Social Icons

Sunday, 30 August 2015

Siri ya vurugu CHADEMA Mbeya

FILAMU ya wanaokatwa kwenye vyama vyao kuhamia vyama vingine iliendelea mkoani Mbeya juma lililopita, na iliyotikisa zaidi ni ile ya Mbunge aliyemaliza muda wake, Jimbo la Mbarali, Modestus Kilufi. 
Agosti 14, mwaka huu, katika Viwanja vya Shule ya Msingi Luanda Nzovwe, Mbunge huyo alitambulishwa rasmi kuhamia Chadema na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, katika mkutano wao wa kihistoria mkoani hapa, ikiwa ni baada ya kukatwa CCM. 

Lakini siku nane baadaye alihamia ACT-Wazalendo baada ya huko nako kukatwa. Kama ilivyokuwa kwa viongozi wengine wa CCM waliokimbilia Chadema baada ya kukatwa, Kilufi alikishutumu chama chake hicho cha zamani na kukilinganisha na kila aina ya uchafu, kama vile ufisadi, wizi, unafiki na ukiukaji wa misingi ya demokrasia, lakini siku nane baadaye huko alikokimbilia nako akakatwa. 

Mbunge huyo aliyefanikiwa kuingia bungeni kupitia turufu ya migogoro ya ardhi wilayani Mbarali, alitarajia kurudi tena bungeni kupitia Chadema baada ya kukatwa CCM, na imani yake hiyo ilipata nguvu zaidi pale alipokubaliwa na uongozi wa chama hicho ngazi ya Mkoa wa Mbeya na taifa. “

Wilaya walinikataa kabisa, Chadema taifa na mkoa walinikubali vizuri sana, lakini wilaya walinikataa,” anasema Kilufi, katika mahojiano yake ya simu na gazeti hili, akithibitisha kukatawaliwa kwake na wanachama wa Chadema wilayani Mbarali. 

Hata hivyo, baada ya kukatwa nako Chadema, mwanasiasa huyo alikimbilia ACT-Wazalendo Ijumaa iliyopita ambapo alichukua fomu ya nafasi ya ubunge kwa Jimbo hilo hilo la Mbarali na kuzirudisha siku hiyo hiyo, ikiwa ni saa chache tu tangu akatwe Chadema, na alithibitisha hatua yake hiyo akisema; “Chadema tulikwama, nimechukua ACT-Wazalendo, sasa hivi ni sherehe tu, natoka kurudisha fomu.” 

Taarifa kutoka jimboni humo zinabainisha kuwa, vyama vya Chadema na CUF, vyote vikiwa sehemu ya Ukawa, vimeweka wagombea ubunge katika jimbo hilo kinyume cha makubaliano ya umoja huo kuachiana majimbo. 

Kwa mujibu wa makubaliano ya umoja huo, Jimbo la Mbarali lilikuwa kimeachiwa Chama cha Wananchi (CUF), lakini kwa mshangao wa wengi, Chadema nao wamesimamisha mgombea. 

Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mbeya, Joseph China anathibitisha kuwepo kwa mkanganyiko huo akidai umetokana na CUF kuweka mgombea wanayetilia shaka uwezo wake kushinda katika Uchaguzi Mkuu ujao. 

“Kupitia makubaliano ya Ukawa Jimbo la Mbarali lilienda CUF, lakini mgombea wake hana nguvu, ana uhusiano na mgombea wa CCM, kwa hiyo iliamuliwa apitishwe aliyeongoza Chadema,” alisema China katika mahojiano maalumu na gazeti hili kwa njia ya simu. 

Hata hivyo, kwa upande mwingine, maelezo ya mwenyekiti huyo kuhusu Kilufi, yanatofautiana na yale ya mgombea mwenyewe, ambapo wakati mgombea huyo akithibitisha kukataliwa Chadema Wilaya ya Mbarali, China alidai ni mkanganyiko uliosababishwa na viongozi kuwa katika shughuli za nje, hivyo kutofanyika kwa kikao cha ndani alichoitisha kujadili suala la chama chao kumsimamisha Kilufi katika nafasi ya ubunge. 

“Tafsiri ya watu ni viongozi walikimbia na fomu, lakini ni kwamba barua ya kutengua uteuzi wa mgombea aliyeongoza katika mchakato wa kura za maoni ilipokuja, tayari alikuwa ameishachukua na kurudisha fomu,” anasema China. 

Inaaminika kwamba hamahama ya Kilufi itaiathiri zaidi Chadema katika Jimbo hilo, baada ya mwanasiasa huyo kuhama na wapenzi wake alioingia nao takribani siku nane tu kabla ya kukimbilia ACT-Wazalendo. Mwenyekiti wa APPT Maendeleo Mkoa wa Mbeya, Godfrey Mwandulusya anaiangalia hali hiyo tata ndani ya vyama vinavyounda Ukawa kwa jicho la mbali zaidi, akisema ni umoja uliotokana na uamuzi wa wakubwa kugawana makubwa, na kwamba hawakujali ushiriki wa wanachama wao. 

“Kama kuna ushirikiano, yuko wapi Dk. Slaa (aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema), yuko wapi Profesa Lipumba (aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF), kuna siri gani hapo hawataki kuweka hadharani, wana siri kubwa wale,” anasema Mwandulusya alipohojiwa na gazeti hili. 

Suala la kuhama linaelezwa na wadau wa siasa za Mbeya kutokuwa na afya kwa siasa za mkoa huo na nchi kwa ujumla, wanabainisha kuwa ni hatua inayothibitisha jinsi ambavyo wanasiasa hao wanavyosukumwa na maslahi yao binafsi na sio ya jamii kama wanavyodai kwenye majukwa ya siasa.

 “Mtu anahama chama leo, anajiunga na chama kingine siku hiyo hiyo na kupewa nafasi ya kugombea, hajui hata katiba ya chama chenyewe, huyu anasukumwa na maslahi binafsi,” anasema Mwenyekiti huyo wa APPT Maendeleo. 

Pamoja na Jimbo la Mbarali, hali pia sio shwari kwa chama hicho kwenye Jimbo la Lupa wilayani Chunya ambako mgombea aliyeongoza kwenye mchakato wa kura za maoni ndani ya Chadema, Mohamed Miraji, kaenguliwa na nafasi yake kupewa aliyewahi kuwa Mbunge wa jimbo hilo, Njelu Kasaka. 

Katika kura hizo za maoni, Miraji aliongoza kwa kupata kura 65 akifuatiwa na Kasaka aliyepata kura 45 na nafasi ya tatu kushikwa na Philip Mwakibinga. Taarifa kutoka wilayani humo zinabainisha kuwa tayari Miraji amekimbilia ACT Wazalendo baada ya kukatwa Chadema. 

Pamoja na Miraji, hofu imetanda miongoni mwa viongozi wa chama hicho kwamba huenda akaondoka na kundi la makada waliofanya kazi kubwa ya kukijenga chama hicho wilayani humo. 

Hali sio shwari pia katika Jimbo la Vwawa ambako mwanachama aliyetumia takribani miaka kumi kukijenga chama hicho wilayani Mbozi, akitumia rasilimali zake, Abraham Msyete kufanyiwa fitina pale alipotangaza kuwania nafasi ya ubunge kwenye jimbo hilo kupitia Chadema. 

Kiongozi huyo wa wilaya, aliamua kukaa pembeni baada ya kushindwa kuhimili, vurugu, unyanyasaji na udhalilishaji aliofanyiwa yeye binafsi pamoja na baadhi ya wanachama walioonyesha kumuunga mkono.

 Taarifa za ndani ya chama hicho wilayani Mbozi, zinawanyoshea kidole walinzi wa chama hicho, maarufu kwa jina la “Red Brigade,” ikidaiwa ndio waliokuwa wakiendesha vurugu, kuteka watu na udhalilishaji wa kina mama na wazee. 

Msyete anakiri kujiweka pembeni kutokana na vurugu alizofanyiwa, na kubainisha kuwa pamoja na pendekezo lake la kutaka kuwepo usuluhishi baada mchakato wa kura za maoni ndani ya chama hicho, hakuna kilichofanyika. “

Nilipochukua fomu tu, nikaanza kuambiwa fisadi, mwizi, sifai, wakakumbatia kundi la waliokuja kimaslahi,” anasema Msyete na alipotakiwa kuelezea msukumo nyuma ya baadhi ya wapambe hao wenye kuendesha vurugu dhidi ya baadhi ya wagombea, alisema; 

“Mikataba, watu wanaingia mikataba, kwamba endapo atachaguliwa, udiwani au ubunge, atawapatia vitu kama nyumba, pikipiki au nafasi za uongozi serikalini kama vile ukuu wa wilaya. Unaulizwa, watu wamekupigania, hivi ukishinda wanapata nini? Lazima utoe mkataba!” 

Kwa mujibu wa kiongozi mmoja ngazi ya mkoa, migogoro iliyotokana na uteuzi wa wagombea nafasi za udiwani na ubunge mkoani humo, imekiathiri chama kwa baadhi ya wanachama wake kutimkia vyama vingine, hususan CCM na ACT-Wazalendo, wakionyesha kutoridhishwa kwao na mwenendo wa chama chao. 

Katika Jiji la Mbeya, Katibu wa Chadema mkoa huo, Boyd Mwabulanga, alijikuta katika wakati mgumu pale alipoenguliwa kutetea nafasi yake ya udiwani, Kata ya Forest, baada ya uongozi wa wilaya kutoa barua mbili za uteuzi, huku ikidaiwa mhuri kwenye moja ya hizo barua mbili kughushiwa. 

Mwabulanga alithibitisha kuwepo kwa utata kuhusu kata hiyo akibainisha kuwa ni tatizo lililosababishwa na uongozi wa chama wilaya. 

Wafuatiliaji wa siasa za Jiji la Mbeya, wanakielezea kitendo hicho kuwa mkakati mahsusi ulioandaliwa kwa muda mrefu kumzuia diwani huyo aliyemaliza muda wake, asirudi tena kwenye Baraza la Madiwani linalotegemewa kutawaliwa na Chadema. 

Vyanzo vyetu vya habari vinathibitisha kuwepo kwa mkakati huo na kubainisha chanzo kuwa ni nafasi ya Umeya, ambapo Mwabulanga alihofiwa kuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kukalia kiti hicho. “

Hapa issue ni Umeya, baadhi ya viongozi ndani ya Chadema wanadai iwapo Boyd atakuwa Meya, hawawezi faidika naye, wanataka kuweka mtu watakayemmudu,” anasema mmoja wa madiwani waliomaliza muda wao jijini humo. Chadema tayari wamejipa uhakika wa ushindi katika jiji hilo wakiamini kuwa watafanikiwa kuwa na madiwani wengi zaidi hivyo kuongoza Baraza la Madiwani. 

Chanzo. Raia mwema

No comments:

 
 
Blogger Templates