Majeshi ya Ukraine na ya waasi wanaoungwa mkono na Urusi bado hawajaziondoa silaha kali kutoka kwenye mpaka wa uwanja wa mapambano mashariki mwa Ukraine. Silaha hizo zilipaswa kuanza kuondolewa leo Jumanne.
Silaha kali za kila upande zilipaswa kuondolewa kuanzia leo kwenye mpaka wa uwanja wa mapambano,kwa mujibu wa makubalinao ya kuyasimamisha mapigano yaliyofikiwa baina ya viongozi wa Ujerumani, Urusi,Ufaransa na Ukraine. Kila upande uliashiria hapo jana kuwa utaziondoa silaha zake ikiwa mwingine nao utafanya hivyo.
Waasi waendelea kuyashambulia majeshi ya Ukraine
Msemaji wa majeshi ya Ukraine Anatoliy Stelmakh ameeleza mapema leo asubuhi kwamba wapiganaji wa waasi wameendelea kuyashambulia majeshi ya Ukraine. Msemaji huyo ameeleza kwenye televisheni kuwa msingi wa kuondolewa silaha kali kwenye uwanja wa mapamano ni kutekelezwa makubaliano ya kuyasimamisha mapigano kwa ukamilifu. Bwana Stelmakh amesema ikiwa waasi wataziondoa silaha zao nzito,majeshi ya Ukraine nayo yatafanya hivyo mara moja.
Waasi wapanga kufanya mazungumzo juu ya silaha kali
Hata hivyo shirika la habari la Urusi,RIA limemnukulu kiongozi wa waasi Andrei Purgin akisema kuwa waasi hao wanaoungwa mkono na Urusi wanapanga kufanya mazungumzo baadae leo na wajumbe kutoka pande tatu juu ya kuziondoa silaha hizo. Pande hizo ni Ukraine, Urusi na Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya, OSCE.
Wakati huo huo viongozi wa Ujerumani,Urusi na Ukraine wamekubaliana juu kuchukuliwa haua madhubuti za kuwaruhusu wajumbe kutoka shirika hilo la OSCE kusimamia utekelezaji wa makubaliano ya kuyasimamisha mapigano ambayo mpaka sasa yanaendelea kutikatika. Taarifa juu ya makubaliano hayo imetolewa leo mjini Berlin.
Hatua hizo zilikubaliwa kwenye mazungumzo ya simu baina ya viongozi wa Ujerumani,Urusi na Ukraine. Taarifa imesema lengo la makubaliano ni kuwaruhusu wajumbe wa shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya kufuatilia utekelezaji wa kuyasimamisha mapigano baina ya majeshi ya Ukraine na wapiganaji wa waasi mashariki mwa nchihiyo, hatua muhimu ikiwa ni kuziondoa silaha nzito za kila upande.
Mapigano yaendelea licha ya makubaliano
Mapigano yamekuwa yanaendelea katika sehemu ya Debaltseve licha ya kufikiwa makubaliano ya kuyasimamisha mwishoni mwa wiki iliyopita. Hata hivyo wajumbe wa Umoja wa Ulaya na wa Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya wamesema kuwa kwa jumla hatua ya kusimamisha mapigano inatekelezwa katika sehemu zingine zote ukiondoa Debaltseve.
Mapigano baina ya majeshi ya Ukraine na wapiganaji wa waasi wanoungwa mkono na Urusi yameshasababisha vifo vya watu zaidi ya 5600 nchini Ukraine tokea vita vianze mnamo mwezi wa Aprili mwaka uliopita.
Ukraine na nchi za magharibi zinailaumu Urusi kwa kuchochea ghasia kwa kuwapeleka askari wake na silaha mashariki mwa Ukraine.Hata hivyo Urusi wakati wote imeyakanusha madai hayo.
Chanzo: dw.de
No comments:
Post a Comment