Chanzo: Dw.de
No comments:
Post a Comment