Ni imani yangu kwamba wasomaji wanayo mengi sana ya kumfundisha mwandishi na mimi nimeamua kuja katika familia hii ya Raia Mwema ili nipate kufaidika na hekima za wasomaji wake. Tunaingia katika kipindi muhimu sana katika historia ya taifa letu.
Kipindi cha kampeni za Uchaguzi Mkuu ambacho kitaanza Agosti 22, 2015 ikiwa ni mbio za kukata mbuga kuelekea Oktoba 25, 2015 siku ambayo Watanzania watakata shauri kuhusu nani wanamkabidhi dhamana ya kuwaongoza kwa kipindi kingine cha miaka mitano kwa mujibu wa katiba.
Tayari vuguvugu la kampeni limeenea na joto lipo juu sana. Pande zote zinazohusika katika mchakato huu wanajifua kwa kila njia ili kuhakikisha kwamba kipenga kitapopulizwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kila mchezaji anakuwa katika nafasi yake na shughuli inaanza mara moja.
Ni kwa sababu hiyo basi ni muhimu kuanza kuangalia jinsi ambavyo tunaingia katika kipindi hicho na hususan kujaribu kuiangalia jamii yetu na matarajio yake kwa viongozi wapya akiwemo kiongozi mkuu yaani Rais.
Ni vyema kujadili kila tunaloliona kwamba ni tatizo ili kuweka ajenda ya wazi kwa yeyote yule atakayechaguliwa kuiongoza nchi hii kwa miaka mingine mitano. Katika kipindi cha ‘kutroti’ kuelekea kwenye kampeni kamili kuna kila sababu ya kusema kwamba kilichojitokeza hadi sasa ni ushabiki wa wajihi wa wagombea zaidi jambo ambalo si baya lakini halina tija sana hususan katika nchi ambayo inahitaji uongozi wa kuivusha kutoka katika umasikini na kuifikisha kwenye neema kwa kutumia rasilimali watu na maliasili zizlizopo.
Moja ya mambo ambayo yanawakera sana wapiga kura ni umasikini uliokithiri. Hili halina ubishi wala halihitaji takwimu kwani macho yanaona na huhitaji kuthibitishiwa kwamba Tanzania ni nchi yenye mamilioni ya wapiga kura na wasiokuwa wapiga kura ambao ni masikini.
Hata hivyo, jambo ambalo linajitokeza ni kama vile umasikini utatokomea mara uongozi mpya utakapoingia madarakani. Ni vizuri kuishi kwa matumaini. Lakini ni hatari kuamini kwamba kuishi kwa matumaini peke yake kunatosha kuondosha umasikini.
Umasikini ni ajenda. Na kwa hakika ni ajenda ya msingi sana ambayo hakuna awezaye kuibeza na sitaki kuamini kwamba kuna mtu mwenye akili zake timamu ambaye atasema kwamba anaupenda umasikini. Lakini kuuchukia umasikini ni hatua ya kwanza tu.
Kinachojitokeza hivi sasa ni kwamba suala la chanzo cha umasikini huo kinaoneshwa kama vile kimetokana na chama tawala na kwamba kama chama hicho kikiondolewa madarakani basi bila shaka atakayeingia ataumaliza umasikini. Hiyo ni kaulimbiu nzuri kwa kampeni bila shaka.
Lakini ni kaulimbiu ambayo inatakiwa kuangaliwa kwa tahadhari sana ili kutokujenga hisia potofu na pofu kwamba umasikini unaweza kutokomezwa kwa kufanya mabadiliko ya chama ama mtu.
Ni vyema suala la umasikini likatazamwa kama jambo mtambuka ambalo si sahihi hata kidogo kuliangalia kutoka upande wa chama na mtu aliyekalia kiti cha urais, kwani kwa kufanya hivyo ni sawa kabisa na kukabidhi nguvu za uumbaji kwa asasi hizo. Umasikini una uhusiano mkubwa sana na falsafa ya kazi na jinsi jamii inavyochukulia suala la kazi na uzalishaji mali kwa ujumla wake.
Wanasiasa wanatuambia kwamba umasikini wetu unatokana na kutokuwa na ajira (hususan kwa vijana).
Ni jambo linalohitaji kujadiliwa kwa mapana kwani kusema kwamba vijana hawana ajira na kuonesha kidole kwa serikali kwamba haitoi ajira kwa vijana ni jambo linalohitaji kutolewa maelezo ya ziada. Kwa sababu serikali haizalishi mali kwa namna ambavyo viwanda na kilimo hufanya.
Serikali inajenga mazingira kwa ajili ya kusaidia uanzishwaji wa viwanda na uzalishaji wa mashambani na si shughuli yake kuanzisha viwanda na kulima mashamba.
Ikumbukwe ajira rasmi zipo katika viwanda, mashamba, hoteli, migahawa na kampuni nyingine za huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na utafiti na maendeleo ya sekta mbalimbali.
Serikali inatakiwa kuweka mazingira kwa ajili ya kufanikisha uwekezaji katika sekta mbalimbali kwa ajili ya kukuza uchumi, jambo ambalo bila shaka litaongeza nafasi za ajira rasmi na zisizokuwa rasmi.
Lakini swali la msingi hapa ni kwamba tunapolalamika kwamba ajira hakuna tunamaanisha kwamba hakuna shughuli za uzalishaji mali au utoaji wa huduma zinazoweza kufanywa nje ya mkondo wa serikali au ni kwamba serikali haitaki kuwaajiri watu kwenda kuifanyia kazi?
Serikali yoyote ile duniani inao ukomo wa kuajiri. Ukomo huo unatokana na sababu kubwa ambayo nimekwishakuigusia hapo juu, kwamba serikali haifanyi shughuli za kuzalisha mali bali hujishughulisha na uwekaji wa mazingira chanya kwa ajili ya uzalishaji mali na utoaji huduma.
Kuitaka serikali iajiri bila ukomo ni kuipanua mno na matokeo yake ni kuwa na bajeti kubwa ambayo inabidi kuigharimia kwa kutumia kodi ambazo nazo zina ukomo wa utozaji wake.
Ipo dhana inayojengeka kwa sababu ama ya uelewa mdogo au makusudi kwa ajili ya kufanikisha malengo ya kisiasa ya muda mfupi. Dhana hiyo ni ile inayolenga katika kuuaminisha umma kwamba serikali inao uwezo wa kuajiri bila ukomo.
Katika muktadha huo basi ni muhimu kujiuliza swali la msingi kwamba kama kielelezo kikuu cha kwamba sisi ni masikini ni kutokuwa na ajira je, ajira ni nini?
Kama jamii tukiweza kukubaliana katika tafsiri ya ajira ni nini basi tunaweza kufika mahali tukakubaliana nini cha kuiambia serikali itakayoingia madarakani hap utakapokamilika uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka huu kuhusu umasikini na jinsi ya kupambana nao. Wiki ijayo nitajadili dhana ya ajira na kuangalia nani anatakiwa kumuajiri nani katika jamii, malipo kama mshahara au ujira na nafasi ya kila mtu nkatika soko la ajira. Mwandishi wa makala haya,
Dk. Gideon Shoo anapatikana kwa simu namba 0784222293.
Chanzo. Raia mwema
No comments:
Post a Comment