Social Icons

Friday, 20 February 2015

Uvamizi wa Ukraine mbinu ya mabeberu kuizingira Urusi


KILA kukicha hali inazidi kuwa tete nchini Ukraine kutokana na kupinduliwa kwa serikali iliyokuwa na uhusiano wa karibu na Urusi na madaraka kushikwa na watawala wanaofadhiliwa na mataifa ya Magharibi.


Wakati Urusi imevinjari ikipinga kujiingiza kwa mataifa ya NATO na Umoja wa Ulaya (EU) katika ‘uwanja’ wake, na Marekani nayo imeamuru ndege zake 12 za kivita aina ya F-16 pamoja na manowari USS Truxtun na USS George H W Bush kusogea karibu na mipaka ya Urusi.


Hali imezidi kuharibika pale watawala wapya wa Ukraine walipoamua kupiga marufuku Kirusi kama lugha rasmi. Kwa upande mwengine, bunge la jimbo la Crimea limeidhinisha kura ya maoni kuhusu kujitenga na Ukraine na kuungana na Urusi. Wananchi walio wengi katika jimbo hili wana asili ya Urusi

Rais Barack Obama ametangaza kuwa uamuzi huu wa Crimea eti ni ‘tishio kwa usalama’ wa Marekani na sera yake ya mambo ya nje. Kwa Urusi pia kujitenga kwa Ukraine na kufungamana na EU ni tishio kwa usalama wake, pamoja na kusogezwa kwa vituo vya kijeshi vya NATO karibu na mipaka yake. 


Ukraine ilipata kuwa sehemu ya muungano wa Kisovieti (USSR). Mapema miaka ya 1990, baada ya miaka mingi ya vita baridi, USSR ikasambaratika na Ukraine ikajitangazia uhuru wake baada ya asilimia 90 ya wananchi wake kupiga kura wakisema wanataka kujitoa. Sasa jimbo lake la Crimea linataka kujitoa Ukraine na kurejea Urusi.


Kwa maneno mengine, wakati ule ilikuwa “sisi wa-Ukraine na wao Warusi.” Sasa ni “sisi wa-Crimea na wao wa-Ukraine” 

Baadhi ya mataifa yaliyojitoa kutoka muungano wa USSR yalijiunga na EU na shirika la kijeshi la NATO. Ukraine ilishikilia msimamo wa kutofungamana licha ya mbinu zilizofanywa na mataifa ya Magharibi kwa lengo la kueneza himaya zake kwenye mipaka ya Urusi.


Sasa baada ya serikali kupinduliwa watawala wapya wa Ukraine wanaelekea kujiunga na Umoja wa Ulaya (EU), kitu ambacho kinapingwa na Urusi. Matokeo yake ni kuwa jimbo moja la Crimea limeamua kujitoa na kubaki na Urusi na jambo hilo nalo linapingwa vikali na nchi za Magharibi.


Tatizo lilianza kujitokeza hadharani Novemba mwaka jana wakati wapinzani walipokataa kutekeleza makubaliano waliyosaini na serikali chini ya uangalizi wa EU. Hakuna hatua iliyochukuliwa na EU dhidi ya wapinzani, badala yake ikaendelea kuwasaidia.


Ndipo yakafanyika maandamano dhidi ya Rais Victor Yanukovich. Kufikia Januari waandamanaji wakaanza kutumia nguvu pamoja na silaha. Watu kadha wakauawa na Yanukovich akalazimika kukimbilia Urusi na nafasi yake ikachukuliwa na Olexandr Turchynov.


“Kosa” la Yanukovich ni kuwa alikataa kujiunga na kambi ya EU na akaendelea kushirikiana na Urusi ambayo iliipa Ukraine msamaha wa deni la dola bilioni 20 na punguzo la theluthi ya bei ya gesi kutoka Urusi. Asilimia 55 ya gesi inayotumika Ukraine inaagizwa kutoka Urusi.


Kwa upande wa pili EU na IMF ziliahidi mkopo wa dola bilioni nne kwa masharti magumu. Masharti ni kuwa serikali ya Ukraine iache kutoa ruzuku katika bidhaa muhimu kama petroli na gesi, ikiongeza maradufu bei ya umeme, ipunguze thamani ya sarafu yake na kubana matumizi katika huduma za kijamii kama afya na elimu pamoja na msaada kwa wazee. Pia ilitakiwa iruhusu uuzaji wa ardhi yake yenye rutuba kwa wawekezaji wa nje.


Watanzania watakumbuka jinsi IMF na wafadhili walivyotulazimisha kutii masharti yao miaka ile chini ya kile walichokiita “kufufua uchumi” wakati wananchi wengi wakikiita kufifisha uchumi.


Yanukovich alikataa kujiunga na EU. Ndipo Magharibi ikaja juu na maandamano makubwa yakaanza hadi Februari mwaka huu. Yanukovich akafanya mazungumzo na Ujerumani, Ufaransa na Poland na wakakubaliana kuwa uchaguzi ufanyike baada ya mwezi mmoja. Hata hivyo Magharibi (hasa Marekani) ilikuwa imekwisha kuamua kuwa serikali ipundiliwe.


Zikachukuliwa  hatua za kuunga mkono makundi ya upinzani na kuyashawishi yafanye maandamano na vurugu dhidi ya Yanukovich. Haya ni makundi yenye siasa na itikadi kali za mrengo wa kulia na za ki-Nazi.


Baadhi yake yana historia ya kushirikiana na fashisti Adolf Hitler wakati wa Vita Kuu ya Pili.  Ni makundi haya ndiyo leo yanayoshika madaraka nchini Ukraine yakisaidiwa kwa hali na mali na mataifa ya Magharibi, angalia magazeti kama ‘Die Welt’ (Ujerumani) na ‘Time’ (Marekani).


Ndiyo maana wakati maandamano yanaendelea mawaziri wa mambo ya kigeni kutoka Ufaransa, Ujerumani na Poland (wakiwakilisha EU) waliwasili mji mkuu wa Kiev na kumwambia Yanukovych afanye mazungumzo na wapinzani wake. Huo ukawa mwanzo wa kuangushwa kwake. Kwani wapinzani walikataa kutekeleza makubaliano hayo ya 21 Februari 2014 na wakaendelea kutumia nguvu na silaha kuiangusha serikali. EU ikakaa kimya na kuangalia licha ya malalamiko kutoka Urusi na Ukraine.


Ukweli ni kuwa makubaliano hayo yalikuwa ni mbinu tu za kuwawezesha wapinzani wanyakue serikali. Hiyo ilidhihirika katika mazungumzo ya siri yaliyofanywa kwa njia ya simu baina ya naibu waziri wa mambo ya nje wa Marekani anayeshughulikia Ulaya Mashariki, Victoria Nuland na balozi wake mjini Kiev, Geoffrey Pyatt.


Wakati wa vurugu Nuland aliwasili Kiev mara nne, akigawa zawadi kama mikate na biskuti kwa waandamanaji. Pia alikutana na viongozi wa upinzaani. Mbinu hizi zilianza zamani. Marekani imekuwa ikiingilia mambo ya ndani ya Ukraine tangu miaka ya 1990. Imetumia zaidi ya dola bilioni 5 kuwatayarisha wapinzani. Haya yalisemwa na waziri Nuland mwenyewe.


Kutokana na vurugu zilizotawala mitaani, serikali ililazimika kuachia madaraka pamoja na wabunge wa chama tawala cha Party of Regions ambacho kilipigwa marufuku. Kukipiga marufuku chama hiki ni kuwanyima wananchi uwakilishi wao waliouchagua kwa ridhaa yao. Hayo ndio mabadiliko yaliyoungwa mkono na Magharibi.


Ni mabadiliko ambayo yalikwenda kinyume na makubaliano wakati Rais Gorbachov alipokubali kuisambaratisha USSR. Wakati huo Rais George H W Bush alimuahidi kuwa NATO haingenyemelea mipaka ya Urusi kwa kuingia katika mataifa yaliyokuwa chini ya USSR (Warsaw Pact).


Hata hivyo, Rais Clinton alivunja ahadi hiyo na NATO leo imeweka silaha zake katika nchi takriban 12 zilizokuwa katika mfumo wa Warsaw. NATO imeweka makombora katika jamhuri ya Czech na inanuia kufanya hivyo katika Poland.


Yaani tayari NATO ina vituo vya kijeshi kaskazini na mashariki mwa mipaka ya Urusi na sasa inanyemelea Ukraine iliyo kusini mwa Urusi. Wachambuzi wanajiuliza iwapo Marekani ingekubali kama Urusi ingefanya hivyo katika mipaka yake.


Hivyo, hatua hii ya mwisho ya kuingilia Ukraine imeichafua zaidi Urusi. Siyo tu Ukraine ina wananchi wengi wa Kirusi kutokana na historia ndefu, bali mamilioni ya Warusi walijitolea roho zao ili kuilinda nchi hiyo isitekwe na majeshi ya Nazi kutoka Ujerumani yaliyoongozwa na Hitler.


Hii sera ya kupanua mipaka ya ubeberu si jambo geni. Aliyekuwa waziri wa usalama wa Marekani, Bw Zbigniew Brezenski amesema katika kitabu chake  kiitwacho “The Grand Chessboard: American Primacy and Its Geostrategic Imperatives(link is external) alichokiandika mwaka 1998 kwamba uwezo wa Marekani kueneza himaya yake ulimwenguni inategemea jinsi itakavyodhibiti nchi za Ulaya Mashariki.

Ni sera hii ndiyo iliyoifanya Marekani itoe Itikadi ya Monroe mnamo 1825 ikisema kuwa mataifa ya Marekani Kusini yako chini ya himaya yake. Sera hii inaendelea hadi leo. Ndiyo maana Waziri Kerry alitamka katika baraza la Seneti mwaka jana kuwa Marekani Kusini iko “uwani kwetu” (our backyard).


Sera hii ndiyo iliyoifanya Marekani ivunje rekodi ya dunia katika kuzishambulia kijeshi na kuzikalia nchi za kigeni katika muda wa karne iliyopita. Haya yameorodheshwa na Dak Zoltan Grossman katika tovuti yake(link is external). Halafu Obama eti anamuonya Rais Putin kuwa akiingilia Ukraine basi atakiona cha mtema kuni, kwa sababu atakuwa anahalifu sharia ya kimataifa?


Chanzo: Raia mwema

No comments:

 
 
Blogger Templates