Social Icons

Friday, 14 August 2015

Ni rahisi zaidi kuwadanganya watu kuliko kuwaelimisha kwamba wamedanganywa

Sijui siku zinaenda wapi. Yaani karibu mwezi mwingine umepita na natamani upate nafasi nyingine ya kuja Dar angalau mara moja mpenzi. Haitoshi kuulizia hali yako. Nataka nikuone, nijihakikishie kwamba kweli mpenzi wangu hajambo, yuko salama, afya tele na mapenzi zaidi. Ndiyo maana nisipokuona kila mwezi sina raha kabisa mpenzi.

Hata mimi nilitegemea kuomba likizo ya angalau siku tatu nije niwasalimie wote lakini wapi! Nilifikiri kwamba labda mambo yatatulia kwa kuwa waheshimiwa wamepumzisha sponji zao za mjengoni na maisha yanakuwa ya kawaida, kumbe wapi! Sasa viherehere vya uchaguzi vyatawala na kila siku wageni wanajaa maana naona huu ni wakati maalum wa kutongoza kwa nguvu.

Wanakuja washenga na hata waposaji wenyewe kila mmoja akijaribu kumshawishi Bosi kwa hali na mali na Bosi anakaa pale huku akipokea zawadi za watongozaji na kuchekacheka kama vile mwali.

Baada ya mifarakano yao, Binti Bosi anakaa mbali kabisa asije akachukizwa zaidi lakini watongozaji hawakwepeki. Hata usiku wa manane, nasikia simu ya Bosi ikilia kisha anaamka kumpokea mgeni huyu au yule. Mara mbili nimeamshwa na mimi ili nitengeneze nyama choma kwa ajili ya watongozaji wenyewe badala ya washenga wao. Na bahasha zinazotolewa! Sitashangaa nikisikia kwamba kumekuwa na uhaba wa bahasha nchini.

Mara nyingine najiuliza kama sisi ndio wehu. Nakumbuka msemo wa mwalimu wetu, eti iwapo wote ni wehu, wenye akili timamu ndio watakaoonekana wehu. Labda tunapaswa kugeuza dunia chini juu tuhalalishe yaliyo haramu na kudhalilisha yaliyo halali. Juzi kaja shangazi yangu. Akasema basi lilisimama mara tatu njiani na kila mara konda akatoka huku akihesabu pesa waziwazi na kuelekea huko nyuma alipokuwa anasubiri linene la barabara. Wote wanajua jambo gani linatendeka, lakini konda hasemi neno, abiria hawasemi neno. Hivi abiria wote wangeamua kutelemka na kumsindikiza konda kwa linene lile, kungetokea nini? Na kama hawafanyi hivyo, si tumehalalisha yaliyo haramu, na kwa hiyo anayekataa hongo kama hizi ndiye haramu mwenyewe. Eti hataki maendeleo.

Haya na kwenye siasa vivyohivyo. Nani hajui kwamba watu wanatoa hongo za kila aina? Tena ndani ya chama hichohicho! Lakini ukiacha malumbano ya makambi, nani anasema? Nani analaani mfumo badala ya kumlaumu tu mtu wa kambi nyingine? Hadi watu wanashikiana mabastola, kuna mtu anafukuzwa hapa? Lakini wakija kwetu tunawapigia makofi, tunawapigia vigelegele badala ya kuwakataa katakata. Kweli sielewi mpenzi. Ama kweli bora kuwa asiyeona kwa macho kuliko kuwa asiyeona kwa akili.

Na bado! Nadhani kuna kundi bovu zaidi tena. Kweli mpenzi. Aheri aheri wanasiasa kuliko wanadini. Shangazi alikuja kwa sababu bado anapigania kurudishiwa shamba lake alilopokonywa na kiongozi wa dini eti mwekezaji wa ndani. Badala ya kuwekeza mbinguni kama inavyoagizwa na msahafu, anataka kuwekeza katika unyang’anyi. Ukiongea na shangazi, utajaa hasira iliyochanganyikana na huzuni.

Utanisamehe lakini ilibidi nimgawie pesa kidogo maana hata khanga yake moja iliyobaki kidogo isambaratike moja kwa moja. Bado anakaa katika kibanda kidogo huku anashuhudia jinsi yule mwanadini anavyojineemesha juu ya upokonyaji mtakatifu. Na shangazi akithubutu hata kusogelea shamba takatifu anatishiwa na bunduki takatifu bila kusahau maji matakatifu yaliyojaa sumu za kila aina zinazotokana na mbolea na dawa za vidudu anazotumia mtakatifu huyu.

Lakini pamoja ya mateso hayo, shangazi ni mtu, mpenzi. Hakubali kushindwa kwa hiyo yeye na wenzie wamekuja kushinikiza huko kwa wanene warudishiwe haki zao. Na kama kawaida, hata kusikilizwa tu, hata kupewa fursa ya kukutana na wahusika, lazima watoe pesa tena. Inaonekana sala zake haziwezi kushindana na sala za bahasha. Baada ya kukumbwa na haya tena, shangazi alicheka kwa uchungu sana.

“Nawashukuru hawa wanaharamu walionipokonya ardhi maana wamenipatia tiketi ya kuingia mbinguni moja kwa moja. Si unaambiwa unatakiwa kuvua utajiri wako ili uweze kupitia mlango mwembamba sana? Nimeshavuliwa, kwa hiyo mimi nitapita bila shida, na nikifika upande wa pili nitafurahi kukaa na kumwangalia huyu mnene atakavyokwama. Kabisa!”

Ndipo hapo nawashangaa tena na tena watu. Nilimdokezea Binti Bosi kidogo, akacheka na kunitolea maneno ya mwandishi fulani wanaowasoma huko shuleni. Eti, ni rahisi zaidi kuwadanganya watu kuliko kuwafanya waelewe kwamba wamedanganywa. Yaani sisi tumekuwa wadanganyiiiika lakini mtu akijaribu kutuonyesha tunavyodanganyika kila siku, tunamwona mjinga, kama si fedhuli.

Hawa manabii wanashindana kwa utajiri bila hata aibu, wanatambiana na mali zao za kuwazuia wasipite kwenye njia nyembamba, wanageuza msahafu chini juu ili kutetea utajiri wao na utajiri wa wafuasi wao wateule, lakini sisi tusio na kitu tunaendelea kujifukarisha ili mnene anone zaidi na zaidi. Tena bila kulalamika. Tena tunatoa huku tukiimba kwa furaha. Tena mtu akithubutu kujaribu kutufunulia macho, tunamkasirikia mno.

Kwa kweli shangazi ndiye shahidi. Baada ya kugonga mwamba wa mibahasha, yeye na wenzie waliamua kwenda kwenye hekalu ya wanono wa dini. Walikuwa wamepewa msaada ya kuchapa maelezo yao ili kuwagawia waumini ili waumini waone mwanga wa jua, mwanga wa kweli badala ya mwanga feki. Si tu walifukuzwa kama mbwa na walinzi wa mali ya wenyewe, waumini wote wale walikuwa wanashangilia jinsi walivyofukuzwa. Wengine walitaka kuwarushia mawe!

Kwa hiyo, nimeona kwamba hata wanasiasa wengine wamekosea. Utajiri uko kwenye dini, hakuna biashara nzuri kama dini na kwa kuwa ni rahisi zaidi kuwanganya watu kuliko kuwadanganyua, wale wataendelea kunona bila taabu yoyote. BB na mimi tulitengeneza orodha kidogo eti na sisi tuanzishe dini yetu.

Kwanza inabidi kuwaahidi waumini kwamba wakikufuata kwelikweli watapata kila wanachokitaka. BB alinisimulia kuhusu kanisa moja huko kwao kwamba watu waliambiwa waje na funguo za gari zibarikiwe na watapata gari. Hata kama una ufunguo wa kibubu tu, ili mradi uutingishe wakati baraka zinatolewa, gari litakuwa lako. Wangapi walipata gari? Lakini wasiopata bado wanaambiwa ni kwa sababu hawajawa na imani ya kutosha, au madhambi yao yamezidi, ili mradi mtu asitambue kwamba ahadi yenyewe ndiyo dhambi.

Siku yoyote ukiona waumini wako hatarini kuamka, waonyeshe adui mwingine waelekeze hasira zao zote huko. Ingawa sipendi kabisa kuwaona hawa viongozi wengi wa dini, sipendi pia kukashifu misingi ya dini ya mtu mwingine. Dini ni msingi wa maisha yetu licha ya mchwa wanaojaribu kutafuna msingi. Lakini ninashangaa pia watu wanavyoweza kuhemka kuhusu kitu ambacho hawajakiona wakati kuna mambo kibao mbele yao ambayo ni kufuru kwa mtu yeyote mwumini.

Tungetumia misingi yetu ya dini kupambana na ufisadi, na kuwang’oa wanaotenda madhambi makubwa sana ya kuharibu maisha ya watu wengine kwa kujitafutia utajiri juu ya migongo iliyopinda kwa kuwanyang’anya hadi tonge la mwisho, naamini hapo dunia itabadilika.

Basi Bwana, shangazi bado yuko na itabidi nimtafutie nauli aweze kurudi nyumbani maana hapa hamna kitu. Watakatifu matajiri oyee!! Sisi maskini tuendelee na umaskini wa mawazo pia ili watukufu waendelee kukufuru.


Chanzo: Raia mwema

No comments:

 
 
Blogger Templates