WANASIASA, wachambuzi, waandishi wa habari na hata wananchi wa kawaida wanasema uchaguzi wa mwaka huu utakuwa ni wa kihistoria kwa sababu ya mwamko mkubwa wa wananchi na sio siri kuwa mwamko uliopo sasa unatokana na hamasa ya wananchi kutaka mabadiliko.
Inavyoonekana ni kuwa watanzania wengi, kwa muda mrefu wamekuwa wakitaka mabadiliko ya utawala. Hata hivyo, huko nyuma, kutokana na udhaifu wa vyama, udhaifu wa wagombea na fikra kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) kina mbinu za faulo za ushindi, watanzania waliona kupigia kura upinzani ni kazi bure.
Mwaka huu hali ni tofauti
Mwaka huu, kuna kila sababu ya kuamini kuwa mabadiliko yanawezekana. Kwanza kuna umoja wa vyama vya upinzani, uendao kwa jina la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa). Pili, kutoka kwa Edward Lowassa katika chama tawala na kuingia Chadema, na kisha kuteuliwa kuwa mgombea atakayewakilisha Ukawa kumeongeza imani zaidi ya wananchi kuwa mabadiliko yanawezekana.
Kuingia kwa Lowassa Ukawa kumeipunguza nguvu CCM na nguvu hiyo kuhamia Ukawa. Pamoja na Lowassa, wanachama wengi wa CCM wamemfuata, wadogo na wakubwa ambao wamerudisha na kuchoma kadi za CCM hadharani, wakakilaani chama hicho na kujiunga na vyama vya Ukawa katika kile kinachoitwa mafuriko au gharika. Wanufaika wakubwa wa mhamo huo wamekuwa Chadema.
Kuingia kwa Lowassa Ukawa pia kumefanya sasa watu waamini wamepata mtu anayezijua mbinu za ushindi za CCM na hivyo atahamishia mbinu hizo Ukawa. Kama ni rafu, na yeye anazijua. Nasikia profesa mmoja alimzungumzia Lowassa kwa kutumia mfano wa jambazi aliyewatoroka wenzake na kuja kuvujisha siri za uovu na kujiunga na raia wema!
Kule mtaani kwetu, vijiweni utasikia watu wakimsifia Lowassa kuwa ana watu kwenye kila taasisi nyeti ya nchi hii - ikiwemo usalama wa taifa, jeshi la wananchi, jeshi la polisi - na hivyo ataweza kunyaka siri za hujuma za CCM dhidi ya Ukawa. Hata nimewahi kusikia eti Lowassa aliwaambia wafuasi wake huko Ukawa kuwa wao wapige kura tu, kazi ya kulinda kura na kushughulika na tume wamwachie yeye. Lowassa amewapa Watanzania wengi hali ya kujiamini.
Hamasa yote hii ya kutaka mabadiliko inathibitishwa na maelfu ya watu wanaojitokeza katika mikutano ya Ukawa - Lowassa katika miji mikubwa ya Mbeya, Mwanza, Dar es Salaam na Arusha. Huku mitaani kila mtu anaimba mabadiliko hadi wachambuzi wanajiuliza CCM watapona mwaka huu?
Binafsi, nimekuwa mgumu kuamini kuwa vuguvugu la Lowassa hili lina mashiko na nafasi ya kufanikiwa. Lakini kila nikiangalia huku mtaani ninapoishi naona CCM wana hali mbaya. Pale saluni ninaponyoa, kila ninapokwenda sioni vijana wanaoshabikia CCM. Kila mtu yupo timu Ukawa.
Jirani yetu pale Magomeni, mama muuza vitumbua, ambaye kiasili ni CCM naye anasema atampigia kura Lowassa. kisa? Kaka yake ambaye ni mfanyabiashara ndogo ndogo amekuwa akikamatwa kamatwa hovyo pale Kariakoo na kisha kunyang’anywa mali zake na migambo ya Jiji. “CCM wanatunyanyasa wanataka sisi wanyonge tukale wapi?”, mama muuza vitumbua alinambia.
Juzi nilikuwa nazungumza na mmoja kati ya wazee wangu waliopo kule wilayani kwangu, Tunduru, bibi wa miaka zaidi 70 naye ananishauri mimi ninayeishi hapa Dar es Salaam nimpigie kura Lowassa! Du! Kama homa, basi joto la siasa za mabadiliko Tanzania limepanda hadi nyuzi 100. Siasa za mabadiliko zinachemka.
Lakini kw kweli, ni mtu mjinga pekee ambaye hahitaji mabadiliko. Hata hivyo, mabadiliko yapo tunayoyaita chanya na mengine hasi. Kutokana na vuguvugu la Ukawa na Lowassa, Watanzania wanategemea mabadiliko chanya.
Hata hivyo, uchambuzi wangu usio wa kisomi sana na maono yangu mafupi yananiambia Watanzania wameweka imani ya upofu kwa vuguvugu hili la mabadiliko, na nachelea tusije tukapata mabadiliko hasi.
Uzoefu unaonesha mabadiliko hasi yamewahi kutokea duniani katika nchi ambazo raia wengi waliweka imani katika vuguvugu kama hili la Ukawa na baadaye watu wakajuta. Nisingekuwa na sababu ya kutia shaka kuwa hilo linaweza kutokea kama nisingekuwa na sababu kadhaa za msingi ambazo mimi sio wa kwanza kuzizungumza.
Kwanza, inaonekana Ukawa wenyewe na wafuasi wao wanaongozwa zaidi na hamu ya kuiondoa CCM kuliko ajenda maalumu za mabadiliko baada ya kuitoa CCM madarakani. Ukizungumza na wananchi, unaona hisia za ‘sina cha kupoteza’, ‘liwalo na liwe’, ‘wamekaa sana madarakani hawa washenzi CCM’.
Ni hisia za watu wanaoonekana wamekata tamaa. Ni jambo zuri lakini pia ni baya. Ni zuri kwa sababu mtazamo huo ni mzuri kwa kuleta mabadiliko, lakini ni mbaya kwa sababu watu hawatumii muda kuzingatia mabadiliko yanayokuja ni ya aina gani.
Wakati fulani ukiwasikiliza baadhi ya viongozi wa Ukawa unaweza kudhani kuwa lengo pekee la vuguvugu hili ni kuiondoa CCM madarakani na kuitia adabu ikiwezekana kuifuta kabisa katika uso wa dunia, kana kwamba ukifanya hivyo matatizo yote ya Watanzania yatakuwa yamekwisha!
Sababu ya pili: ya kutilia shaka uwezekano wa kutokea mabadiliko chanya ni ‘mchanyato’ wa hatari (dangerous, even poisonous mix) uliotengeneza Ukawa. Kuna vyama walau viwili, Chadema na CUF, ambavyo najua vina falsafa na mitazamo tofauti sana lakini pia kuna ongezeko kubwa la wanachama kutoka CCM, ambao hao huhitaji shahada ya saikolojia kujua kuwa wanaongozwa na maslahi binafsi na uroho na tamaa ya madaraka. Hawa nazungumzia wote ambao walitoka CCM baada ya kushindwa kura za maoni, wakadai kuna rushwa nyingi – kumbe tofauti yao na walioshinda ni kuwa walioshinda walitoa rushwa zaidi.
Tatu, nina wasiwasi mkubwa kuwa watu walioingia sasa hivi ndani ya Chadema (Chadema maslahi binafsi/ fuata upepo) wanaweza kabisa kuwazidi nguvu Chadema asilia – na hata kuigeuza kuwa kopi mbaya ya CCM, kama ambavyo Profesa Ibrahim Lipumba alivyodai. Huhitaji kuwa mtaalamu sana wa siasa kujua kuwa uadilifu, uaminifu na uzalendo wa baadhi ya watu wanaotoka CCM na kuhamia Ukawa unatia shaka
Nne, Lowassa na wahamiaji wenzake hawafanani na mambo ambayo Chadema wamekuwa wakiyasimamia. Mpaka anahamia Ukawa, Lowassa amekuwa muumini wa serikali mbili, muungaji mkono wa Katiba Inayopendekezwa na falsafa za sera, itikadi na falsafa za CCM.
Leo, Lowassa na wenzake wanavua falsafa hizo kama mtu anavyovua nguo – kirahisi rahisi tu. Binafsi, ningemuelewa Lowassa na wenzake waliotoka CCM, kama angeunda chama chake au angeingia katika vyama vidogo ambavyo havijajijenga kiitikadi na kukibadilisha kiwe CCM – mbadala.
Mwisho, nimalizie kwa kusema kuwa wakati Watanzania wengi tunataka mabadiliko, tunahitaji pia kufikiria vema kuhusu vuguvugu au wimbi hili kubwa linalokuja. Ni kweli ni wimbi la mabadiliko, lakini je ni wimbi la mabadiliko mazuri tunayoyahitaji au tunaenda kucheza kamari mbaya.
Najua baadhi ya jamaa zangu watanishambulia sana na kuniita mnazi wa chama tawala lakini tahadhari kama hizi, ambazo mimi sio wa kwanza kuzitoa, si za kupuuzwa hata kidogo na pande zote, wananchI na hata Ukawa. Wasiwasi huu unaoibuliwa uwape wananchi uelewa wa maswali ya kujiuliza na kujiridhisha kabla ya kukumbatia ama kuzuia mabadiliko.
Kwa Ukawa, haya tunayoyaandika na kusemwa na wachambuzi dhidi yao yawe changamoto kwao ya kuboresha ushirikiano wao ili ulete tija. Ukawa baada ya kuing’oa CCM idhibiti mabadiliko.
Chanzo. Raia mwema

No comments:
Post a Comment