“Mmefika wapi,” aliuliza mzee Linus, swali ambalo alijibiwa kuwa ndiyo kwanza wanatoka Kibaha, kabla ya kukata simu.
Sasa endelea...
“Mwenzangu, hapa nilipo nina mawazo kama nini, kwanza hata sijui naenda wapi, sijui huko itakuwaje, yaani sioni hata raha ya simu yenyewe, natamani saa hizi ningekuwa nimesinzia nisahau haya mambo ya dunia,” alisema mama Tonny kumweleza dereva wake.
Ingawa ni kweli kuwa alikuwa amechanganyikiwa, lakini kitu kingine kilichomfanya akose raha na simu yake ni kuwa ilikuwa imeunganishwa na Polisi, ujumbe au maneno yoyote ambayo angeongea na simu yake, yangesikika pia kwao.
Alikuwa na uhakika askari walikuwa hatua chache nyuma yao na hakuona usalama wowote wa yeye, mumewe na mtandao wao wote, akili yake ilikuwa inamtazama mumewe akiwa mahakamani, akihukumiwa kwa uhalifu alioufanya!
**
Jimmy, Maria na dereva wao, badala ya kupita barabara ya Kawawa, wakapinda kushoto na kuelekea Kigogo huku wakiendelea na mawasiliano na mtu aliyekuwa na Stone.
Walifanya hivyo ili kumpa urahisi mtu wa Bajaj ya tatu ili asikumbane na foleni katika barabara hiyo eneo la Magomeni. Walishawasiliana na mwenzao na alikuwa anakuja spidi ili amuwahi mtu aliyekuwa na Stone.
Bajaj ya akina Maria haikuwa inakimbia sana, hivyo na hata ile ya Stone nayo ikawa inakuja mwendo mdogomdogo. Wakati akina Maria walipofika Kigogo Mwisho, Stone alikuwa nyuma yao na Bajaj iliyokodishwa kwa ajili ya kumpiga picha ilishaingia njia hiyo ya Kigogo na ilikuwa hatua chache nyuma ya akina Stone.
Wakatumiana meseji ili azime Bajaj mara moja, ajifanye tatizo la kiufundi ili amuwahi atakaposimama na kumpiga picha. Katika eneo linalojulikana kama First Inn, Bajaj ya mbele ilikuwa inaelekea Mabibo, ya kati ikazimika ghafla.
“Dah, hii ngoma mbona inataka kuzingua, kuna kiwaya kinasumbua, dakika moja bro,” dereva wa Bajaj hiyo alisema huku akishuka, akijifanya kwenda nyuma na kufunua kisehemu kimoja na kujifanya kama anaunga kitu.
Stone aliendelea kubaki kwenye Bajaj lakini macho yake yakiwa yameganda mbele akiwafuatilia kwa makini uelekeo wao. Aliyetakiwa kupiga picha alishafika alipokuwa Stone, akaipaki mbele yao na kumsemesha mwenzake.
“Oyaa vipi imebuma? Ngoja kwanza nikupige picha kwa kumbukumbu yako,” alisema huku akifanya zoezi hilo, akimchukua Stone aliyekuwa hana habari. Aliwaona kama watu wanaofahamiana kutokana na wote kufanya kazi moja. Baada ya kupiga picha mbili tatu, akaondoka zake huku akimtania mwenzake.
Dereva alishamaliza kuunganisha waya aliosema, akarejea kwenye usukani na kuiwasha, kwa spidi kali akaondoka kuifuata Bajaj ya mbele yake.“Khaaa, huyu ni Stone, Mungu wangu, maisha yangu yako hatarini,” alisema Maria mara tu baada ya picha za mtu aliyeko kwenye Bajaj kutumwa kwa dereva wao.
Jimmy alimtazama Stone, hakuwahi kumuona kabla, lakini alipata simulizi zake kutoka kwa mpenzi wake, wakati ule aliosemekana alitaka kumdhuru mdogo wake. Lakini hakuonyesha hofu yoyote, alitaka waendelee na safari hadi mwisho ili waone mwisho wake. Maria alikuwa akitetemeka sana, alitaka kuwataarifu wazazi wake wajue la kufanya.
Jimmy akamtaka kuwa mtulivu na dereva wa bajaj waliyopanda, akataka waucheze mchezo huo waone mwisho wake.“Twendeni mpaka mwisho wa safari, huyu dada akishuka, mimi na wewe tujifanye tunaondoka, halafu tumvizie huyu tuone atafanya nini,” alisema, kauli ambayo iliungwa mkono na Jimmy. Akaongeza kasi na akina Stone nao wakaongeza kasi hadi walipofika katika nyumba moja iliyopo ndani kidogo ya kituo kinachoitwa Kanisani.
Jimmy hakushuka, bali Maria aliteremka na kukimbilia ndani. Stone alimuona na nyumba aliiona. Akaisimamisha Bajaj yao na kutaka kiasi cha pesa zinazotakiwa kulipwa. Alipomalizana naye, akashuka na kuanza kutembea kurudi kituo cha basi.
Jimmy na dereva wake wakarudi na kwenda kupaki sehemu ambayo Stone asingeweza kuwaona. Kwa mshangao wao, Stone hakukaa sana, lilipopita daladala akadandia na kuondoka zake!!
No comments:
Post a Comment