Wakapigiana simu na kukubaliana kuondoka eneo hilo mmoja mmoja, ili wakakutane barabara, lakini wakati huo huo, wakawasiliana na akina Dayani ndani kuwa kulikuwa na watu, ambao kwa vyovyote ni askari waliokuwa nje ya nyumba hiyo. Wakawataka kutoka mmoja mmoja haraka iwezekanavyo!
Sasa endelea...
Hakuna wakati ambao Dayani aliwahi kuwa katika hofu kama siku hiyo. Alitambua kuwa wakati wowote kuanzia muda huo angeweza kukamatwa na yeye hakuwa tayari kuwekwa chini ya ulinzi kirahisi. Akawaambia wenzake kuwa wanatakiwa kutoka haraka ndani ya nyumba hiyo, kwani tayari wamezingirwa.
Dayani alikuwa wa kwanza kutoka ndani ya nyumba hiyo baada ya kuwa amefungua geti, mavazi yake yalionyesha kama mtu ambaye anajiandaa kwenda kulala. Alipofika nje, simu yake mkononi, akawa anazungumza huku akipiga hatua taratibu kuyaacha makazi hayo. Dakika moja baadaye, wanawake wawili walitoka na kufungua geti, gari dogo jekundu likawa linataka kutoka.
Ndani ya gari hilo kulikuwa na dereva tu huku wale wanawake wawili wakionekana wazi kuwa watakuwa ni abiria.
Vijana wanne wa Kimasai walipotoka walimshtua Frank, mmoja kati ya askari kanzu waliokuwa wameweka doria katika mitaa hiyo. Katika kipindi chote tangu waanze kujikusanya hapo, hakukuonekana dalili za kuwepo walinzi. Lakini kilichomshtua zaidi, ni jinsi walivyotoka na baadaye kutoweka kwa namna ya kushangaza, ingawaje hapo mwanzo walionekana kama waliotoka mara moja.
Kitendo hicho kilimpa mashaka. Hata hivyo, hulka ya Frank siku zote ni kuzifanyia kazi hisia zake, mara moja akafanya mawasiliano na wenzake, akawaambia kuhusu wale vijana wa Kimasai na hofu yake katika nyumba ile. Askari nao wakajipanga, waliokuwa barabarani wakawa wanawafuatilia wale vijana wa Kimasai ambao walikutana katika baa moja iliyokuwa barabarani.
Macho ya askari pia yakaongezeka kwenye nyumba hiyo na hata Dayani alipotoka, askari wawili walienda naye. Kilichowashtua Polisi, ni kwamba naye alikwenda moja kwa moja na kujiunga na vijana wale wa Kimasai katika ile baa.
Baada ya kupashana habari, wakaazimia kuwakamata ili kufanya nao mahojiano. Hadi wakati huo, hawakuwa wamemtambua mtu yeyote kati ya wale waliokuwa wameketi pale baa. Wakati wakijipanga, ndipo walipoliona geti likifunguliwa na gari dogo likionekana kutaka kutoka.
“Kwa nini katika usiku huu watu nane wanatoka katika nyumba moja?” Frank alijiuliza akiwa anasogea karibu na barabara, tayari kwa kulisimamisha gari hilo.
Mzee Linus ndiye alikuwa dereva, akalirudisha gari nyuma na kulitoa kabisa. Baadaye wale wanawake wawili nao wakajipakia garini na safari ikaanza. Ni wakati akibadili gea ya kwanza tu, gari lao likamulikwa na taa kubwa za gari lililokuwa mbele yao. Zilipozima, watu wawili walishuka kwenye gari hilo na kuwapungia mkono, dalili za kuwaomba kusimama.
Wote watatu ndani ya lile gari walipatwa na hofu wakajibishana haraka haraka wakati wakijiandaa kusimama.
“Tuwalipue tusepe zetu,” msichana aliyekuwa amekaa na mkewe mzee Linus aliuliza huku akitoa bastola yake yenye uwezo wa kubeba risasi tisa.
“Hapana, ngoja kwanza tuone, yaweza isiwe hatari,” mzee Linus alisema huku akiliegesha gari pembeni. Aliposimama, aliliona gari lingine likiwasogelea, likaegeshwa nyuma yao. Watu wengine wawili wakatoka na kuwafuata pale walipokuwepo.
**
“Dereva unaweza kuongeza mwendo zaidi, maana naona kama unatambaa vile,” Jimmy alimwambia dereva wa Bajaj aliyopanda, kwani wito wa mpenzi wake ulimfanya mwili wake usisimke, alitamani kukutana na Stone haraka sana.
Dereva akaongeza mwendo uliomfurahisha Jimmy na muda mchache baadaye akawasili katika hoteli ile aliyokuwa mpenzi wake. Hakupata taabu kumuona alipo, akaenda moja kwa moja na walipokutana, wote wakasimama, wakapigana busu kama wafanyavyo watoto wa mjini!
“Niambie sweet, yuko wapi huyo mpumbavu?” Jimmy alimuuliza huku akizungusha kichwa chake kuwatazama watu waliokuwa hotelini hapo, kila mtu akiwa bize kwa shughuli zake.
Je, nini kitatokea? Usikose kufuatilia simulizi hii ya kusisimua inayoelekea ukingoni.
Chanzo: globalpublishers
No comments:
Post a Comment