“Jamani pole sana, simu niliizima muda mrefu, sikutaka usumbufu, basi asante ntampigia baba nimsikie,” alisema na Jumba akatikisa kichwa huku akiondoka sehemu hiyo.
Sasa endelea...
Jumba alipotoka, mke wa mzee Linus alibonyeza namba za mume wake na haraka sana ikapokelewa. Mzee Linus hakuamini aliposikia sauti ya mke wake, alitambua kwa vyovyote angekuwa mikononi mwa dola. Swali la kwanza alilomuuliza ni kuhusu sehemu aliyokuwepo. Alipojibiwa kuwa alikuwa bado hotelini kwake, alipomua na kumwelezea mambo yote yalivyokwenda hadi pale walipo.
“Kwa hiyo sasa nifanye nini?” mama alimuuliza mumewe.
“Sina uhakika, lakini jaribu kuzima simu, uwe unawasha kila baada ya saa tatu au nne na unipigie nikupe maendeleo, sawa?” mzee Linus alimweleza mkewe ambaye alikubali.
Alipokata simu tu, namba asiyoijua ikaingia katika simu ya mama, akajiuliza maswali mengi kabla ya kupokea. Iliita hadi ikakata. Ilipokata akampigia mumewe kumweleza kuhusu simu hiyo, akamuuliza kama aipokee au la maana aliitilia mashaka. Mumewe akamshauri kupokea lakini kama itakuwa ni ya Polisi, basi adanganye kuwa yupo nje ya Dar.
Namba ileile ikaingia tena, akaipeleka simu sikioni huku akitetemeka. Sauti ya kike ya upande wa pili ilimpa unafuu, akarejesha ujasiri wake na kutulia. Baada ya kusalimiana, aliyepiga alijitambulisha kama mwalimu wa shule anayosoma mwanaye Tonny, kwani alikuwa na siku tano sasa hakuwa amekwenda na hawana taarifa zake.
“Jamani tulipatwa na matatizo, tukajikuta tumechanganyikiwa, nyumba yetu iliungua moto na kuteketea yote, hivyo watoto wote wanaishi kwa ndugu zao ambao wapo mbali na nyumbani,” alisema mama Tonny.
“Sasa kuna fomu zinatakiwa kujazwa na mzazi pia kuchukua ripoti yake ya mwisho wa mwaka, tutafanyaje mama?” Mwalimu alimuuliza.Wakakubaliana aende akachukue, akawaahidi kwenda kesho yake saa nne asubuhi!
Aliamka kiasi cha saa mbili asubuhi, akajinyoshanyosha mwili wake halafu akaingia bafuni kuoga, kisha akavaa nguo zake na kutoka nje, moja kwa moja kwenye mgahawa uliokuwa ng’ambo ya pili ya barabara, akaagiza chai na vitafunwa, alipomaliza kunywa, akachukua bajaj kuelekea shuleni kwa mtoto wake, Mother Of Mercy, Madale.
Alikaribishwa ofisini kwa mwalimu mkuu, ambako baada ya kujieleza, aliulizwa pia kuhusu sababu za mwanaye kutoonekana shule, akaelezea ilivyokuwa. Akapewa pole nyingi, kisha akakabidhiwa ripoti ya mtoto wake ya mwisho wa mwaka.
Aliwashukuru walimu, akajiinua kitini na kutoka nje ambako aliangaza macho na kuliona gari moja dogo jeupe limeegeshwa katika njia ya kutokea nje ya shule, gari hilo halikuwepo wakati akiingia. Hakujali, akaanza kutembea taratibu hadi alipolifikia, mlango wa gari ukafunguliwa na msichana wa umri wa miaka kama 28 hivi akatoka na kumsimamisha.
“Mama shikamoo, samahani..!”
“Marahaba, bila samahani mwanangu, unasemaje,” alimjibu huku akiangalia ndani ya gari, ambako kulikuwa pia na watu wawili, dereva na msichana mwingine aliyekuwa amekaa siti ya nyuma.
“Mimi ni askari polisi kutoka kituo cha Wazo, kuanzia sasa upo chini ya ulinzi na tunaomba tuongozane kituoni kwa mahojiano zaidi,” alisema msichana huyo huku akimtolea kitambulisho, kitendo kilichomfanya mama Tonny kupoteza mawasiliano kichwani mwake kwa sekunde kadhaa!
Akili yake ilipokaa sawa, akajaribu kuuliza sababu za yeye kutakiwa kituoni, askari akamshauri kuwa mtulivu kwani suala hilo angeweza kulifahamu mara tu baada ya kufika huko. Akakubali kwa shingo upande kuingia ndani ya gari. Wale watu wengine waliokuwa garini, ambao nao walikuwa bado vijana, walimsalimia kwa heshima na safari ya kuelekea kituoni ikaanza.
Chanzo: Globalpublishers
No comments:
Post a Comment