Shosi akawasha pikipiki, wakitaka wapitie katika vichochoro vya upande wa pili wa njia. Ghafla akahisi kama kitu kimemuingia begani, alipojitazama, akaona damu zinatoka. Alipomtazama Beka, akamuona akianguka na fuko lake la hela mtaroni, macho yake yakaanza kuhisi giza, taratibu akapoteza fahamu!
Endelea...
DAYANI, mzee Linus na mkewe walikuwa wamekaa nje ya hoteli waliyofikia, wakibadilishana mawazo kuhusiana na tukio lililotokea, huku akiwahakikishia kuwa vijana wa kazi walikuwa wamekwenda kurekebisha mambo na muda wowote kuanzia wakati huo watachukua kilicho chao.
Mama alionekana mwenye mawazo mengi yaliyotoa ishara kwa Dayani kama wasiwasi, akazidi kumtaka shemeji yake huyo kuamini alichokuwa akikisema.
“Kwa hiyo sasa hawa jamaa zetu ndiyo inakuwaje, tunawaacha?” Dayani aliuliza huku macho yake yakiwa zaidi kwa shemeji yake.
“Hatuwezi kuwaacha, lakini nadhani tubadili mbinu, maana hii ya moto tunaweza kushtukiwa, nyumba mbili mtaa mmoja lazima jamii itashtuka, hii tu yenyewe naona watu wanaanza kunitilia wasiwasi,” alisema mzee Linus, mkewe akitingisha kichwa kukubaliana naye.
“Lakini pia ningependa jambo hili nalo lisichukue muda mrefu, ikibidi misiba iambatane,” Dayani alisema kwa sauti yenye msisitizo. Linus na mkewe walitingisha vichwa kuonyesha kukubaliana naye.
Baada ya kuzungumza kuhusu suala hilo, waliendelea na mambo mengine hadi ilipofika mchana, wakati Dayani alipoaga kurejea nyumbani kwake, akiahidi kuwapigia simu na kuwaeleza kuhusu mzigo wao kabla jua halijazama.
***
Katika chumba maalum kwenye hospitali ya Mwananyamala, watu wawili walikuwa wamelazwa huku miguu yao ikiwa imefungwa pingu, chupa za dripu zikiwa zimefungwa mikononi mwao huku madaktari wawili wakiwashughulikia. Pembeni yao, askari kanzu wasiopungua wanne nao walikuwa wakiangalia kila hatua inayoendelea.
“Hawana majereha makubwa, baada ya kuwatoa hizi risasi, ni majeraha ambayo wanaweza kwenda kuponea nyumbani, kwa hiyo tunaweza kuwaruhusu watoke kesho,” Dr Editha, mwanamama shupavu kwa upasuaji, aliyekuwa daktari kiongozi katika shughuli hiyo, aliwaambia askari waliokuwepo chumbani.
“Vizuri, fanya hivyo, na nafikiri usiwaongeze tena hiyo nusu kaputi, kama majeraha siyo makubwa, basi tunaweza kuongea nao baadaye kidogo,” Inspekta Jonas, mpelelezi kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi alimwambia dokta Editha.
Vitandani, walikuwa ni Beka na Shosi, ambao walipigwa risasi wakati wakijiandaa kutoroka na fuko la fedha baada ya kunusurika ajali. Walikamatwa na fedha zote zikaokolewa. Wale vijana wa Kinyarwanda nao hawakufika mbali, kwani baada ya mmoja wao kupigwa risasi na Sean, wenzake walipojaribu kukimbia kimyakimya, wananchi walianza kuwakimbiza huku wakiwazomea.
Kuona vile wakaanza kupiga risasi ovyo, lakini kadiri walivyokuwa wakipiga na wananchi kukimbia, ndivyo walivyozidi kuwazonga kiasi kwamba wakajikuta wameishiwa risasi, wananchi wakawasogelea na kuwafikia, waliwaangushia kipigo na kuwachoma moto wote watatu.
Askari walijitahidi kuwafikia na kuwatawanya kwa mabomu ya kutoa machozi, lakini hadi walipotawanyika, vijana wale walibakia majivu!!
***
Beka na Shosi wote walirudiwa na fahamu kiasi cha saa kumi jioni, walishangaa kujikuta wakiwa vitandani, miguuni wakiwa na pingu mikononi na chupa za dripu. Wakatazamana na walipogeuza zaidi shingo zao, wakakutana na macho ya watu wasiowafahamu.
“Vipi wazee, salama?” walisalimiwa na jamaa aliyekuwa akitabasamu, mbele yao.
“Salama tu kaka, vipi?” Beka alikuwa wa kwanza kujibu.
“Poa, vipi mnajua hapa ni wapi,” aliwauliza huku vijana wale wakiendelea kushangaa.
Wakatingisha vichwa kuonyesha kutotambua lolote, lakini wakiendelea kujikumbusha. Baada ya kama dakika kumi hivi, Yule mtu aliyekuwa chumbani akawaambia kuwa pale walikuwa hospitalini, na kwamba waliokotwa wakiwa wamejeruhiwa kwa risasi na majambazi..!!!
Beka na Shosi wakatazamana, kwa mbali kila mmoja akaanza kupata picha.
Je, nini kitaendelea? Usikose kufuatilia simulizi hii ya kusisimua katika toleo lijalo.
Chanzo: globalpublishers
No comments:
Post a Comment