Dar es Salaam. Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha-Rose Migiro amesema kila kata nchini itapata nakala 300 za Katiba Inayopendekezwa ili kuwawezesha wananchi kuisoma na kushiriki katika Kura ya Maoni iliyopangwa kufanyika Aprili 30, mwaka huu.
Amesema mpaka kufikia Februari 9, mikoa 11 nchini ilikuwa tayari imepatiwa nakala hizo na kwamba Serikali imepanga kuchapisha nakala milioni 2 kwa ajili ya kuzisambaza nchi nzima.
Amesema nchini kuna zaidi kata 3,800 na lengo la Serikali ni kusambaza nakala hizo kwenye vijiji, vitongoji na mitaa kupitia Ofisi za wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi wa halmashauri za miji, manispaa na majiji.
Akizungumza na Mwananchi leo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, (Terminal one)
akitokea mkoani Dodoma, Dk Migiro alisema mbali na nakala hizo, Katiba Inayopendekezwa pia imewekwa katika tovuti za Wizara ya Katiba, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Bunge.
“Wananchi waliokuwa katika miji na vijiji siyo wote wanaweza kupata nakala katika mtandao. Ukiwa na nakala halisi unaisoma wakati wote kwa hiyo Serikali imekuwa na nia ya kuwapatia watanzania nakala halisi haraka iwezekanavyo,” alisema.
Alisema Serikali ilipoanza mchakato wa uchapaji wa nakala hizo liliibuka tatizo la mitambo kwa baadhi ya wachapishaji na hivyo kuchelewesha kuzigawa, lakini kwa sasa nakala nyingi na zinaendelea kusambazwa kadri zitakavyokuwa zikichapwa.
“Karibu nusu ya mikoa yote imepelekewa nakala hizo. Tumeweka utaratibu mzuri ambao kila mkoa utapata nakala kutokana na wingi wa kata zake, hatuwezi kugawa nakala sawa kutokana na kutofautiana kwa idadi ya kata” alisema.
Aliitaja mikoa ambayo imepata nakala hizo na idadi yake katika mabano: Katavi (15,640), Rukwa (27,040), Ruvuma (47,740), Mbeya (78,640), Simiyu (34,840), Mara (52,540), Tabora (58,540) na Kigoma (41,440).
Mikoa mingine ni Kagera (54,340), Geita (36,940), Mwanza (57,040) na Pwani ambapo usambazaji umeanza kwa wilaya ya Mafia ambayo imepata nakala 2,400.
Alipotakiwa kufafanua kama nakala hizo zitatosha ikilinganishwa na idadi ya Watanzania alisema, “Jambo la muhimu ni utolewaji wa elimu kuhusu Katiba Inayopendekezwa. Nakala hizi zinatosha kwa sababu Katiba ni waraka wa kisheria unaweza ukausoma na bado ukabaki kuhoji baadhi ya mambo.”
Alisema nakala 1,800,000 zinasambazwa Tanzania Bara na nakala 200,000 zinasambazwa Zanzibar.
No comments:
Post a Comment