Wakakubaliana wawapigie simu wake zao na kuwaeleza hali halisi ilivyo na kwamba baada ya hapo watazima simu zao na hawatawasiliana kila baada ya saa sita. Dayani alimpata mkewe na kumwelezea walipofikia, lakini simu ya mkewe mzee Linus haikupatikana, kitendo kilichomtia wasiwasi!
Sasa endelea..
Mzee Linus hakujua nini kilitokea kwa mkewe, kwani tokea alipoondoka ghafla pale hotelini na kumuacha, hakuwasiliana naye tena. Akajaribu kupiga tena na tena hakupatikana. Ingekuwa zamani, angepiga kwa mke wa mzee Komba na kuzungumza naye na kujua nini kimemsibu. Pia kwa wakati ule, angeweza kuwapigia watu kadhaa kule nyumbani kwake, lakini asingeweza kwa sababu mkewe hakuwa kule!
Baada ya kufikiria sana, akaamua kumpigia kijana mmoja aliyekuwa akielewana naye sana kule kwao Nakalekwa, alimzoea kwa jina la Jumba, kutokana na umbo lake kubwa.
“Shikamoo mzee Linus, dah umepotea kabisa,” Jumba alimsalimia mara baada ya kuona namba ya simu ya mzee huyo ikiingia kwenye simu yake, hawakuwa wamewasiliana kwa muda mrefu kidogo.
“Marahaba Jumba, mambo vipi? Bwana nipo si unajua tena haya matatizo niliyopata?” alisema mzee Linus baada ya kupata salamu kutoka kwa Jumba.
“Dah kweli mzee pole sana, umepotea kabisa, haupo mjini nini?” Jumba alimuuliza.
“Yaaa, nipo Dodoma mara moja. Sasa nina tatizo kidogo, najaribu kumpigia mama simpati kwa simu yake, sijui ana matatizo gani,” alisema.“Aisee, lakini na yeye simuoni huku, hata washkaji zangu nao hawapo, leo kama wiki sasa,” alisema Jumba.
“Yaa ni kweli, unajua baada ya tukio lile tulisambaratika kidogo, ila mama yupo kwenye ile gesti ya pale Tegeta, naomba ukimbie mara moja ukamtazame maana nina shida sana, nahitaji kuongea naye,” alisema mzee Linus.
Jumba alikuwa akimuheshimu sana mzee huyo, ingawa alikuwa na kazi zake, akaamua kuahirisha, akatafuta usafiri wa bodaboda, akaenda zake kumfuata mtu ambaye alimuita mama!
**
Stone ambaye bado alikuwa na hasira na familia ya jirani yao, alijiapiza kuwa ni lazima siku moja atalipiza kisasi kwa kifo cha kaka yake Festo, aliyefariki katika ajali pamoja na Asfat, walipokuwa wakirejea nyumbani kutoka kula maisha.
Kariakoo, majira ya saa nane hivi, katikati ya watu wengi katika mtaa wa Kongo, akamuona Maria, dada yake Tonny, msichana wa tatu kuzaliwa katika familia ya mzee Linus. Mapigo ya moyo wake yakasimama kwa muda, hakuamini macho yake.
Yalipoanza tena, akaanza kumfuatilia taratibu, alitaka kujua ni wapi anaishi, kwani sasa alikuwa na nafasi kubwa ya kulipiza kisasi, alijua huyu angemuongoza walipo ndugu zake, maana tokea kuungua kwa nyumba yao, hawakuonekana tena maeneo yale na hawakuwa na mawasiliano.
Maria akiwa hajui hili wala lile, alitembea kwa kukwepa watu na hatimaye akaifikia hoteli moja ya ghorofa iliyokuwa katikati ya mtaa huo. Akaingia na kwenda kukaa katika kiti, muda uleule mhudumu alimfuata na kumhudumia alichohitaji.
Stone alipomuona ameagiza chakula, akaongeza mwendo na kwenda katika mashine ya ATM, akatoa kadi yake na kuchukua kiasi kadhaa cha fedha, hakujua baada ya pale angetumia usafiri gani, kwani kama angepanda teksi, naye angelazimika kuwa na teksi, kama ni bodaboda vilevile na yeye angekuwa vile.
Alipochukua akageuza haraka na kwenda kumchungulia Maria pale alipokuwa, akamkuta ananawa tayari kwa kutoka, akasimama eneo flani hivi kisha macho yake akayakaza katika mlango wa ile hoteli.
Maria akatoka, akaangaza macho huku na kule, Stone akajificha kwenye mojawapo ya nguo zilizokuwa zimetundikwa nje ya duka moja la nguo. Kisha msichana huyo akaanza kuondoka taratibu akiufuata mtaa wa Msimbazi!
Chanzo: globalpublishers
No comments:
Post a Comment