Social Icons

Thursday, 12 February 2015

Nimrod Mkono anavyowatesa wapinzani Musoma Vijijini


Hata hivyo, katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, ulilishuhudia jimbo hili likienda mikononi mwa chama cha upinzani, huku CCM ikiambulia patupu

Jimbo la Musoma Vijijini

Jimbo hili linapatikana katika W ilaya ya Musoma Vijijini, mahala alipozaliwa, kukua, kucheza na kusoma, mwasisi wa Taifa letu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Hata hivyo, katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, ulilishuhudia jimbo hili likienda mikononi mwa chama cha upinzani, huku CCM ikiangushwa vibaya.

Wakati huo, mshindi alikuwa ni Balozi Paul Ndobho ambaye aliungwa mkono na wananchi wengi, huku Taifa likishangazwa na msimamo wa Mwalimu Nyerere wakati huo, kumuunga mkono mgombea huyu wa NCCR na kumuacha yule wa CCM.

Katika uchaguzi wa mwaka 2000, CCM ilipeperushiwa bendera na mwanasheria maarufu Nimrod Mkono. Huyu inasemekana hakuwa anapatana na Mwalimu Nyerere na alirejea na kuwa na nguvu ndani ya CCM mara tu baada ya Mwalimu kufariki. Sababu za tofauti zake na Mwalimu hazielezwi kwa uwazi.

Hata hivyo, Mkono alishiriki msiba wa Mwalimu Nyerere kwa hali na mali na baadhi ya wanafamilia wanasema alitoa mchango mkubwa. Nikukumbushe kwamba Nimrod Mkono alipita bila kupingwa katika jimbo hili mwaka 2000, hii ilimshangaza kila mtu, kwamba jimbo ambalo baada ya kuongozwa na upinzani, ghafla uchaguzi unaofuatia linatoa mbunge kutoka CCM na akapita bila kupingwa!

Baada ya miaka mitano ya uongozi wa Nimrod Mkono, ilitarajiwa kwamba angepata upinzani mkubwa katika uchaguzi wa mwaka 2005, lakini kichekesho kingine kikatokea, vyama vya upinzani havikuweka wagombea. Kuna wagombea kadhaa kutoka vyama vya Chadema, CUF na vingine walijitokeza na kuchukua fomu za ubunge, lakini hawakurudisha fomu hizo. Hadi sasa haifahamiki kuna nini nyuma ya pazia kuhusiana na tabia hii ya wagombea wa upinzani kuchukua fomu na kutojitokeza tena hasa katika Jimbo la Musoma Vijijini.

Mwaka 2010 kulikuwa na dalili kuwa Mkono angeweza kuangushwa na makada wenzake wa CCM katika kura za maoni. Watu wengi walisubiria jambo hili litokee bila mafanikio yoyote. Mkono akavuka kigingi cha kura za maoni na akapitishwa kuwa mgombea. Kwa sababu ari ya upinzani katika nchi ilikuwa kubwa hasa katika majimbo ya Mkoa wa Mara, wengi walitarajia kuwamba Mkono atakutana na mpinzani mwenye nguvu na labda anaweza kuangushwa.

Jambo la aibu lilijitokeza tena, wagombea wa upinzani walimiminika kuchukua fomu za ubunge kutoka kila kona na kisha siku ya kuzirudisha zaidi ya wagombea 10 walitomokea kusikojulikana. Hii ndiyo Musoma Vijijini na kama hapa pana ‘ndumba’ ilishatupwa baharini!

Ikiwa vyama vya upinzani vingeendelea kusimamisha mgombea thabiti mwaka 2000, 2005 na 2010, naamini jimbo hili lingerudisha historia ya kurudi mikononi mwa upinzani. Hata hivyo, kuna uwezekani mkubwa kwamba Nimrod Mkono akakwaa kisiki katika uchaguzi wa mwaka 2015. Ilivyo ni kuwa kama siyo ndani ya kura za maoni za CCM basi anaweza kuangushwa kirahisi na mpinzani imara atakayejitokeza.

Kuanguka kwa Mkono na hata CCM yenyewe kunachachewa na mabadiliko ya kiutawala yaliyofanywa hivi karibuni, ambapo jimbo la Musoma Vijijini limegawanywa na kuwa wilaya mbili, wilaya ya Butiama na Wilaya ya Musoma Vijijini.

Kwa kanuni hiyo ya ugawaji, haitawezekana ufike mwezi Oktoba mwaka huu kukiwa na wilaya mbili zenye mbunge mmoja. Inategemewa kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi italigawa jimbo la Musoma Vijijini ili kupata majimbo ya Butiama na Musoma Vijijini.

Chanzo: Mwananchi

No comments:

 
 
Blogger Templates