Social Icons

Tuesday, 17 February 2015

Hadithi: Familia tata- 26


“Vifaa vyangu vinaonyesha kila kitu, kuna kitu kibaya sana kinaelekea kutokea kwenye wakati wowote kuanzia sasa,” alisema na kuwazidishia siyo tu mshangao bali hofu ndani ya mioyo yao.
Sasa endelea...

“Hebu tueleze vizuri bwana mtaalamu, unajua utatuua kwa presha,” mzee Komba alimwambia mganga huyo, kwani maneno yake yalimfanya ahisi baridi mwili mzima.

Mganga akawaelezea kwa kifupi jinsi jirani yao alivyokuwa akipanga mipango ya kuwadhuru na kuwasifu kuwa waliamua wakati muafaka wa kwenda kwake ili aweze kuwalinda. Baada ya maelezo hayo, akataka kusikia kama wana lolote.

“Sisi hatutaki ubaya nao, lakini hatutaki watudhuru, watakachotaka kutufanyia kiwarudie wenyewe,” alisema mkewe mzee Komba na kuungwa mkono na mumewe ambaye alitingisha kichwa kuonyesha kukubaliana naye.

Mganga kusikia hivyo akakubaliana nao na kabla ya kufanya kitu chochote, aliwauliza maswali kadhaa kuhusu familia yao, kama vile idadi ya watoto, kama wana kinga yoyote ya kishirikina waliwahi kupata na vitu vingine kadha wa kadha ambayo yote alijibiwa.

Baada ya hapo akachukua mkeka mdogo, akautandika mbele yao na kuwataka wote kukalia pale, kisha akawafunika kwa kijishuka cheupe, ambacho alikimwagia dawa yenye rangi nyeusi kisha akawanyunyizia na maji huku akizungumza maneno wasiyoyajua, akiwazunguka.

Alipowazunguka kama mara tatu hivi, aliwafunua na kuwataka kurejea walipokaa awali, huku yeye akiendelea kuwafanyia mambo. Nusu saa baadaye aliwakabidhi mfuko wenye dawa kadhaa na kumalizia kwa kuwapa maelezo yafuatayo.

“Usiku huu, chimbieni dawa hii (akiwaonyesha aliyoweka katika chupa nne za soda) katika kona zote nne za nyumba yenu, wewe mama utachimbia za kusini na kaskazini, baba mashariki na magharibi. Hii mnatakiwa kunywa watu wote mnaoishi ndani ya nyumba yenu na hii hapa mtajifukisha kila mtu kwa wakati wake lakini kabla jua halijachomoza.”

Wakaondoka kuelekea nyumbani kwao, ambako walifanya kama walivyoambiwa kabla ya kujitupa kitandani kulala, kusubiri kitakachotokea.
***
Saa tano asubuhi vijana wawili wakiwa kwenye pikipiki walikuwa wanarandaranda katika mitaa ya Nakasangwe wakiwa kama watu wanaomtafuta mtu au nyumba. Waliingia mtaa huu na kutokezea mtaa ule, lakini hakuna hata mmoja aliyewatilia maanani.

Baadaye wakaenda Kwa Big Pub, sehemu moja maarufu sana eneo hilo kwa vinywaji. Wakakaa na kuagiza bia. Walionekana kuwa makini na walichokuwa wakikifanya, lakini hakuna hata mmoja aliyewajua wala kukisia walichokihitaji.

Walikuwa wameifuata nyumba ya mzee Komba na walishaiona. Ni Beka na Shosi, vijana wa kazi ambao hufanya kazi na Dayani. Vijana hawa ni hodari katika kuua na kuharibu. Ndiyo waliopewa kazi, siyo tu kumshughulikia Stone, bali pia kufanya na uhalifu mwingine ili kuitia adabu familia nzima.

“Mungu bwana, yaani jamaa huko aliko anapanga mipango yake, lakini hajui kama jua la kesho hataliona, angejua tupo hatua chache kuichukua roho yake angepotelea huko huko aliko,” Beka, akiwa anakunywa bia yake ya pili alimwambia mwenzake kwa sauti ambayo waliisikia wenyewe tu.

Nia yao ilikuwa ni kumuona Stone, kwani kwa jinsi walivyoelekezwa, hawakuwa wamemuona kijana yeyote aliyefanana na sifa zake. Waliendelea kukaa pale wakiwa na vinywaji vyao huku macho yao yakiwa hayauachi mlango wa mbele wa nyumba ya mzee Komba.

Wakiwa katika bia yao ya nne, mlango wa nyumba hiyo ulisikika ukifunguliwa, gari likaonekana likitoka, Beka akainuka na kuifuata pikipiki waliyoipaki pembeni, Shosi alijua anakoenda, hivyo akabaki kimya pale alipokaa.


Inaendelea

Chanzo: Globalpublishers

No comments:

 
 
Blogger Templates