Social Icons

Saturday, 28 March 2015

Hadithi: Familia tata - 42

“Ndiyo, ile shotgun nimeiacha kwenye mtaro ila ile ndogo ninayo naondoka nayo,” mkewe alimjibu akiwa anatazama huku na huko kuona kama watu wanaweza kumtambua! 
Endelea

Dayani alianza kuhisi hatari kufuatia mazungumzo yake na mkewe, lakini akaamua kukaa kimya bila kumfahamisha rafiki yake Linus juu ya kinachoendelea. Na mkewe Imelda naye ndiyo kwanza aliona kama sinema inaanza, alitamani apate kashikashi ili azidi kukomaa katika kazi za kijambazi.

Mzee Linus alihisi kama kitu usoni mwa rafiki yake, kwani alikuwa na uzoefu naye, ingawa hata hivyo naye hakutaka kumshtua, akabakia kumezea moyoni mwake. Hata hivyo, akataka kujua kuhusu kinachoendelea, akaamua kumpigia simu mkewe.

Simu ya mkewe haikupatikana. Kwa kuwa ilikuwa bado mapema, akaamini ilikuwa kwenye chaji na kwamba angeongea naye muda ukifika. 
**
Mkuu wa kituo cha Polisi Wazo alikuwa anapekua pekua kitabu kikubwa cha ripoti na majalada mbalimbali, alikuwa anatafuta sehemu aliyoandika taarifa iliyomhusu mzee Linus, kumbukumbu ilikuwa bado kichwani mwake kuwa mtu huyo aliwahi kupeleka malalamiko yake kwake.

Mkuu huyo alikuwa pamoja na askari kanzu waliokuwa pamoja na Beka na Shosi, ambao walisharejeshwa kituo kikuu cha Polisi kati. Baada ya kupekuapekua, hatimaye akakuta sehemu palipoandikwa malalamiko ya mzee Linus, aliyekwenda kutoa taarifa ya hofu ya maisha ya mwanaye aliyedai kutishiwa maisha na mtoto wa jirani yao!

“Yaaa, huyu hapa bwana, unaona eeh, alikuja hapa kulalamika kuwa mtoto wake anaweza kudhuriwa na kijana wa jirani yao. Nafikiri ndiyo katika mwendelezo wa vita vyao vya chinichini, ngoja nichukue namba zao niwapigie,” alisema huku akiandika pembeni namba zake.

Akaichukua simu yake na kubonyeza namba za mzee Linus, ambaye baada ya kuziangalia na kutotambua ni simu ya nani, akaamua kutopokea, alishaanza kuhisi mambo kuanza kwenda kombo.
“Mbona hupokei Chuga,” Dayani alimuuliza alipoona anaitumbulia macho simu yake bila kupokea.
“Nahisi kama siyo simu nzuri Chuga,” mzee Lius alimjibu mwenzake.
“Tucheze kamari, hebu pokea,” alimwambia.

Mzee Linus akaipokea na kuipeleka sikioni na kuita Halooo..!
Baada ya kusalimiana, upande wa pili ukajitambulisha na kumweleza kuwa ulikuwa unamhitaji kituo cha polisi kwa mahojiano mafupi, alipouliza ni kituo gani na kutajiwa, akawaambia kuwa alikuwa safarini Dodoma.

“Kama uko Dodoma pia unaweza kwenda kuripoti pale, utaulizwa mambo machache halafu utaendelea na shughuli zako mzee wangu, ni muhimu kidogo,” askari alimwambia mzee Linus kwa sauti ya upole.
Simu ikakatwa na tayari mwili mzima wa mzee huyo ulikuwa umeloa jasho. Akamsimulia alichokisikia na Dayani akatoa tabasamu lisilo rafiki.

“Kimenuka rafiki yangu, wale watoto watakuwa wamebanwa, wametapika hadi utumbo,” alisema Dayani, dhahiri kumuonyesha kwamba mambo hayakuwa mazuri.
“Tunafanyaje sasa?” Mzee Linus alimuuliza Dayani ambaye alikuwa ameinua macho yake juu darini, akionyesha kutafakari sana.

Akilini mwake, alikuwa anajiuliza kama akina Beka walikuwa wanapajua pale Morogoro alipo. Hata hivyo, hakukumbuka kama wale vijana waliwahi kufika pale, ingawa walikuwa wanajua uwepo wa sehemu ya kujificha.

Wakakubaliana wawapigie simu wake zao na kuwaeleza hali halisi ilivyo na kwamba baada ya hapo watazima simu zao na hawatawasiliana kila baada ya saa sita. Dayani alimpata mkewe na kumwelezea walipofikia, lakini simu ya mkewe mzee Linus haikupatikana, kitendo kilichomtia wasiwasi!

Je, mke wa mzee Linus amepatwa na nini? Usikose kufuatilia simulizi hii ya kusisimua katika toleo lijalo.

Chanzo: globalpublishers

No comments:

 
 
Blogger Templates