Social Icons

Friday, 14 August 2015

Wanawafuata viongozi wao


NIMEJITAHIDI kueleza ni jinsi gani tunazalisha wakimbizi wa kiuchumi wanaokimbia maisha “yasiyoishika’ ya shamba na kuingia mijini kwa kasi kubwa, na jinsi ambavyo huko mjini waendako wanakuwa ni chanzo cha matatizo kadhaa yanayotokana na ukweli kwamba hawana maandalizi yo yote ya kuwafanya waweze kuishi mjini kwa maslahi yao wenyewe, mijini wanakokwenda na nchi yao kwa ujumla.

Ukimuuliza ‘mkimbizi’ wa aina hii kama alipenda mwenyewe kuachana na maisha ya kijijini na kuhamia mjini, bila shaka atajibu kwamba ulikuwa uamuzi wake binafsi, lakini harakati za watu wa aina hii huamuliwa na nguvu ambazo wao wenyewe hawawezi kuzieleza isipokuwa tu kusema kwamba maisha ya kijijini ni magumu.

Msingi wa hali hii ni mahusiano tenge baina ya walio-nacho na wasio-nacho, baina ya maisha ya mjini na maisha ya shamba, baina ya maisha ya Uropa na Marekani na masha ya dunia ya tatu, baina ya kuwa na matumaini na kukata tamaa.

Kadri tunavyoshuhudia wakulima wakikimbia shamba na kuingia mijini ndivyo tunavyoshuhudia pia vijana wa dunia ya tatu wakizikimbia nchi zao kwenda Uropa na Marekani. Haishangazi, kwani Uropa na Marekani ndiyo miji na nchi zetu, pamoja na miji yake mikuu, ndivyo vijiji vya dunia. Kimantiki, hata hao vijana wanaotoka nyuma ya Kamachumu na kuingia Dar es Salaam kwa mkupuo mmoja, wako ‘transit’ wakielekea ‘majuu’.

Sasa, hali hii ingeweza kurekebishwa kama zingekuwapo dalili kwamba, labda, hii ni hali ya mpito na muda si mrefu mambo yatakaa sawa kwa sababu ‘wahusika’ wanahangaika kutafuta namna ya kuondokana na hali hii isiyofaa. Lakini wanaona nini?

Kila uchao kinachodhihirika ni kwamba hao ambao wangetakiwa warekebishe hali ya maisha vijijini, wenyewe tayari walikwisha kukimbia kitambo. Lingekuwa jambo la kutarajiwa kwamba wawakilishi wa wananchi, hususan wabunge, wangeishi kijijini wakisaidiana na wananchi kuelewa mazingira yao na kuchukua hatua za kuyabadilisha, lakini wabunge hao hao ndio wa kwanza kuachana na maisha ya kijijini.

Wengi wa wabunge wetu, ambao asilimia 80 wanawakilisha majimbo ya shamba, wanaishi mjini. Yako makundi mawili ya wabunge hawa: kwanza wako wale walioishi mjini miaka 30 au zaidi wakiwa watumishi katika asasi fulani, na baada ya kustaafu wakaenda shamba kuwahadaa wananchi kwamba “watawaletea maendeleo”.

Pili, ni wale waliokuwa wakiishi shamba muda wote huo wakiwa ni walimu, makarani au wakulima, na baada ya kupata ubunge wakahamia Dar es Salaam.

Sababu moja ya aina zote mbili za wabunge kupenda kuishi Dar es Salaam ni kwamba, kama ilivyo kwa wale wakulima wanaokimbia maisha ya shamba, maisha ya vijijini si maisha na mjini ndiko yaliko maisha. Wanafuata vile vitu ambavyo tunavihusisha na maendeleo, kama maji, umeme, barabara za lami, maduka, sehemu za starehe, msongamano wa magari barabarani, kelele za ‘promosheni,’ na kadhalika.

Sababu nyingine ni kwamba jijini Dar es Salaam ndiko wanakoishi watawala wakuu wa nchi, na wao ndio wenye maamuzi juu ya kila kitu kinachohitajika kwa ajili ya maendeleo ya nchi nzima. Kukutana na kuzoeana na watawala hawa ni hatua muhimu katika jitihada za mbunge ye yote “kupeleka maendeleo” kwa watu wake.

Kwa maana hiyo, mbunge ye yote anayetaka kuonekana kama anawafanyia watu wake jambo la tija hana budi kuwa na maskani jijini Dar es Salaam. Najua kwamba hakuna mbunge anayeweza kuwapelekea maendeleo watu wake. Aidha najua kwamba wapo wabunge wanaoishi na wananchi wao huko vijijini, na watu wao wanawakubali kama watu wanaochangia kuleta maendeleo jimboni.

Hata hivyo, katika zama zetu hizi za hadaa, muonekano ndio ukweli, na wanaofanya mambo yanayoendana na mantiki na wakaruhusiwa kuendelea kuwapo katika nafasi zao ni wachache. Rahisi imekuwa ndiyo sarafu, miigizo imechukua nafasi ya halisi na bazazi sasa ni imam!

Kwa walio wengi kuishi Dar es Salaam muda mwingi zaidi kuliko kuishi kijijini ni dalili ya mafanikio. Hakuna fahari katika ‘kuufuma’ ubunge halafu ukabakia kijijini ‘unasota’ na wapiga kura wako, ambao wanaamini kwamba kura zao zilitakiwa zikufanye uwe ‘umeukata.’ Unatakiwa uwe mjini ili uweze kuwasiliana vilivyo na ‘wakubwa’ na kwa kufanya hivyo uweze ‘kupeleka maendeleo’ kwa watu wako.

Hali halisi tunayoishi nayo kwa hivi sasa inaweza ikaelezwa kifupi kama ifuatavyo: watawala wakuu wako Dar es Salaam, na wao ndio wenye maamuzi kuhusu kila kitu kinachohusu maisha ya wananchi wa Tanzania ko kote waliko; wawakilishi wa wananchi wameing’amua hali hiyo, na wao wamehamia jijini ili wawe karibu na wakubwa ili waweze kubembeleza “miradi ya maendeleo” iende katika majimbo yao; wananchi nao wameibaini hali hiyo, na wao pia wanafuata wawakilishi wao huko huko Dar es Salaam ambako, hata kama hawatapata maendeleo, angalau watashuhudia “maajabu ya maendeleo’” kama vile msongamano wa magari.

Kwa mtindo huu, vijiji  vyetu vitaendelea kupoteza watu, hasa vijana wenye uwezo wa kufanya kazi za kilimo na nyingine, na miji yetu itazidi kufurika, ikijazwa na wakulima ambao hawana shughuli yo yote ya maana mjini isipokuwa kwamba wanakimbia ngwamba na maisha yasiyovumilika sehemu za shamba.

Kama nilivyoandika mapema, hii si hali inayotusibu sisi peke yetu kama Watanzania au Waafrika; ni hali ya jumla katika nchi za dunia ya tatu, nchi zilizokwama kimaendeleo mabara ya Afrika, Asia na Amerika Kusini. Hata hivyo, hatuwezi kuiruhusu hali hii iendelee kukomaa kwa kutokuchukua hatua madhubuti, kwani madhara yake yatakuja kuwa makubwa, na kama hayakutukuta yatawakuta wanetu na wana wao.

Hatua zinazohitajika kuchukuliwa ni za aina nyingi. Kwa hakika, kama ilivyo katika kutafuta ufumbuzi wa matatizo mengi, hakuna aina moja ya hatua inayofaa, bali ni mchanganyiko wa hatua, ‘matriki’ mwafaka inayounganisha juhudi na tafakuri katika medani mbali mbali.

Mojawapo ya hatua zinazopasa kuchukuliwa katika matriki hiyo ni kuangalia upya mipangilio ya utawala wetu na jinsi inavyoathiri maisha na maendeleo ya watu wetu, hususan jinsi ambavyo utawala wetu na mifumo yake vinavyoathiri uwezo wa wananchi wetu kujifanyia maamuzi yanayolenga kuleta maendeleo.

Katika kuyajadili masuala haya nitaanzia msingi wa hoja (premise) unaokiri kimsingi kwamba kuna hitilafu katika mifumo yetu ya utawala, na kwamba hitilafu hizi hazikuzuka hivi hivi tu, bali zina historia yake, na tukiielewa historia hiyo tutakuwa tunajiweka katika nafasi nzuri ya kuchukua hatua zinazopasa.

Aidha, katika zoezi hili ninaongozwa na ile dhana ambayo kila mara napenda kuirejea: kila kilichopo kiliundwa na kuwekwa, na kinaweza kubadilika ama kubadiliswa kama kitaonekana hakina manufaa tena.


Chanzo: Raiamwema

No comments:

 
 
Blogger Templates