Social Icons

Saturday, 21 March 2015

Hadithi: Familia tata - 39

“Jamaa hajatokea, tufanyeje?” aliwauliza wenzake.
“Hebu wamcheki tena kumuuliza amefika wapi,” mwingine alishauri. Wakakubaliana, wakatoa simu ya Beka na kumpa ili apige tena simu kwa Dayani.
Sasa endelea..

Moyoni, Beka alijua bosi wake ameshashtukia mchezo na kwa jinsi alivyokuwa akimfahamu, hivi sasa atakuwa njiani kuelekea chimbo. Akaichukua simu hiyo na kupiga namba ya Dayani, huku akiwa ameweka laudi spika.

Kule alikokuwa, Dayani aliiona simu ya Beka ikiingia, wakati huo, alikuwa anaingia barabara ya kuelekea Morogoro, inayotokea katika eneo la Tamco, mbele kidogo ya Kibaha mkoani Pwani.
“Hao, wanataka kujua nimefika wapi, ngoja niwasubirishe,” Dayani alimwambia Mzee Linus kabla ya kuichukua simu na kuipokea.

“Yes Beka, niko njiani, hapa Lugalo kuna kafoleni kidogo, nadhani kuna ajali hapo mbele, nisubiri tu nadhani muda si mrefu natia timu hapo, si unajua tena leo bia hadi majogoo..” Dayani alizungumza kwa kujiamini huku akimbinyia jicho mzee Linus aliyekaa pembeni yake.

“Okee bro, maana naona umechelewa sana na si unajua tumeshaleta noma sasa hofu tupu kuwa na huu mzigo,” Beka alizungumza upande wa pili huku wale askari wakitingisha vichwa kuonyesha kukubaliana naye.

Beka na Dayani wakaagana. Akiwa sasa ameshatulia katika barabara hiyo, Dayani alipunguza mwendo pale tu aliposubiri gari la mbele yake kabla ya kulipita na kwenye matuta. Kama watasubiri nusu saa kuanzia muda ule, atakuwa ameshapita Chalinze.

Baada ya kusikiliza mazungumzo ya Beka na Dayani, wale askari wakakutana tena kujipanga upya na majadiliano zaidi. Kiongozi wao, Inspekta Jonas, akiwa ameliegemea Prado, lenye namba za kiraia aliwaambia wenzake.
“Uzoefu wangu wa miaka 15 katika kazi hii, unaniambia kwamba huyu jamaa tunayemsubiri hawezi kufika, ameshashtuka. Huyu jamaa ni jambazi mzoefu, ninamfahamu na tumeshamkosa kosa kwenye matukio mengi sana. Kila siku tunakosa ushahidi ili kumkamata, sasa tujipange kwa ajili ya kumtafuta, siyo kumsubiri tena,” alisema na kuwatazama wenzake, ambao nao walikubaliana naye kwa kutikisa vichwa vyao.
Wakaingia kwenye magari yao, lile la akina Beka likiwa mbele. Beka nyuma ya usukani na Shosi pembeni yake, askari wawili wenye miili mikubwa walikuwa nyuma yao wakiwaelekeza cha kufanya.
“Huwa mnakutana wapi kwa ajili ya kupanga mipango yenu ya uporaji,” askari mmoja aliwauliza wale vijana.

“Mara nyingi huwa ni pale kwenye baa yake ya Zanzi,” Shosi alijibu. Alipowauliza kama kulikuwa na watu wengine zaidi walikuwa viongozi wao zaidi ya Dayani, walikataa na kusema yeye ndiye kila kitu.
***
Dayani alijua wapi anakwenda. Mzee Linus akili yake ilishahama, alijiona mwenye mikosi baada ya jaribio lake la kumdhuru jirani yake, sasa kuonekana kama litamaliza kabisa. Hakuwa na furaha kabisa moyoni mwake, kitu ambacho Dayani alikiona dhahiri.

“Chuga siku hizi umekuwa mlokole sana, yale makeke yako yamepotea kabisa, yaani hapa ni kama niko na mzoga endapo jamaa watatokea na kuanzisha mapambano,” Dayani alimwambia mzee Linus.“Siwezi kuwa na ushujaa na ujasiri kama wa kipindi kile, mimi nimeishi uraiani miaka zaidi ya ishirini bila kumtoa mtu utumbo, sasa wewe kila siku unatoa roho za watu, hatuwezi kufanana,” alisema mzee Linus.

“Ni kweli najua, lakini sasa katika ishu kama hii lazima ukomae, jivalishe ujasiri wa enzi zile za hatari ili tuvuke salama, hili jambo litaisha tu na dhamira yetu itatimia,” alisema Dayani na kupapasa sehemu ya mbele, akafunua eneo moja hivi na kutoa sigara, akaiwasha.

Saa moja na nusu baadaye waliingia mjini Morogoro, katika mzunguko wa Msamvu, Dayani akakizunguka na kulielekeza gari njia ya Dodoma.

Kilometa kama kumi, katika eneo linaloitwa Mkundi, akawasha indiketa kuonyesha kwamba anakata kulia, akaingia katika njia ya vumbi na baada ya kama dakika tano, akasimama nje ya nyumba moja kubwa, iliyozungushiwa ukuta mkubwa, mbele ya geti kubwa, akapiga honi!Je, hapo ni kwa nani? Hekaheka za kutafutana zitafikia wapi? Usikose kufuatilia simulizi hii ya kusisimua katika toleo lijalo.

Chanzo: globalpublishers

No comments:

 
 
Blogger Templates