Kama ilivyokuwa katika makazi yake ya Dar es Salaam, Dayani pia alijenga nyumba hii kwa ajili ya ulinzi wake binafsi wakati wa matatizo yake ya kihalifu. Nyumba ndogo ambayo Devon na mama Asfat waliingia ilikuwa na sehemu ya kuingilia, yenye ngazi zilizotokeza kwenye nyumba yake na ndimo walimopitia. Kitufe cha njano alicho kibonyeza, kiliziba njia hiyo kwa zege kubwa lililoonyesha kama mwisho wa njia hiyo.
Sasa endelea....
BAADA ya Stone kupanda daladala na kuondoka, walibakia dereva wa Bajaj na Jimmy pale walipokuwa wamejibanza. Wakawa wamebakia kimya kwa muda kabla ya kuanza mazungumzo.
“Una mawazo gani mshkaji,” Jimmy alimuuliza dereva wa Bajaj, ambaye alishajitambulisha kwa jina la Sensei.
“Nadhani jamaa alitaka kujua anapoishi huyu msichana, huenda anajipanga siku maalum ya kuja, nilidhani tungetoa ripoti polisi,” Sensei alimshauri Jimmy.
“Ni kweli, halafu hatuwezi kujua siku gani atakuja, nadhani umetoa ushauri mzuri, lakini sasa wa kuripoti polisi inabidi awe Maria mwenyewe,” Jimmy alikubaliana na Sensei.
Jimmy akatoa simu yake na kumpigia Maria, wakazungumza kuhusu mpango ule, ambao msichana huyo alikubaliana nao. Akatoka nje na wakapanda tena Bajaj hadi Kituo cha Polisi Kawe ambako alitoa taarifa hizo. Askari aliyekuwa akiandika maelezo, alikuwa ni yuleyule aliyeandika maelezo ya baba yake katika Kituo cha Wazo, akamkumbuka Stone.
“Hivi wewe kwenu ni Nakasangwe?” askari alimuuliza Maria, ambaye alishangazwa na swali hilo, ambalo hakulitegemea.
“Ndiyo, umejuaje kama naishi kule wakati nimekuja kutoa ripoti huku,” naye alijibu kwa swali, huku akionyesha tabasamu.
“Kuna kesi kama hii niliandikisha kule Wazo, wewe una mdogo wako ambaye alitaka kudhuriwa na huyuhuyu Stone? Niliandika maelezo yanafanana sana na jina ni hilihili, nyinyi mna matatizo gani ya kifamilia?” aliuliza askari.
Walibadilishana maneno mawili matatu, kisha baadaye wakaondoka. Yule askari alilichukulia suala lile kwa umakini, akapiga simu Kituo cha Wazo na kuwasiliana na wenzake, akawataarifu kuhusu maelezo aliyonayo pale kituoni kwake.
Kikao cha dharura kikaitishwa, ikakubaliwa kuwa kijana huyo atafutwe na akamatwe, kwa sababu kulikuwa na kila dalili za kutokea maafa. Wakati wakipekuapekua mafaili mezani kituoni Wazo, wakakutana na faili la mzee Linus, ambaye watoto wake walikuwa wanatafutwa na Stone!
“Kuna ugomvi mkubwa wa kifamilia baina ya majirani hawa, unakumbuka huyu mzee ndiye aliratibu mpango wa kuchoma nyumba ya mwenzake lakini bahati mbaya wakaichoma nyumba yake mwenyewe? Hawa wanalipiziana kisasi, ni vizuri huyu bwana mdogo akakamatwa kabla hajaleta madhara, maana kuna kesi kubwa inakuja na hawa watu watatiwa mbaroni wakati wowote kuanzia hivi sasa,” mkuu wa Kituo cha Polisi Wazo aliwaambia askari kanzu aliowaita ili kuwaeleza kwa kifupi suala hilo lilivyo.
Wakakubaliana waende kuendesha msako wa kumtafuta Stone na wakati huohuo kuweka ulinzi wa siri nyumbani anakoishi Maria ili kuhakikisha hadhuriwi. Askari wawili waliondoka kuelekea Nakasangwe nyumbani kwa akina Stone na wakapiga simu kituoni Kawe kuwataarifu umuhimu wa Maria kulindwa bila mwenyewe kujua.
***
Stone alifika Kawe tangu asubuhi na mapema. Zamani aliwahi kuishi ndani ya Kambi ya Jeshi ya Lugalo, wakati huo baba yake mdogo akiwa askari miaka ile ya 2000. Alipata kuwa na marafiki sehemu za Ukwamani, Tanganyika Packers, Kanisani hadi Kawe Beach. Alivijua vijiwe vingi vya wavuta bangi na wahuni wanywa gongo.
Asubuhi hii, aliingia katika nyumba moja iliyo pembezoni kabisa na uzio wa kambi hiyo, ambako wanauza gongo na bangi, baadhi ya wateja wao wakubwa ni vijana wa jeshi hilo. Alifahamika na ingawa alikuwa havuti wala hanywi, lakini walimzoea kama mtu wa kijiweni.
Hakumweleza yeyote kilichompeleka hapo, lakini aliwaambia kwamba siku hiyo alikusudia kulala mitaa hiyo na tayari alishafanya miadi ya kulala kwa rafiki yake wa muda mrefu, Alva.
Ilipofika saa tisa, akaamua kusogea karibu na makazi ya akina Maria, kulikuwa na saluni moja ya kiume iliyopo uchochoroni, ambako akikaa aliweza kuona watu wanaotoka na kuingia katika nyumba hiyo.
Alipiga stori hapo hadi saa kumi na moja jioni, alipomuona Maria akitoka. Mavazi yake, yalionyesha alikuwa na mtoko maalum, akapata furaha moyoni mwake. Maria alikwenda hadi kituoni na kuchukua Bajaj. Stone, akiwa amevaa kofia iliyoficha uso, naye alimfuata taratibu..
Je, nini kitaendelea? Usikose kufuatilia simulizi hii ya kusisimua katika toleo lijalo.
No comments:
Post a Comment