Social Icons

Friday, 20 February 2015

Project ondoa Mwakyembe yapamba moto


JIMBO la Kyela mkoani Mbeya, kwa kipindi hiki si mtaji wa kisiasa pekee bali ni kimaslahi zaidi, watu wanahaha kuingia kwenye mitandao ya urais watengeneze fedha.

Wakati kwenye majimbo mengine mkoani hapa, wanachama wa vyama mbalimbali vya siasa wanahaha huku na kule kujitambulisha kwa wapiga kura, Kyela ni tofauti. Ni Project Ondoa Mwakyembe.

Baadhi ya wanachama wa CCM wameungana na wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuendesha mkakati kujenga taswira ya kutokubalika kwa Mbunge wa Jimbo hilo, Dk. Harrison Mwakyembe. Chadema wao wanaamini ni Project inayowasaidia kupenya kwenye jimboni, ambalo huko nyuma liliwasumbua kiasi cha kukiri hadharani.

Katika uchaguzi wa mwaka huu ni tofauti, ikiwa ni kuanzia ule wa serikali za mitaa, wameweza kujijenga, anagalau pale mjini.

Baadhi ya viongozi waandamizi wa chama na serikali, wamekuwa wakiyatazama mambo yanayoendelea wilayani humo kwa jicho la tahadhari zaidi, ambapo wanabainisha kuwa ni mkakati wenye lengo la kumuondolea umakini katika kazi zake za kitaifa na kubaki akihangaika na siasa za jimbo.

Thamani ya jimbo hilo kuelekea Uchaguzi Mkuu, baadaye mwaka huu imepanda kwa kasi ya ajabu katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni kutokana na kuongezeka kwa kasi ya wasaka urais nchini, ambao katika mikakati yao hawawashughilikii wanaonyesha nia pekee, bali hata walio kimya, waliowapa jina la “silent candidates.”

Mbunge wa Jimbo hilo la Kyela, Dk. Mwakyembe amewekwa kwenye orodha ya “silent candidates,” kwa maana ya Watanzania wenye uwezo lakini wako kimya japo waweza kuingia wakati wowote, na kwa mtazamo wao anahatarisha nafasi zao.

Kambi za urais zajenga ngome mkoani Mbeya;
Katika kufanikisha mkakati wake huo, moja ya kambi za urais inadaiwa kununua majengo Kyela Mjini na jijni Mbeya, zikiwemo hoteli mbili na nyumba za kuishi mbili.

Jijini Mbeya inatajwa hoteli moja maeneo ya Sae pamoja na nyumba ya kuishi iliyokuwa ikimilikiwa na mmoja wa wafanyabiashara maarufu jijini humo. Na kwa Kyela mjini inatajwa moja ya hoteli kubwa mjini humo pamoja na nyumba ya mmoja wa wastaafu wa utumishi wa umma.

Taarifa za ndani ya CCM mkoani hapa zinabainisha kuwa hoteli na nyumba hizo hutumika kuwahifadhi wapambe wa kambi ya mwanasiasa mwenye kuusaka urais, wawapo jijini Mbeya au Kyela.

Pamoja na ununuzi wa nyumba hizo, mkakati huo unahusu matumizi ya mitandao ya kijamii, ambapo imefunguliwa kwa lengo la kuendesha siasa za jimbo hilo tu la Kyela. Mada zinazoingizwa kwenye mitandao hiyo ni zile zenye kujenga taswira ya Wilaya ya Kyela kutokuwa na jambo lolote la maana linalofanyika.

Hata hivyo, ni hoja zinazojadiliwa katika mitandao hiyo zilizowafumbua macho wakazi wa Mkoa wa Mbeya, hivyo kuanza kuhoji, kulikoni. Ni baada ya kuona ni mwendelezo wa mashambulizi dhidi ya mbunge huyo, mashambulizi yenye lengo la kufifisha taswira yake.

Vurugu zilizojitokeza wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge, Miundombinu, zilizidisha mashaka miongoni mwa wana CCM mkoani humo kiasi cha kuamua kumchunguza Mwenyekiti wao wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Gabriel Kipija.

Taarifa toka ndani ya vikao vya CCM Wilaya ya Kyela zinabainisha kuwa mwenyekiti huyo alikiri kuandaa vurugu zile na kwamba aliwasiliana na Prof. Juma Kapuya kumuomba kibali, ambapo pia alimwomba ahakikishe wananchi hao hawabughudhiwi na vyombo vya dola, kwamba polisi wasiwasumbue wananchi kuwatawanya kama wahalifu.

Taarifa hizo, ambazo hata hivyo chanzo kimeomba kutotajwa jina kwa sababu suala hilo lipo ngazi ya mkoa, zinabainisha kuwa walianza kushuku nyendo za mwenyekiti wao tangu mapema mwaka jana, na kwamba ilipofika mwezi Julai aliitwa kuhojiwa naye akakanusha.

“Tulimhoji akakanusha, nasi tukamwambia sawa na tumefunga hiyo hoja, lakini tuliendelea kumchunguza na kupata ushahidi wa kila jambo analolifanya dhidi ya chama,” anasema kiongozi mmoja wa juu ndani ya chama hicho.

Katibu wa CCM Mkoa wa Mbeya, Mwangi Kundya, anathibitisha kuwapo kwa tuhuma dhidi ya Mwenyekiti huyo wa Halmashauri ya Kyela zilizowasilishwa ofisini kwake, zikiwamo za usaliti kwa chama chake.

“kimsingi vikao vya wilaya vimetoa mapendekezo yake, kesho (kwa maana ya jana 17/02/2015), Kamati ya Usalama na Maadili inaenda Kyela, itasikiliza pande zote,” anasema Katibu huyo akithibitisha kupokea tuhuma hizo.

Kipija amepinga tuhuma hizo na kutishia kuwafikisha mahakamani walioanzisha jambo hilo. Katika mahojiano yake ya simu na Raia Mwema anadai kuwa ni njama zinazosukwa kumdhibiti asiwanie ubunge wa jimbo hilo la Kyela.

Hata hivyo, taarifa za ndani ya CCM kuhusu mwenendo wa mwenyekiti huyo zinabainisha kuwepo kwa mahusiano yenye shaka kati yake na Chadema, mahusiano ambayo yalikiwezesha kupata ushindi mkubwa katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Kyela Mjini.

Mtandao wa mtafuta urais, unaelezwa kujipenyeza katika mtafaruku huo ndani ya CCM Wilaya ya Kyela na tayari majina kadhaa wilayani humo, yakiwemo ya wana CCM, na watumishi wa umma, yanatajwa kuwemo kwenye mtandao huo.

Jimbo jipya hewa lagonganisha vichwa
Katika mkakati huo, wapo wenye kuamini kuwa katika uchaguzi wa mwaka huu, Kyela itakuwa na majimbo mawili, wakitegemea kuanzishwa kwa Jimbo jipya la Kyela Mjini, hivyo kuingia kwenye harakati za kumdhoofisha mbunge huyo ili asijikite pale mjini na badala yake aendelee na Jimbo la Kyela Vijijini ambako wanadai si rahisi kuwabadili wananchi mitazamo yao juu ya mbuge wao.

Baadhi ya wenye nia ya kuwania ubunge wilayani humo, wanaelezwa kuitumikia kambi hiyo ya urais, wakiamini kuwa nguvu ya kifedha ya kambi hiyo itawawezesha kuifikia ndoto zao.

“Hawa wengine wameingia katika mradi huu wakiliwinda jimbo hewa, Kyela Mjini, lakini wanasahau kuwa wanayemshambulia ndiye mwenye turufu,” anasema mzee mmoja, mdau wa siasa za Kyela.
Hadi tunaenda mitamboni majina ya wenye nia na jimbo hilo hayako wazi, bali yanayotajwa zaidi ni yale yaliyomo kwenye mkakati huo wa kumshughulikia Mbunge wa Jimbo hilo, Dk. Mwakyembe.

Dk. Mwakyembe mwenyewe hadi sasa hajatamka iwapo atagombea tena nafasi hiyo au la, wala kuzungumzia kuwania nafasi ya urais. Kinachoendelea mpaka sasa ni hisia za watu.

“Hii vita ni kubwa kuliko mnavyodhani. Mtu hajatangaza kugombea watu wanamwaga fedha kumshughulikia, kama wana nguvu zaidi yake si wangesubiri wapambane kwenye sanduku la kura, hii vita ni zaidi ya ubunge,” anasema kiongozi mmoja wa CCM mkoani hapa.

Zipo taarifa zilizovuja, kwamba Chama cha Mapinduzi hivi sasa kinafuatilia mienendo ya wanachama wake wenye nia ya kugombea uongozi katika Uchaguzi Mkuu ujao, ambapo wale wote watakaobainika kukichafua chama hicho kwa lengo la kujijenga kisiasa wataenguliwa.

Uchunguzi kuhusu mienendo ya wanachama wake hao, unafanyika katika maeneo mengi, lakini kubwa ni kwenye mitandao ya kijamii, ambako wanachama hao huendesha kampeni zenye kukipaka matope chama chao, kwa lengo la wao kujijenga kisiasa. -

Chanzo: Raiamwema 

No comments:

 
 
Blogger Templates