Social Icons

Monday, 6 April 2015

Hadithi: Familia tata - 52

Alipiga stori hapo hadi saa kumi na moja jioni, alipomuona Maria akitoka. Mavazi yake, yalionyesha alikuwa na mtoko maalum, akapata furaha moyoni mwake. Maria alikwenda hadi kituoni na kuchukua Bajaj. Stone, akiwa amevaa kofia iliyoficha uso, naye alimfuata taratibu..
Sasa endelea...

BAJAJ aliyochukua Maria iligeuza na kuifuata njia ya Mikocheni, Stone naye akaifuata mojawapo na kuichukua. Katika mzunguko wa Kawe, Bajaj ilikata kushoto na kuifuata barabara ya Mbezi, ikaendelea hadi iliposimama nje ya hoteli moja iliyopo pembezoni mwa barabara hiyo ya zamani ya Bagamoyo.

Maria akaingia ndani ya hoteli hiyo na kwenda moja kwa moja hadi katika meza zilizokuwa zikilitazama jukwaa la muziki lililokuwa limeandaliwa siku hiyo. Vipeperushi vilivyokuwa vimefungwa kuzunguka jukwaa hilo vilionyesha kuwa siku hiyo kulikuwa na onyesho la bendi ya Kalunde Band. Ilikuwa ni bendi nzuri, iliyokuwa chini ya kinara wake, Deo Mwanambilimbi.

Baada ya kujiuliza mara mbilimbili kuhusu kama aingie ndani ya hoteli hiyo au la, hatimaye Stone, aliyekuwa ameshashuka kwenye Bajaj iliyomleta, aliamua kuingia na kuangalia wapi alikuwa amekaa. 
Kama mtu asiyekuwa na haraka, alilifuata geti la hoteli hiyo na kuingia ndani huku macho yake yakiwa makali kutazama kila upande kwa haraka, lakini kwa umakini. Kwa vile alishamuona Maria alivyovaa, ilimchukua sekunde chache tu kugundua alipokuwa amejiweka, naye bila kutazama kule alikokuwa amekaa adui yake, akaufuata upande wa pili na kukaa, katika usawa ambao angeweza kumuona vizuri msichana huyo!

Hakukuwa na watu wengi, lakini walitosha kuweza kumficha mtu aliyetaka kujificha. Mhudumu alipomfuata, akaagiza juisi na kukaa macho yake yakiwa katika jukwaa la muziki, ambako kijana mmoja alikuwa akiimba nyimbo za kunakili kutoka kwa wanamuziki wa nje. Pale, alikuwa anaimba wimbo wa hayati Bob Marley uitwao Redemption Song ambao Stone alikuwa akiupenda sana!

“Uko wapi Jimmy, nakufa leo,” Maria alimwambia mpenzi wake, mara baada ya simu aliyompigia kupokelewa upande wa pili. Muda wote tangu alipotoka nyumbani kwao, moyo wake haukuwa sawa, alijihisi mzito kana kwamba chochote kinaweza kumtokea. Hata alipofika pale akiwa katika ile Bajaj, hakuwa na amani kabisa.

“Ndiyo nachukua Bajaj hapa Makonde, kuna nini?” Jimmy alijibu upande wa pili. Ahadi yao ilikuwa ni kukutana katika ukumbi huo kwa ajili ya kufurahia wikiendi, kwani wote walikuwa ni mashabiki wakubwa wa Kalunde Band!

“Stone yupo hapa, inaonekana kabisa amenifuata, Mungu wangu, natetemeka mwili mzima,” Maria alimwambia mwenzake kwenye simu. Kauli hiyo, iliusisimua mwili wa Jimmy, ambaye alimjibu kuwa awe mpole, kwani angekuwa mitaa ile si zaidi ya dakika kumi kuanzia muda huo..!

**
“Tonsaa,” Dayani aliita kutoka ndani alikokuwa wakati akifungua mlango na kurejea sebuleni. Kijana mmoja wa kazi, aliitika na kukimbia kuja pale alipo mara moja.
“Naam mkuu,” aliitika tena baada ya kufika sebuleni.

“Kimenuka, hebu tokeni nje kuangalia hali ya hewa, tunatakiwa kuondoka eneo hili haraka sana, wanoko wako araundi,” Dayani alisema huku Tonsa akiingia chumbani kwao, sekunde chache baadaye, vijana wanne wakiwa wamevalia kama Wamasai, waliibuka. Walikuwa wamebadili muonekano wao ili waonekane kama walinzi.

Wakatoka nje baada ya kufungua geti na kulifunga, wakasambaa kila mmoja katika pembe moja ya nyumba. Uzoefu wao wa kihalifu ukawaonyesha kuwa watu wasio wa kawaida walikuwa wameizingira nyumba yao ndogo. Hata pale walipokuwa, napo palionekana kuwa na watu karibu ambao hawakuwa wa kawaida!

Wakapigiana simu na kukubaliana kuondoka eneo hilo mmoja mmoja, ili wakakutane barabarani-, lakini wakati huo huo, wakawasiliana na akina Dayani ndani kuwa kulikuwa na watu, ambao kwa vyovyote ni askari waliokuwa nje ya nyumba hiyo. Wakawataka kutoka nje mmoja mmoja haraka iwezekanavyo!

Chanzo: globalpublishers

No comments:

 
 
Blogger Templates