Social Icons

Sunday, 5 April 2015

Hadithi: Familia tata - 49

Jimmy na dereva wake wakarudi na kwenda kupaki sehemu ambayo Stone asingeweza kuwaona. Kwa mshangao wao, Stone hakukaa sana, ilipopita daladala akadandia na kuondoka zake.
Sasa endelea...

Inspekta Jerom, aliyekuwa ameegesha gari lake pembeni ya mzunguko wa Msamvu, Morogoro, aliliona Prado VX lenye rangi ya damu ya mzee kama alivyoelekezwa na wenzake waliokuwa nyuma, walikuwa wametega magari katika njia zote, ile ya kuingia mjini, kuelekea Iringa na Dodoma. Lilipochagua njia ya kwenda Dodoma, askari waliokuwa mbele ya kituo cha mabasi, wakaamriwa kuondoa gari taratibu ili wapitwe wakiwa wanaendesha.

Walipokata tu kona, kama mtu aliyefahamu kwamba walishafika Moro, mzee Linus akampigia simu mkewe na kutaka kujua walipo, na alipoelezwa kuwa walishatoka katika mzunguko wa Msamvu wakielekea Dodoma, akakata simu mara moja na kumgeukia Dayani.

“Wameshapita Msamvu wanakuja,” alimwambia huku akiwa ameshikilia simu yake, kwa shauku.
“Devo anapajua hapa na hata namna ya uingiaji wake anaujua, wewe tulia,” Dayani alimjibu huku akipuliza sigara yake kwa mikupuo ya mfululizo.

Jibu hilo lilimfanya kutokuwa na nia tena ya kumpigia mkewe kama mwanzo, wakaendelea kutazama televisheni ambayo wakati huo ilikuwa inaonyesha marudio ya mpira wa miguu kati ya Brazil na Ujerumani katika fainali za Kombe la Dunia, mechi ambayo iliisha kwa Wadachi kuibuka na ushindi wa mabao 7-0.

Gari alilopanda mkewe mzee Linus lilikuwa limewekwa katikati. Mbele kulikuwa na magari mawili  ya polisi yaliyokuwa na namba za usajili za kiraia na nyuma pia yalikuwa mawili. Yale ya mbele yalikuwa yakipishana, moja likija nyuma ya gari lao na lingine likiwa mbele yao, ili mradi tu hawakuweza kugundua kinachoendelea. Lile gari lililokuja kulisindikiza lile Prado, liliunganisha kituo kikuu cha polisi mjini Morogoro.

Lilipofika na kukata kulia eneo la Mkundi, magari yote mawili ya Polisi yaliyokuwa mbele yalishapita, hivyo ikawa rahisi gari moja likakata kulifuata gari hilo, lakini kwa mbali. Prado lilikwenda likaipita nyumba ya Dayani na kwenda kupaki katika nyumba ndogo iliyokuwa mbele ya nyumba hiyo. Yule dereva aliteremka, akaenda kufungua geti.

Akarudi garini na kuliingiza ndani. Halafu akarejea na kulifunga, kitu kilichowashangaza Polisi. Kwa mujibu wa maelezo waliyokuwa nayo, watu hao wangelakiwa na wenzao, ambao ndiyo hasa waliokuwa wanatakiwa.

Polisi wakapashana kuhusu jambo hilo, askari kanzu wawili wakaachwa kwa mbali kulichunga eneo hilo, wengine wakarejea kituo kikuu kwa ajili ya mazungumzo ya kujipanga, lakini kila mara walikuwa wakiwasiliana na wenzao ili kujua kinachoendelea.

Baadaye, zikaja taarifa kutoka kwa majirani kwamba nyumba ile ilikuwa ikitumika mara chache sana na ni nadra kumuona mtu akiingia na kutoka. Jambo hili nalo liliwatia mashaka Polisi ambao walipanga kufanya shambulio la kushtukiza usiku wa siku hiyo.

Hadi ilipofika saa nne za usiku hakukuwa na mtu yeyote aliyekuwa ametoka, ingawa taa zilikuwa zinawaka ndani, ishara kwamba kulikuwa na watu. Kitu cha kwanza walichofanya polisi, ni kuwasiliana na Tanesco, ili kuzima umeme katika eneo lote lile, zoezi ambalo lilitimia baada ya dakika ishirini.

Umeme ulipokatika tu, askari wawili waliokuwa jirani na nyumba hiyo waliruka ukuta na mmoja akakimbilia katika mlango, mwingine akabingirika na kuingia chini ya uvungu wa gari. Askari wengine walikuwa nje, nao wakasogea katika mlango wa nyumba hiyo lakini kabla hawajafika, taa zikawaka!

Wale wa ndani wakapatwa na taharuki kubwa, lakini kwa mshangao wao, hawakuona dalili zozote kama kulikuwa na mtu. Kwa kutumia ufunguo m****** wakafungua geti, wenzao waliokuwa nje wakaingia ndani. Ua ulikuwa mkubwa, ndani kulikuwa kimya, wakakubaliana kuuvunja mlango. Wakitumia bastola isiyotoa sauti, wakapiga risasi tatu kwenye kitasa, kikaachia, mlango ukafunguka!

Chanzo: globalpublishers

No comments:

 
 
Blogger Templates