Social Icons

Saturday, 21 March 2015

Hadithi: Familia tata - 37


Wakatingisha vichwa kuonyesha kutotambua lolote, lakini wakiendelea kujikumbusha. Baada ya kama dakika kumi hivi, Yule mtu aliyekuwa chumbani akawaambia kuwa pale walikuwa hospitalini, na kwamba waliokotwa wakiwa wamejeruhiwa kwa risasi na majambazi..!!!
Beka na Shosi wakatazamana, kwa mbali kila mmoja akaanza kupata picha.
Sasa endelea...

Inspekta Jonas aliwaangalia wale vijana pale kitandani sura yake ikiwa imejaza tabasamu, kiasi kwamba kadiri Beka na Shosi walivyokuwa wakirejewa na fahamu zao, walishindwa kumwelewa kama alikuwa ni askari au daktari.

“Samahani Bro, sasa wewe ni askari au daktari na tuliokotewa wapi,” Shosi alimwuliza baada ya kuwa ameshakumbuka mchezo mzima ulivyokuwa.

“Mimi ni daktari tu, sielewi lolote, wamewaleta tu hapa na kutuzuia kuuliza kitu chochote, walituambia tu tuwatibu,” Inspekta Jonas aliongopa na wakati huohuo akawaomba udhuru kuwa anatoka kidogo, lakini akawatahadharisha kuwa wasijitingishe sana, maana pingu walizofungwa zinabana kadiri wanavyojitingisha.

Inspekta Jonas akatoka, akiwa ameacha vinasa sauti vilivyofungwa chini ya vitanda vya wawili hao, akaenda nje kuungana na vijana wake waliokuwa wanacheza drafti. Akawaambia kwamba jamaa wamezinduka na amezungumza nao kidogo.

***
Baada ya kutolewa hospitalini kesho yake, Beka na Shosi walipelekwa katika eneo moja lililo katikati ya jiji la Dar es Salaam, lakini lililokuwa kimya sana. Ndani ya nyumba moja kubwa, iliyokuwa haina dalili za kuishi watu, waliwakuta watu kama sita hivi, wakiwa na miili iliyojazia, wenyewe wakisema mabaunsa.

Wakati wakitoka Mwananyamala hospitalini na kuelekea mjini, walijua wanakwenda Kituo kikuu cha Polisi, lakini walipoona wanaingia mjini zaidi, wakaamini wanapelekwa makao makuu ya Polisi, sasa wakajikuta wanachanganyikiwa walipopita makao makuu hayo na kuendelea kuelekea hospitali ya Ocean Road.

Katika kiuchochoro kisafi, wakashangaa zaidi walipoona mlango wa geti kubwa jeusi ukifunguka na gari kwenda moja kwa moja. Gari likasimama ndani na geti likarejeshwa, milango ikafunguliwa na vijana wale wakatolewa mikononi wakiwa na pingu zao. Zikafunguliwa nao wakaelekezwa kukaa kwenye benchi lililokuwa pembeni.

Katika gari waliyokuja nayo, Prado yenye rangi nyeusi, kulikuwa na askari kanzu wanne akiwemo Inspekta Jonas na Sean. Kwenye nyumba hiyo, licha ya wale mabaunsa sita, pia kulikuwa na watu wengine wawili wenye umri wa makamu.

Beka na Shosi waliwatambua watu wawili miongoni mwa wale mabaunsa, ni askari ambao walishawahi kuwaponyoka katika matukio mawili siku za nyuma. Walipotazamana, wale askari walitabasamu, lakini kwa vijana wale, wakasinyaa, ujasiri waliobaki nao ukazidi kutoweka.

“Nadhani mnafahamu kwa nini mpo hapa vijana au nimekosea,” aliuliza mmoja kati ya wale watu wazima wawili baada ya kuwa wamewazunguka pale walipokuwa wamekaa. Beka na Shosi wakatazamana kabla ya kujibu, walionekana kutegeana.

“Nataka kuamini kuwa mnajua. Hawa vijana wenzenu waliojazia, kazi yao ni kuwakumbusha watu kama nyinyi wajibu wa kutambua kilichowaleta hapa, kwa hiyo kama hamjui kilichowaleta hapa niwaruhusu wawakumbushe,” alisema tena yule mzee kwa sauti ya upole sana.

“Lakini kabla sijawaambia wawakumbushe, nataka kuwapa tahadhari, ni watu wachache sana waliowahi kutoka hapa wakiwa hai baada ya kukumbushwa, kwa hiyo ni juu yenu sasa kucheza kamari,” alisema.

“Tunajua mzee,” wote kwa pamoja walijibu, majibu ambayo yalimfurahisha sana yule mzee, ambaye aliwaambia;

“Kitu kimoja cha faida kwenu, tunafahamu nyinyi ni watu wa kutumwa, tunamtaka aliyewatuma na sisi tutawalinda, vinginevyo tutawapoteza na mnayemficha pia tutamfikia, haya nani atatupa mkanda, wewe hapo elezea, nadhani unajua kuwa tunajua ukweli, ole wako utamponza na mwenzio,” alisema mzee huyo akimuonyesha sura ya kutisha Beka aliyeteuliwa kuongea.

Beka akakohoa, kuonyesha kujiandaa kwa ajili ya kutoa maelezo. Yule mzee alimpa kitu kama simu, akimwambia wakati anazungumza akiweke mdomoni mwake, ambacho dhahiri kilikuwa ni kipaza sauti. Macho ya vijana wote wawili yalionyesha woga, kitu kilichowapa nguvu wale watu waliowazunguka…

Chanzo: globalpublishers

No comments:

 
 
Blogger Templates