Akili yake ilipokaa sawa, akajaribu kuuliza sababu za yeye kutakiwa kituoni, askari akamshauri kuwa mtulivu kwani suala hilo angeweza kulifahamu mara tu baada ya kufika huko. Akakubali kwa shingo upande kuingia ndani ya gari. Wale watu wengine waliokuwa garini, ambao nao walikuwa bado vijana, walimsalimia kwa heshima na safari ya kuelekea kituoni ikaanza.
Sasa endelea...
STONE aliondoka katika duka lile alilosimama na kunywa soda kwa muda mrefu, akasogea katika pub moja hivi iliyokuwa kwa mbali kidogo na nyumba aliyokuwa ameingia Maria, hata hivyo angeweza kumuona na kumtambua mtu yeyote ambaye angetoka au kuingia.
Pale alipokaa, akaagiza tena soda yake baridi, akaendelea kunywa taratibu huku macho yake yakiwa yameganda pale kwenye nyumba ile. Kwa muda aliokuwa ameshautumia kukaa pale, haukuweza kumshawishi kama ndipo wanapokaa wale majirani zao, kwa sababu hakumuona tena mtu mwingine akitoka wala kuingia anayemfahamu.
Muda wa saa kumi na moja na nusu hivi, macho ya Stone yaliona kitu alichokitaka, Maria, akiwa na nguo zilezile, alitoka akiwa ameongozana na jamaa mmoja hivi, ambaye kwa kuwatazama, walionekana kama wapenzi.
Ndiyo, Jimmy, kijana mmoja mkakamavu alikuwa ni mpenzi wa Maria kwa muda mrefu na pale ndipo alipokuwa amepanga. Kwa muda wote ambao wamekuwa na matatizo, msichana huyo alipata mwanya wa kuwa anakwenda pale mara kwa mara, lakini hakuwa akilala.
Stone akahisi hivyo pia na kwa kuwa walikuwa wanaondoka, akadhamiria kuwafuata tena nyuma, kuona ni wapi ambako Maria angemalizia safari yake. Akamaliza haraka soda yake, akainuka na kuwafuata wapenzi wale ambao baada ya kuingia katika uchochoro na kutokea upande wa pili wa barabara, wakaifuata Bajaj na kujipakiza.
Stone naye akaifuata Bajaj iliyokuwepo eneo lile, akaingia na kumwambia dereva aifuate ile iliyokuwa mbele yake.“Kwani vipi Bro na ile Bajaj?” dereva alimuuliza.
“Kuna jamaa kaingia na demu wangu, nataka kuwafuatilia nijue wanakoenda, sina shida na mwanaume, nataka ushahidi wa kumuacha demu,” Stone aliongopa tena, uongo ambao dereva wa Bajaj aliutilia shaka. Kwa kuwa aliyekuwa akiendesha ni watu wanaofahamiana, akaamua kumtumia ujumbe mfupi wa maneno na kumweleza kuhusu suala hilo.
Dereva wa ile Bajaj baada ya kusoma ujumbe ule, hakutaka kuremba, mara moja akawaambia abiria wake kuhusu kufuatiliwa na mtu nyuma yao.
Maria alishtuka sana kusikia vile, kwani kwa zaidi ya miaka mitatu aliyokuwa na Jimmy hakuwahi kutoka na mwanaume mwingine. Jimmy kwa upande wake, alikuwa mtulivu, akamwambia dereva wa Bajaj aendelee kuwasiliana na mwenzake ili kujua nyendo zake.
Waliuliza kuhusu umbo lake, muonekano wake na sauti yake kama angeweza. Ujumbe mmoja ulioingia ulianza kutoa mwanga kwa Maria na Jimmy, ambao dereva aliwasomea … “Jamaa kavaa tisheti kifuani imeandikwa Join Them.”
“Kuna sehemu nimeshawahi kuiona hii flana, wapi, wapi wapi vile jamani, aaaah kuna mtu namjua,” alilalama Maria aliyekuwa akijitahidi kukumbuka, lakini kabla hajamaliza, Jimmy akaja na wazo.
“Sikia dereva, wasiliana na mwendesha Bajaj mwingine mwambie aje resi amfuate mshkaji wako, akampige picha abiria wake alafu akurushie tumuone huyo jamaa, si inawezekana,” alisema na wote wakakubaliana naye.
Sasa walikuwa wanaingia eneo la Kigogo Sambusa, safari yao ilikuwa ni Kawe, ambako Maria ndipo alipokuwa anaishi.
**
Gari liliingia katika kituo cha Polisi Wazo kwa mwendo wa taratibu, likaenda na kuegeshwa sehemu yake, kisha mama Tonny akateremka na kuwafuata askari waliomsindikiza ndani ya kituo hicho. Akaongozwa moja kwa moja hadi katika chumba kimoja, ambacho hakikuwa na mtu. Akatakiwa kusubiri kwa muda.
Wale askari wakatoka na kumuacha peke yake. Moyoni mwake, alijawa na wasiwasi usio kifani, katika maisha yake yote, hii ilikuwa ni mara yake ya kwanza kukamatwa.Baada ya muda mchache askari aliyemkamata, aliingia akiwa ameandamana na mwanamke mwingine aliyekuwa amevalia kiraia, ambaye baada ya kukaa alijitambulisha kuwa ni askari, mkononi mwake akiwa na karatasi kadhaa.
“Sikia mama, tuna taarifa zote kuhusu kilichofanyika katika nyumba yenu, tunajua wewe pia unajua kilichotokea. Mumeo yuko wapi?” alimuuliza kwa sauti ya upole kabisa.
“Kwa kweli mimi sijui alipo, mara ya mwisho alinipigia simu akisema yupo Dodoma, lakini akaniambia anaelekea Mwanza,” alijibu.“Sasa sikia..” yule mwanamama askari akamwambia mama Tonny!
Chanzo: globalpublishers
No comments:
Post a Comment