Social Icons

Saturday, 21 March 2015

Hadithi: Familia tata - 40

Saa moja na nusu baadaye waliingia mjini Morogoro, katika mzunguko wa Msamvu, Dayani akakizunguka na kulielekeza gari njia ya Dodoma.

Kilometa kama kumi, katika eneo linaloitwa Mkundi, akawasha indiketa kuonyesha kwamba anakata kulia, akaingia katika njia ya vumbi na baada ya kama dakika tano, akasimama nje ya nyumba moja kubwa, iliyozungushiwa ukuta mkubwa, mbele ya geti kubwa, akapiga honi!

GETI lilifunguliwa na kijana mmoja mwenye umri upatao miaka kama 16 hivi, lakini aliyeonekana mkakamavu, kutokana na misuli ya mikono yake kutuna. Akaliacha wazi na Dayani akaliingiza gari lake hadi ndani na nyuma yake, geti lile likafungwa.

Akalisimamisha gari hilo katikati ya magari mengine kama sita hivi yaliyokuwa yameegeshwa mle ndani. Nyumba ilikuwa kubwa iliyomshangaza mzee Linus, akamtazama kwa mshangao kidogo na kwa uzoefu wake, akatambua kuwa ile ilikuwa ni maficho yake mambo yanapochafuka.

Dayani akampa ishara ya kushuka, wakateremka na kuufuata mlango mkubwa mbele yao. Akionekana kuwa mwenyeji, aliufungua mlango na kuingia sebuleni. Ilikuwa sebule kubwa pia, ya kisasa ambayo ilikuwa imepangiliwa vizuri sana.

“Karibu Chuga, hapa ndipo yatakuwa makazi yetu kwa muda tukisikilizia kinachoendelea Dar es Salaam, humu ndani kuna kila kitu, tunaweza kukaa mwezi mzima bila kutoka nje,” Dayani alimweleza rafiki yake.
“Nani anaishi humu?” mzee Linus alimuuliza.

“Hii ni nyumba yangu, lakini ni chimbo letu kila linapotokea tatizo. Wanaweza kututafuta dunia nzima lakini wasijue kama tupo hapa. Kama umekaona kale kakijana kalikofungua mlango, wako wenzake kama wanne hivi, ndiyo walinzi na ni vijana wa kazi vilevile, usiwaone vile, wanaweza kuangusha mbuyu wale,” alisema Dayani, maneno yaliyomsisimua mzee Linus.

Dayani alibonyeza kengele moja iliyokuwepo pale sebuleni na baada ya dakika moja, vijana watano wa kiume walikuwa wamesimama mbele yake, wakionyesha nidhamu ya hali ya juu.

“Chuga, kama nilivyosema, hawa ni vijana wetu wa kazi ambao wanaishi hapa. Wanasoma shule moja ipo hapo mbele, lakini pia wanaweza kufanya jaribio lolote la hatari ambalo unaweza kufikiria. Vijana, ni rafiki yangu wa muda mrefu na ni mchapakazi, tumekinukisha Dar, tutakuwa hapa kwa muda,” alisema na kuwatazama vijana wake kwa zamu.
***
Beka alisimamisha gari hatua chache kabla ya kufika nyumbani kwa Dayani, nyuma yake kulikuwa na magari mawili ambayo yalimpita na kwenda moja kwa moja hadi kwenye geti la nyumba yake. Lililokuwa limetangulia lilipiga honi, lakini mlango haukuonekana kufunguliwa.

Mtu mmoja akashuka na kutoa ishara kwa Beka kuteremka, akashuka garini na kumfuata na alipomfikia, akaambiwa agonge mlango.“Najua kuna namna zenu za kuwasiliana, hebu gonga ili ajue kuwa ni wewe,” Yule askari alimweleza.

“Sisi hatujawahi kufika hapa hata mara moja, mikutano yetu yote huwa pale baa au eneo lingine, lakini si hapa, alitukataza kabisa kusogelea nyumba hii,” Beka alimweleza.
Askari wengine wasio na sare walitoka nje ya magari na kusogelea pale mlangoni. Baada ya majadiliano ya muda mfupi, wakakubaliana kwenda kumchukua mjumbe wa mtaa ili aje kusaidia kugonga mlango.
***
Imelda, mke wa Dayani aliyaona magari yote matatu yaliyosimama nje ya geti la nyumba yake na kwa kuwaangalia, aliwatambua kuwa ni askari. Akakumbuka jinsi mume wake alivyomweleza, akaamua kutoroka kupitia handaki maalum lililojengwa ndani ya chumba chao cha kulala.

Dayani alitengeneza handaki ambalo lilitokeza kwa nje, umbali wa kama mita 100 kutoka kwenye uzio wa eneo lake. Sehemu ya kutokea eneo hilo, pia ilikuwa ni eneo lake ambalo alijenga nyumba ndogo iliyokuwa haikaliwi na mtu.

Imelda alivipanga vizuri vitu vyake, akatoa bastola na bunduki moja vilivyokuwemo chumbani, akaingia chini ya uvungu wa kitanda, akafunua mfuniko wa kuingia ndani ya handaki, akaurudishia vizuri, akaanza kuteremka na kutambaa kuelekea nje.

Chanzo: globalpublishers

No comments:

 
 
Blogger Templates