Social Icons

Sunday, 5 April 2015

Hadithi: Familia tata - 47


“Sikia mama, tuna taarifa zote kuhusu kilichofanyika katika nyumba yenu, tunajua wewe pia unajua kilichotokea. Mumeo yuko wapi?” alimuuliza kwa sauti ya upole kabisa.
“Kwa kweli mimi sijui alipo, mara ya mwisho alinipigia simu akisema yupo Dodoma, lakini akaniambia anaelekea Mwanza,” alijibu.
“Sasa sikia..” yule mwanamama askari akamwambia mama Tonny!
Sasa endelea...

Mama Tonny alibakia kimya akimuangalia yule askari ambaye alikuwa akizichezea karatasi zilizokuwa mikononi mwake. Akatumia kiasi cha dakika 15 kumuelekeza jinsi ya kufanya kwa ufasaha kabisa bila kukosea, vinginevyo angekosa bahati ya kuondolewa katika shitaka kubwa linalomkabili mumewe pamoja na watu wengine.

“Nadhani umenielewa mwanamke mwenzangu?” askari alimuuliza mkewe mzee Linus, ambaye alitingisha kichwa kuonyesha kuelewa. “Haya sasa, piga,” askari mwanamama alimwambia.
Mama Tonny alibonyeza namba za mumewe, baada ya sekunde chache, mzee Linus aliipokea simu hiyo, kama kawaida akiwa na hofu flani moyoni mwake.

Mkewe alimsalimia na baadaye alimuuliza kama yupo sehemu ambayo anaweza kuongea bila wasiwasi. Akiwa sebuleni kwa Dayani, kule Morogoro, alimtoa wasiwasi mkewe na kumwambia anaweza kuendelea, lakini huku akimkonyeza rafiki yake Dayani.

“Nimepigiwa simu na Polisi, sijui wamepata wapi namba yangu, wanataka niende kituoni eti kuna jambo wanataka kuzungumza na mimi, nimewakubalia, lakini kabla sijaenda nikataka kwanza ushauri wako, niende nisiende?” mkewe aliongea huku askari aliyekuwa naye karibu, akirekodi kwa kuwa simu ilikuwa imewekwa ‘loud speaker’.

“Hebu ngoja kwanza nitakupigia baada ya dakika mbili, ngoja nishauriane na Dayani,” Mzee Linus alisema simuni na kukata. “Safi sana, ninakuhakikishia usalama wako, ni kufuata tu vile tunataka utusaidie,” mwanamama askari alimwambia mkewe mzee Linus.

Dakika mbili baadaye, mumewe alikuwa hewani akimtafuta kwenye simu yake.
“Sikiliza, hawa hawatakiwi kabisa kutupata muda huu, ngoja kwanza tupotee ili angalau tujipange tujue jinsi ya kujitetea. Kwani sasa hivi uko wapi,” alimwambia mkewe.

“Nimeamua kuondoka ile hotel, nimehamia nyingine kule chini kidogo,” mkewe alimjibu.
“Sasa sikiliza, sikiliza vizuri, nenda kachukue mizigo yako, halafu uende pale Kimara, kuna gereji moja bubu ipo mbele tu ya Resort Inn, muulizie mtu anaitwa Bob, jitambulishe, utapewa usafiri uje hapa tulipo,” alisema mumewe, akimsisitizia kufanya zoezi hilo haraka.

Baada ya kukata simu, askari alitoka chumbani, akaingia chumba kingine na baada ya dakika ishirini, kila kitu kikawa sawa. Gari moja nyekundu, yenye namba za kiraia ilimchukua mama Tonny na askari wengine wawili waliovalia kiraia.

Dereva aliendesha kasi hadi walipofika Kimara, katika gereji bubu iliyokuwa mbele ya Resort Inn. Mama huyo akashuka garini huku askari wa kike wakimtazama, alikwenda hadi kwa kijana mmoja na kuzungumza naye maneno machache. Kisha, mtu mmoja mwenye mwili mkakamavu akajitokeza na kwenda kuzungumza naye. Alipoanza kujitambulisha tu, akamkatiza.

“Ingia kwenye ile pale gari, kwani una mizigo zaidi ya huo mkoba? Hawa rafiki zako unaweza kuwaaga tu,” Bob akamwambia akimuonyesha gari moja nyeupe, lakini yenye vioo vya giza, aina ya Prado VX!
Mama Tonny alirejea kwenye gari alilokuja nalo, akawakonyeza askari na kuwaaga kwa kuwapa mikono, akalifuata Prado na kuingia. Gari la askari likageuza na kurejea zake mjini, wakati alilopanda mkewe mzee Linus, likaingia upande wa Morogoro, safari ikaanza!

Katika gari hilo, kulikuwa na watu wawili tu, yeye na dereva ambaye pia alikuwa mwanamke. Hakumsemesha jambo lolote hadi walipopita mizani Kibaha, tena baada ya kuwa ametoka kuwasiliana kwa simu.

“Mama nimependa tabia yako, kwa kawaida sisi kama tuko na mtu tusiyemfahamu, hatupendi awe anatumia simu yake, lakini wewe tokea tumepanda sijakuona uhangaike na simu yako,” sauti nyororo kutoka kwa mwanamke dereva ilipenya masikioni mwa dereva na kabla mkewe Linus hajajibu, simu yake ikaita.

“Ndiyo kama nimeiambia iite sasa, lol,” alisema na kusababisha wote kuangua kicheko, ilikuwa inatoka kwa mumewe.
“Mmefika wapi,” aliuliza mzee Linus, swali ambalo alijibiwa kuwa ndiyo kwanza wanatoka Kibaha, kabla ya kukata simu.

Chanzo: Globalpublishers

No comments:

 
 
Blogger Templates