Tanga. Tukio la kurushiana risasi kati ya polisi wakishirikiana na askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) dhidi ya watu wanaosadikiwa kuwa majambazi au magaidi limeacha maswali 10 muhimu yanayolifanya lionekane lenye utata.
Mpaka sasa hakuna taarifa za kina juu ya tukio hilo lililotokea siku nne zilizopita na kusababisha kifo cha mwanajeshi na wapiganaji wengine zaidi ya sita ambao hawajajulikana kujeruhiwa.
Jana katika mkutano wake na waandishi wa habari Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Magalula Said Magalula alijaribu kujibu baadhi ya maswali hayo ambayo yamewafanya wananchi wa Tanga na mikoa mingine nchini, kupata taharuki na kufananisha tukio hilo na matukio ya kigaidi yanayotokea katika nchi mbalimbali duniani.
Hata hivyo, majibu ya Magalula, kama ilivyokuwa katika taarifa ya awali iliyotolewa na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja, yaliwaacha waandishi wa habari na maswali mengi kuliko majibu, kwani mbali na kuwatoa hofu wananchi, kuna maswali aliyajibu kwa kifupi bila ufafanuzi wa kutosha, hivyo kuzidi kulifanya tukio hilo kuwa na utata.
Swali la kwanza ambalo wananchi wanajiuliza ni iwapo tukio hilo ni la kigaidi au ujambazi?
Akijibu swali hilo na kukataa kuulizwa swali la aina hiyo tena, Magalula alisema tukio hilo ni la ujambazi.
Kauli ya mkuu huyo wa mkoa inafanana na ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Mathias Chikawe ambaye juzi aliliambia gazeti hili kuwa tukio hilo ni la uhalifu wa kawaida.
Alisema polisi wanafahamu kuwa kuna hali ya hatari na wameshaongeza ulinzi katika maeneo yote, kwamba juhudi zaidi zinaendelea kufanyika ili kulinda usalama wa raia na kuifanya Tanzania ibaki kuwa kisiwa cha amani.
Swali la pili, waliohusika katika mashambulizi hayo ni raia wa nchi gani?
Magalula alisema swali hilo halina majibu na kwamba majibu yake yatapatikana baada ya kukamatwa kwa watu hao wanaosadikiwa kuwa ni majambazi.
Juzi, Kamishna Chagonja alikaririwa akisema mapigano hayo yalifanyika katika msako wa majambazi walioiba silaha kwenye kituo cha polisi mkoani Tanga, huku taarifa nyingine zikisema mmoja wa watuhumiwa tayari alikuwa mikononi mwa polisi.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi Makosa ya Jinai nchini (DCI), Diwani Athumani alisema matukio ya uhalifu yanayotokea nchini ni mapya na yanayochochewa na ukuaji wa teknolojia ya habari na mawasiliano.
Swali la tatu ni iwapo wahalifu hao waliuawa katika mashambulizi au walitoroka na walipita wapi?
Katika majibu yake Magalula alisema hakuna mwili wowote ulioonekana au kuokotwa na operesheni ya kuwasaka bado inaendelea.
Swali la nne, ni juu ya eneo la Amboni yalipotokea mashambulizi kama lina mapango yanayoishia mkoani humo au yanatokezea hadi nchi jirani kama inavyodaiwa?
Pamoja na Magalula kusema kuwa kuna simulizi nyingi ambazo hazina uhakika juu ya pango hilo, mkazi mmoja wa eneo hilo ambaye hufanya kazi ya kupiga picha alisema eneo la Amboni lina jumla ya mapango 13 yaliyogunduliwa lakini yanayotumika ni mawili. Mapambano yamefanyika katika pango la mbali na lile linalotembelewa na wageni.
Swali la tano, ni juu ya waliojeruhiwa katika tukio hilo?
Magalula alisema waliojeruhiwa ni askari wa JWTZ na polisi na wamelazwa katika hospitali ya Bombo, lakini hadi sasa hawajatajwa majina.
Mbali na maswali hayo, pia wananchi wanajiuliza maswali mengine ambayo ama hayajapata majibu au majibu yake hayajawaridhisha, kama vile, Je, lengo la uvamizi lilikuwa nini, mtuhumiwa aliyekuwa anashikiliwa na polisi alitorokaje, je, alikuwa amefungwa pingu na iwapo sasa kuna uhakika wa usalama?
Maelezo ya ziada
Akitoa maelezo zaidi juu ya tukio hilo, RC Magalula alisema hadi jana mchana hakukuwa na mtu yeyote aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo.
Alisema kufuatia hali hiyo, maofisa wa vikosi vya ulinzi na usalama wameahamia kwenye mapango mengine ili kujiridhisha kama wahalifu hao watakuwa wamejificha huko.
“Kama inavyofahamika eneo la Amboni lina mapango zaidi ya 13, hili lililofanyiwa mashambulizi liko umbali wa kilomita tano kutoka lile linalotumika kwa utalii, kwa hiyo ili kujiridhisha ni lazima maofisa wakague sehemu zote,” alisema Magalula.
Mkuu huyo wa mkoa alisema hali sasa imerejea kuwa shwari na amewataka wananchi kuendelea na shughuli zao.
Alipotakiwa na waandishi wa habari kufafanua kwanini aseme hali ni shwari wakati hakuna hata jambazi aliyekamatwa wala silaha zilizotumika kuwashambulia askari akiwamo Sajenti Said Kajembe aliyeuawa, Magalula alijibu kwa kifupi kuwa ni kwa sababu vyombo vya ulinzi na usalama vimeshatafuta kila pembe ya Tanga na kujiridhisha.
“Serikali ina mkono mrefu imeshatafuta kila pembe ya Tanga na imejiridhisha kwamba hali ni shwari na ndiyo maana nipo hapa kuwaeleza wananchi waendelee na kazi zao,” alisema Magalula.
Eneo la utalii
Kuhusu eneo la utalii la mapango ya Amboni, Magalula alisema halikuguswa wala wahalifu hawakuwa wamejificha huko na ndiyo maana shughuli za kuwapokea na kuwatembeza wageni zilikuwa zikiendelea.
Mwananchi ilikwenda katika lango kuu la mapango ya utalii ya Amboni ambako mhifadhi mkuu, Jumanne Gekora alisema tukio la mashambulizi limeathiri shughuli za mapango hayo.
Mhifadhi huyo aliviomba vyombo vya habari viifahamishe jamii kwamba sehemu iliyoshambuliwa si hapo kwenye utalii bali ni umbali wa zaidi ya kilomita tano na ni mapango ambayo hayapo hata kwenye utaratibu wa kuwatembeza wageni.
Hospitalini Bombo
Habari kutoka hospitalini walikolazwa majeruhi watano ilielezwa kuwa hali zao zinaendelea vizuri ingawaje bado waandishi wa habari hawajaruhusiwa kwenda kuwaona na hawakutajiwa majina yao.
Wakati huohuo askari aliyeuawa katika mashambulizi hayo,Sajent Said Kajembe (47) wa kikosi cha 37 JWTZ amezikwa leo katika kijiji cha Bungu kata ya Dindira Wilayani Korogwe akiwa ameacha mjane na watoto watatu.
Mdogo wa marehemu, Bakari Kajembe alisema familia yao imepokea kwa masikitiko kifo hicho kwa sababu Sajenti Said alikuwa tegemeo kwao kutokana baba yao kufariki dunia miaka ya nyuma.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment