Na Maggid Mjengwa.
NIPO katika mgahawa wa Neema Craft mjini Iringa. Mzee David Butinini na mimi tumepanga tukutane mahali hapa kwa chakula cha mchana na mazungumzo kuhusu alichokishuhudia miaka 40 iliyopita. Inahusu tukio la mkulima Said Mwamwindi kumpiga risasi aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Kleruu.
Zikiwa zimebaki dakika mbili kabla ya kutimu saa saba mchana tuliyoahidiana, namwona Mzee Butinini akipandisha ngazi za mgahawa. Pamoja na umri wake mkubwa, Mzee Butinini bado anaonekana kuwa na mwili wa kimichezo pia.
Kwa wasiomjua, kwenye miaka ya sitini na wakati akiwa kwenye Jeshi la Polisi, Mzee Butinini alipata pia kuchezea klabu ya soka ya Ushirika ya Mwanza wakati huo ikiitwa Mwanza-Coop. Huyu ndiye baba pia wa wanamichezo mahiri; marehemu Duncan Butinini kwenye soka na Jane Butinini kwenye mpira wa pete.
Namuuliza Mzee Butinini; “Dk. Kleruu alipata kuwatamkia watu wa Iringa, kuwa kama hawamjui wawaulize watu wa Mtwara. Na wewe unasema ulikuwa naye Mtwara kabla hajahamishimiwa Iringa, je, Dk. Kleruu unayemfahamu wewe ni mtu wa namna gani?
“Sikumfahamu Dk. Kleruu kama rafiki, nilikuwa namwona zaidi kikazi. Kikazi nilianzia Masasi, Mtwara. Na nakumbuka akiwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Dk. Kleruu alifika Masasi na kuzungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara. Nilikutana naye pia wilayani Newala. Ni kweli, hata kule Mtwara Dk. Kleruu alionekana kuwa ni kiongozi mkali na mwenye kuhimiza mambo kwa nguvu.
Lakini pia ieleweke hapa, kuwa maeneo kama Newala na sehemu nyingine za Mtwara yalikuwa ni maeneo ya Vita. Itakumbukwa tulikuwa kwenye kuwasaidia ndugu zetu wa Msumbiji hususan Frelimo kwenye mapambano yao ya ukombozi kutoka kwenye utawala wa Wareno. Sasa labda hali kule Mtwara ilikuwa ni tofauti na ilimtaka mtu kama Dk. Kleruu,” anasema Mzee Butinini.
Na umesema kuwa Kleruu alipohamishiwa Iringa nawe ukahamishiwa Iringa pia. Je, Dk. Kleruu uliyemwona Mtwara alikuwa na tofauti gani na Dk. Kleruu uliyekutana naye Iringa?
Niliripoti Iringa mwezi Machi. Nami nilikuwa mgeni pia na mkoa huu wa Iringa. Nilikuwa askari kijana sana pia. Kule Mtwara Dk. Kleruu alikuwa zaidi kwenye kuhimiza wananchi kwenye masuala ya maendeleo lakini zaidi kwenye hali ya kijeshi ikiwamo mambo ya kuchimba mahandaki kutokana na hali niliyoielezea hapo.
Na watu wa Mtwara walikuwa katika hali duni sana kimaendeleo. Mtwara Dk. Kleruu hakukumbana na upinzani katika kutoa amri zake.
Sasa nadhani hapa Iringa Dk. Kleruu alikutana na hali tofauti. Kwa mawazo yangu nadhani Dk. Kleruu kama Mkuu wa Mkoa alipaswa kujiandaa na zaidi kujifunza juu ya mila na desturi za watu wa Iringa. Maana, watu wa Iringa ni watu wa Iringa.
Dk. Kleruu alikuwa kijana mdogo sana kwenye macho ya wazee wa mji huu wa Iringa. Na mji huu wa Iringa ulikuwa na kundi dogo la wakulima wazawa waliokuwa na kipato kikubwa. Ndio waliokuwa wakiijenga Iringa. Hawa hawakuwa wakulima wadogo wadogo. Walikuwa wanamiliki mashamba makubwa sana. Walikuwa wanamiliki magari, malori na matrekta ya kulimia. Mmoja wa wakulima hao ndiye huyu mkulima Said Mwamwindi.
Namuuliza tena; Mzee Butinini, umeaniambia huko nyuma kuwa mara baada ya kupigwa risasi na kuawa kwa Dk. Kleruu kuna wakulima hapa mjini Iringa waliokamatwa na kutiwa nguvuni. Je, inakuwaje wakulima waishi mjini?
Anajibu; Unajua Maggid, Iringa ilikuwa tofauti sana. Wakulima wakubwa wa Iringa walikuwa na mashamba yao pale Isimani. Ni umbali wa kilomita arobaini hivi kutoka hapa. Sasa kule shamba walijenga nyumba za kufikia tu wakati wa msimu. Lakini makazi yao haswa ya kudumu ilikuwa hapa mjini.
Kuna wakulima waliokwenda shamba asubuhi na usafiri wao na jioni walirudi Iringa Mjini. Na kuna ambao mjini hapa walikuwa wamewekeza kwenye shughuli nyingine. Hawa watu walikuwa matajiri hata kwa kiwango cha wakati ule. Walikuwa ni watu wenye ushawishi pia. Walisikilizwa na watu, waliheshimiwa.”
Namuuliza swali hili Mzee Butinini; Mmoja wa wazee nilioongea nao kwa simu na natarajia nitakutana nae kwa mazungumzo ya ana kwa ana ni mkulima Mzee Pesambili na ambaye alikuwa rafiki wa Said Mwamwindi. Huyu bwana ni mmoja kati ya wale waliokamatwa na kuwekwa kizuizini. Je, unafikiri ataniambia nini kuhusu kilichotokea?
Mzee Pesambili is still bitter! Unasikia, huyu bwana ana machungu sana. Na nadhani huenda atafurahi kuongea nawe ili aseme machungu yake. Na wakati nakuja kukutana na wewe, nimemwona anatembea kwa miguu pale Stendi ya Daladala ya Miyomboni. Amevalia pama lake. Hatukusalimiana. Ukiongea nae ujue, kuwa utakutana na mtu mwenye machungu ya yaliyomkuta.
Maana, usiku ule wa tukio aliposikia polisi tunamfuatilia alikimbia makazi yake. Akaenda kukamatiwa Mufindi huko. Na baadae akapelekwa kusikojulikana. Aliporudi akakikuta kiwanja chake pale Kihesa kimechukuliwa. Kimsingi maisha yake yakaharibika. Ari na moyo wa kuendelea na kilimo ikamwishia. Na mifano mingine ya watu kama mkulima Pesambili.
Wakati wa sakata lile, watu waliokuwa wakikamatwa walikuwa wakisafirishwa usiku na ndege ya jeshi. Huko walikokwenda walitawanywa. Hawakukutana. Na huku nyuma mambo yakazidi kuwa mabaya. Unajua Maggid, unapomkamata mzee mwenye mji wake. Kisha akapelekwa mahali ambako ndugu zake hawajui, basi, unawaweka wana ukoo katika hali ya mashaka. Na pengine jamii ambayo mtu huyo aliishi. Tunajua kuwa kuna wenyeji ambao walipinga kilichokuwa kinafanyika. Lakini hofu ilitawala.
Na siku zote, watu ni watu. Hata wakikaa kimya, wanasema katika kimya hicho. Nakumbuka wakati wa operesheni ile kulikuwa na vituo vya usalama kwenye maeneo ya vijijini. Mimi nilipangiwa eneo la Igula. Kwenye vilabu vya pombe wenyeji waliimba kwa mafumbo na kwa lugha yao, nyimbo za kushutumu dola. Lakini, huwezi kumfungulia mshtaka mtu kwa kuimba nyimbo ya mafumbo!
Nikuulize Mzee Butinini; Fikiri kama tukio lile lisingetokea siku ile ya Jumapili ya Desemba 25, 1971, je, Iringa leo ingekuwaje?
Iringa ingekuwa imeendelea sana, lakini hili lingetegemea pia na sera za nchi. Maana, tatizo lingebaki kama sera zingebaki kuwa zile zile. Ukumbuke kuwa Dk. Kleruu alikuwa anaamini anatekeleza sera za Azimio la Arusha za Ujamaa na Kujitegemea. Kwamba kumfuata mtu shambani kwake, tena siku ya Krismasi, kwa Dk. Kleruu aliamini hiyo ni sehemu ya kazi yake ya kuhimiza kilimo. Ingawa, bado ni kitendawili, kwa nini afanye hivyo siku ya Krismasi?
Na nadhani ugomvi mkubwa kati ya Dk. Kleruu na wakulima wakubwa wa Iringa ulikuwa kwenye sera ya kuchangia mashamba. Haya mambo ya mashamba ya ushirika. Dk. Kleruu alishindwa kwenye right approach kwa maana ya msogeleo sahihi kwa wenyeji katika kuifanya kazi yake.
Sasa basi, hata kama Mwamwindi asingefanya tendo lile baya la kuua, bado, mazingira ya wakati ule yangefanya kuwepo na mgongano mkubwa kati ya wakulima wakubwa na watawala. Na hili kwa kweli lilijitokeza mahali pengi hapa nchini.”
No comments:
Post a Comment